Hilo ndinga la Mondi usipime!

Muktasari:

AKIWA hata hajapona kwenye sakata lake la kuwania tuzo za BET, mkali wa muziki wa kizazi kipya nchini, Diamond Platnumz a.k.a Chibu siku tatu zilizopita aliibua gumzo baada ya kuanika gari la kifahari aina ya Cadillac Escalade Sky Captain.

AKIWA hata hajapona kwenye sakata lake la kuwania tuzo za BET, mkali wa muziki wa kizazi kipya nchini, Diamond Platnumz a.k.a Chibu siku tatu zilizopita aliibua gumzo baada ya kuanika gari la kifahari aina ya Cadillac Escalade Sky Captain.

Hili ni ndinga kali ambalo limekuwa likitumiwa na mastaa kibao duniani, lakini Mond ni kama kawasapraizi mashabiki wake, ambao kwa sasa huko mtandaoni imekuwa gumzo kubwa.

Moja ya sifa kubwa ya gari hilo ni ukiachilia gharama kubwa katika kulinunua pia halipenyi risasi na hapo ndipo Mond ama Dangote akithibitisha madai yake kwamba, akaunti yake ina umatemate wa kutosha, sema watu wanamchukulia poa tu, kwa vile amekulia Tandale!

Kwa mara ya kwanza picha za gari hizo zilimuonyesha mtoto wa Diamond, Nillan ambaye hivi karibuni amewasili nchini akitokea Afrika Kusini na Mama yake, Zari The Bosslady, akiwa ndani ya gari hilo.

Awali katika ujumbe ambao amewekwa kwenye ukurasa wa Instagram wa mtoto huyo, umeashiria kuwa staa huyo wa kimataifa wa muziki nchini, ndiye mmiliki wa gari hilo, japo mwenyewe pamoja na menejimenti yake hawajadhibitisha hilo.

Licha ya kuwepo kwa usiri juu ya ndinga hilo, kwa wahusika kushindwa kufunguka licha ya kusakwa mara kadhaa, lakini ukweli ni kwamba kwa wiki nzima na katika nyakati tofauti Diamond pamoja na familia yake wameonekana wakiwa katika gari hilo akiwemo dada yake Esma ambaye ameonekana pia kulitambikia.


GARI YA AINA GANI?

Cadillac Escalade Sky Captain ni gari la aina gari hasa na sifa zake ni zipi? Huenda hilo ni swali linalosumbua vichwa vya wengi ambao wasiojua ndinga hilo la kisasa.

Ukiachana na uwezo wa kutoruhusu risasi kupenya, pia ni automatic, ukikanyaga mafuta chini ya sekunde sita itatoka ziro hadi 60 kwa saa. Hii ikiwa na maana ili ulimiliki ni lazima akaunti yake iwe imenona na usiwe na maisha ya kuungaunga, kwani unaweza ukashindwa kulihudumia.

Kama hujui ni kwamba gari hili la mwaka 2016, ndani kuna friji la kuhifadhi vinywaji na matunda, pia kuna Air Condition (AC) inayoweza kugundua hali ya hewa na kubalansi ubaridi au joto kulingana na mazingira ulipo, pia kuna ya TV nchi 48.

Kadhalika ndinga hiyo matata, pia ina meza za mtindo wa ndege ambayo imezungukwa na dhahabu ya karati 24. Kuta zake ni laini na madirisha yana mapazia ya faragha.

Ina skrini mbili za inchi mbili za kufuatilia kinachoendelea nje ya gari ambapo aliyeko ndani ataweza kuoana mandhari yote ya nje kirahisi kabisa.

Aidha lina iPad zilizounganishwa Mac Mini na yenye uwezo wa kufanya mkutano kwa njia ya video (zoom).

Kama ilivyo kwa mifano mingine ya magari ya kifahari, abiria wanaweza kudhibiti mfumo mzima wa burudani kwa kutumia skrini (touchscreen) ya kugusa kwenye kiti cha mkono wake. Pia gari hili kama hujui katika orodha ya magari saba ya starehe duniani linashika nafasi ya tano na ukiwa ndani unajihisi kama upo kwenye ndege.


BEI YAKE SASA

Bei ya gari hilo inakadiriwa kuanzia Dola 350,000 hadi 500,000 sawa na Sh811 Milioni hadi 1.15 Bilioni fedha ambayo kwa harakaharaka ndio bajeti ya mfuko wa Sanaa ya Utamaduni iliyotengwa kwa mwaka huu kwa ajili ya wasanii wetu.

Ikumbukwe, Diamond anagonga tena vichwa vya habari na gari hilo mara baada ya hivi karibuni kuibuka tetesi kuwa amenunua ndege kitu kilichofanya baadhi ya mashabiki kuhoji kuhusu mpango wa msanii huyo kudai ananunua gari aina ya Rolls-Royce Dawn.


NI JIPYA AU MTUMBA

Haya ndio maswali yanayowasumbua watu huko mitandaoni, ambapo badhi wanasema kuwa gari hilo ni mtumba (used) na amenunua kwa mmoja wa watoto wa mfanyabiashara mkubwa hapa nchini na kulifanyia ukarabati.

Hata hivyo watu wake wa karibu wanalipinga hili na kusema jamaa kaliagiza kutoka nje na ni jipya kabisa, huku bei yake kwa mujibu wa mtandao ikionyesha linashika nafasi ya saba kwa kuwa ghali duniani.

IMEANDALIWA NA PETER AKARO KWA MSAADA WA MITANDAO