He! Kisa bodaboda ndo umtose, we dada vipi?

Msikie huyu... Mi naona huyu dada anachekesha sana. Ila kwa majibu ya Anko Lao nadhani atakuwa ameelewa cha kufanya.
Alichouliza: "Anko Lao, nina mpenzi ninayempenda sana ila shida iliyopo, mimi sipendi kazi anayoifanya ya kuendesha bodaboda. Nifanyeje?
Irene, Dar
Jibu: Hadi unamzimikia hukujua kazi anayoifanya au unajishaua tu? Halafu kitu gani kinakufanya uichukie kazi ya bodaboda, wakati hiyo ni kazi kama kazi nyingine inayomuingizia jamaa michone iliyokuzuzua hadi ukajibebisha kwake. Mwache mwenzio apambane, si unajua ajira zenyewe ni shida?
Wengi wamekumbwa na masahibu yao kwenye maisha ikiwamo ya uhusiano na mengine. Anko Lao ana majibu yao. Cheki hapa.
1. ANKO Lao, kijana miaka 23, nimekaa na mwanamke kwa zaidi ya mwaka mmoja na hatujafunga ndoa, nilitaka kwanza anibebee ujauzito ndio tufunge ila naona hamna kitu. Sasa sijui shida nini?
Abdul Kimaro, Dar
Jibu: Nyie ndio mnaoitwa vijana wa hovyo kwa kufanya mambo ya kiduwanzi, yaani badala ya kuoa unaishia kujifanya testa...Kama hujui tatizo ni wewe, kudunga mimba sio kazi rahisi kama unavyodhani. Ushauri wangu nenda kajicheki mapema ili usije ukafungisha huko mbele ya safari!
2. ANKO Lao, kijana miaka 35 nina mke tunayependana sana, lakini hataki kunizalia mtoto. Nifanyeje?
Charles Mkemia, Tanga
Jibu: Hivi unajua mke wewee au unajisemea tu...huwezi kuimAliza njaa bila ya kula, haiwezekani kama kweli wewe ni mume, usijue majukumu yako kama kichwa cha nyumba badala yake unasubiri hisani za mkeo! Ukiendekeza huo uduwanzi, ujue kabisa itakula kwako mazima! Chakarika upate pointi tatu!
3. ANKO Lao, kijana miaka 28 nina mke niliyezaa naye mtoto mmoja ila shida inakuja kwa wazazi hawataki nikae naye, kwa sababu nafanya ibada Roma halafu wao ni Waislamu. Nifanyeje?
Benjamin Peter, Kahama
Jibu: Hivi unajua maana ya mke wewee au unakurupuka tu? Kuwa mke na mume sio kitu rahisi kama unvyofikiria, ndo maana wazazi wanakuzingua...Wanakuona ni mhuni kama wahuni wengine tu, kwani haiwezekani unajimegea kisela, halafu unajiona we ni mume. Cha kufanya ni kufanya chapu ili mfunge ndoa kwa mmoja wenu abadili dini ili mlee mtoto, la sivyo kila mtu ale kona yake!
4. ANKO Lao, naishi na mama wa kambo na kwa kweli ananitesa sana, ila nashindwa kumwambia baba yangu. Nifanyeje maana naumia?
Neyratty Issa, Dar
Jibu: Sijajua umri ulionao, ila sidhani kama unateswa bali nahisi unaleta zile simulizi zinazowatia ubaya mama wa kambo...kwani kama ni kweli, ni wazi jamii inayokuzunguka ingejua na kuchukua hatua hata kama we unaogopa kumtonya mdingi. Ila ni vyema ukaishi na huyo mama hata kama hajakuzaa kwa heshima na adabu ili maisha yawe freshi, usilete ununda...ukizingua utazinguliwa!
5. ANKO Lao, kijana miaka 30 ila tatizo langu kila nikitongoza nakataliwa, kwani mara ya mwisho kupendwa ilikuwa 2017. Nitakuwa na shida gani?
Julius Laizer, Arusha
Jibu: Tatizo lako huna swaga na vilevile unaonekana unasikilizia sana fedha zako... hata kama ni kweli una pesa za mawazo, lakini siku moja moja lainisha mambo ule raha, si unajua hakuna mkate mgumu mbele ya chai. Pia kumbuka maisha yenyewe mafupi, jipe raha na utamu uoe kabisa. Hivyo tu!
6. ANKO Lao, nina miaka 27 na natamani sana kuwa tajiri mkubwa, japo najua ni ndoto kubwa ila je nidhamu ya kipato changu ndiyo itakayonifanikishia hilo au kuna lingine la kuzingatia?
Thomas Ntahindwa, Kigoma
Jibu: Utajiri hautamanwi, ila unatafutwa! Kitu cha kufanya pambana kwa njia ya halali kupiga kazi na Mungu ataleta neema zake, ukiishia kutamani tu, utaishia kwenye kusaka utajiri kwa njia ya mkato na kushindwa kuinjoi maisha. Utajiri wa masharti ni noma sana. Kazi kwako!
7. ANKO Lao, kijana miaka 20 kuna mwanamke wa miaka 40 nampenda ila ananipiga sana vibomu na sina malengo naye. Nifanyaje?
Juma Kilaza, Muheza
Jibu: Tamaa ya kupenda mishangazi kwa kuamini ina hela ndio iliyokuponza...halafu kwa umri huo kushobokea vibibi ni kujitia mikosi bure, ndio maana unaishia kulalama kupigwa mizingi, ulitumwa?!
8. ANKO Lao, kijana wa miaka 30 ila wakati nina 25 nilipata mtoto na demu mmoja hapa mtaani, lakini kila nikitaka kumuona mtoto ananikatalia, licha ya kutoa matumizi. Sijui tatizo na nifanyeje?
Masoud JR, Mwanza
Jibu: We umezingua, ulipaswa kabla ya kubebeshana mizigo ungeend akujitambulisha kwao na kuoa kabisa, haya yasingekukuta. Unabaniwa kwa vile unaonekana ni mhuni tu kama wahuni wengine. Jipange, ulee damu yako!
9. ANKO Lao, nina mpenzi anayenipenda sana ila tuko mbali, lakini shida yake kila akinitafuta lazima aombe hela yaani hadi namchoka. Nifanyeje?
Khamis Kalengo, Jaribu
Jibu: Punguza makasiriko, maji ukiyavulia nguo huna budi kuyaoga...ulipoamua kujitosa kwenye malavidavi, ulishaamua kubeba mzigo huo wa kupigwa mizinga...hujui kama starehe gharama? We vipi?!
10. ANKO Lao, nina miaka 25 na mpenzi tunayependana sana ila shida yake ni wivu uliopitiliza yaani inakuwa kero. Nifanyeje?
Amina, Dar
Jibu: Wasiwasi ndio akili na siku zote tunakumbushwa abiria chunga mzigo wako...huyo jama'ako bado haamini kama anamiliki pisi kali kama wee, ndo maana analeta hizo, ila sema naye mwambie atulize akili...kwanza hajakuoa hivyo asikuletee uduwanzi wa hivyo, pia mhimize akuoe asikuchezee kiboya!
11. ANKO Lao, kijana miaka 27 na kila nikiwatokea wasichana wananikubalia ila shida ni kupiga shoo yaani visingizio vinakuwa ni vingi wakati maokoto natoa. Nifanyeje?
Abi Nassoro, Kibaha
Jibu: Ni wazi we bado unaishi enzi za ujima, aliyekuambia ukiimbisha na kudakisha, utaungishwa? Hao mademu wameshakuona we ni boya ndio maana wanakula vyako kisha wanatembea...cha kufanya tafuta pisi moja kali utakayoielewa, peleka posa uoe ule raha kuliko kuchunwa bila faida!
12. ANKO Lao, kijana miaka 28, nimeoa lakini tatizo wazazi wangu na wale wa mke wangu hawaelewani. Nifanyeje ili kuwapatanisha?
Mponda Adiche, Ilela
Jibu: Sijajua kitu gani kinachowafanya wazazi wenu wasielewane, ila ni wazi ndoa baina yenu kuna upande haikuiridhia ndo maana leo yanatokea hayo. Ni ngumu we kuweza kuwapatanisha, ila jaribu kushirikisha wazee wenye busara zao, wawapatanishe la sivyo hiyo ndoa yenu itakuwa rehani!
13. ANKO Lao, kijana miaka 20, nipo kwenye uhusiano lakini kila siku nimekuwa ni mtu wa mawazo. Nifanyeje niepukane na hali hiyo?
Chado Mganda, Msasani
Jibu: Ni wazi umeyakurupukia malavidavi bila hata ya kujiandaa wala kujua ni pasua kichwa hasa kama ukiingia pabaya. Kitu cha kufanya ni kupima kwani kuna ulazima wa kuendelea na uhusiano huo au unaweza kujiongeza, ila kumbuka tu...jogoo hafi kwa utiriri, ukiweza jikaze maisha yaendelee!
14. ANKO Lao, binti miaka 23 nimeolewa na nina mtoto mmoja, ila mume wangu anapenda kusikiliza maneno ya kuaambiwa na nduguze badala ya mie mkewwee, wakati uhusiano wetu ulianza tangu nikiwa shule, kiasi nilikataa kwenda chuo kwa ajili yake, leo naona amenibadilikia. Nifanyeje?
Neimah Ayoub, Bagamoyo
Jibu: Pole kwa changamoto unazopitia, ila jitathmini...huenda kuna mambo unayafanya hadi mumeo kukubadilikia. Jirekebishe kisha ishi kwa raha maadam we ni mke halali. Kitu muhimu upunguze mdomo, ishu ya kukacha chuo kwa ajili ya jamaa, ni uduwanzi wako, lakini zungumza na jamaa ajue ameshaoa na anapaswa kuendeshwa kwa akili yake na sio akili za kushikiwa. Hivyo tu!
15. ANKO Lao, binti miaka 19, kuna boy tunapendana, ila ana mtoto nmini sina na anasema anataka kunioa. Nifanyeje?
Vero Zakayo, Kigoma
Jibu: Sijajua msingi wa swali lako, maana umenichanganyia mada, kwani jama'ako kuwa na mtoto inakuzuia kuolewa? Halafu nini? Kabla ya kushobokea ndoa, jiulize aliyezaa na msela kilimtokea nini hadi wakatemana? Isije jamaa kakuingia na gia ya ndoa ili akunase kisha aje akuache solemba. Kuwa makini, mayanki wa zama hizi hawasomeki na wepesi wa kulitibua! Kazi kwako!
16. ANKO Lao, binti miaka 20, kuna boy tunapendana sana, lakini tatizo lake ana wivu sana, kwani hata akiniona naongea na rafiki zangu wa kike au kiume anawaka. Nifanyeje?
Neema Elisha, Mwanza
Jibu: Hili ndilo tatizo la kulavidika bila kujuana vyema, kwani jiulize tu, hapo hajakuoa ana wivu kama nyegere, vipi akikubeba jumla, si anaweza hata kukuzuia kusalimia majirani? Kaa naye chini umwambie aache miyeyusho yake, ajiamini na awe na amani nawe!
17. ANKO Lao, binti miaka 18 nina mpenzi mwenye umri kama wangu, hana pesa wala kazi kiasi anashindwa kunihudumia, lakini amejitokeza kijana mwingine aliyepo chuo na anauza duka la nguo na ananihudumia ikiwamo kunitoa outing. Nifanyeje?
Angela Kasimba, Tabora
Jibu: Kwa umri ulionao na kasi uliyoanza nayo ujue mapema utachakaa, kwani unaonekana unatawaliwa na tamaa na si unajua tamaa mbele mauti nyuma...? Jitulize, ikiwezekana pambana kwanza kuitafuta kesho yako kuliko hicho unachokifanya sasa, kwani siku zote majuto ni mjukuu!
18. ANKO Lao, kijana miaka 18 nipo kwenye uhusiano na binti wa jirani na kwa sasa amenasa mimba anayotaka kuitoa wakati mie namkataza na hataki kunisikia. Nifanyeje?
Simon, Kigoma
Jibu: Umezingua sana kulimsha goma kabla ya kuoa, kwani kwa umri ulionao ulipaswa kwanza kuipambania kesho yako badala ya kushobokea malavidavi...ndo maana mwenzio amepagawa akitaka kuflashi. Cha kufanya jisalimishe kwa wakwe uombe msamaha, kisha fanya chapu uoe, mambo yasiwe mengi. Hivyo tu!
19. ANKO Lao, nina umri wa miaka 26 nimeolewa na nina mtoto wa miaka miwili tunaishi kwa wakwe zangu, tatizo mwenzangu mwenye tunayelingana umri, nikimshauri tuhame tukakae mbali na wazazi wake inakuwa ugomvi, kwani hataki kabisa. Nifanyeje maana nimechoka?
Tumain Mwinuka
Jibu: Ulibugi sana kukubali kuolewa kabla hujamsoma vizuri, huyu jama'ako ni wale watoto wa mama ambao ni waoga wa maisha na wanaopenda kitonga. Barubaru aliyekamilika hawezi kuoa na kuishi kwao. Zungumza naye kwa upole ajue anavyojichoresha kinoma na mweleze hawezi kukua kama anaendelea kutegemea nyumba ya wazazi, atoke hapo akapambane naye kutafuta vyake! Hivyo tu.