Harmonize kunogesha tamasha la Rais Samia Mbeya

Mbeya. Msanii wa bongo fleva, Rajabu Abdul ‘Harmonize’ anatarajia kusimamisha Mbeya kwenye matukio mawili tofauti ikiwamo tamasha la mafanikio ya miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza leo Machi 16, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema katika kuazimisha miaka miwili ya mafanikio ya Rais Samia, Harmonize ndiye atatumbuiza katika tamasha hilo litakalofanyika Jumamosi kwenye viwanja vya Ruanda Nzovwe.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera

Amesema kabla ya Jumamosi, itaanza kongamano litakalofanyika kesho Ijumaa ambalo litakuwa ni kuelezea mafanikio ya kimaendeleo aliyofanya Rais Samia mkoani Mbeya.

“Katika tamasha hili mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, huku msanii Harmonize akitarajia kutumbuiza kwenye tamasha hilo kisha atafunika kule wilayani Chunya yanapoendelea maonesho ya madini,” amesema Homera

Homera ameongeza kuwa ipo miradi mingi ya maendeleo iliyotekelezwa na Rais Samia kwa miaka miwili ikiwa ni barabara, afya, maji na elimu na kwamba lazima wananchi wajivunie.

“Kuhusu barabara nne tayari mkandarasi amewasili Mbeya kuanza kazi, vivyo kwa upande wa mradi wa maji mto Kiwira, haya yote ni sehemu ya mafanikio ikiwamo hospitali ambapo MSD wanaanza kuleta vifaa,” amesema.