HAMAHAMA: Wasanii hawa hawatulii bendi moja
Muktasari:
- Hamahama hii ya wanamuziki huwavuruga wamiliki wa bendi na pia kuzisababishia bendi nyingi kukosa uimara wa kudumu.
KUHAMA kutoka bendi moja kwenda nyingine ni jambo ambalo limekuwa kama tabia kwa baadhi ya wanamuziki wa dansi, huku wengine wakidumu muda mrefu katika bendi moja au kuhama mara chache tena pale wanapolazimika tu kutokana na mazingira.
Hamahama hii ya wanamuziki huwavuruga wamiliki wa bendi na pia kuzisababishia bendi nyingi kukosa uimara wa kudumu.
Kuhama sio ishu hasa kwa mwajiriwa, lakini kali ambayo huzua gumzo zaidi ni pale msanii walioitumikia bendi fulani kwa miaka mingi, kisha wakahama ili kwenda kuanzisha bendi zao, lakini ghafla wakazihama bendi zao na kurudi walikotoka ama kwenda kwenye bendi zinazomilikiwa na watu wengine.
Ally Choki aliwahi kuhama African Stars ‘Twanga Pepeta’ na kwenda kuanzisha bendi yake ya Extra Bongo, lakini baadaye akaiacha na kurudi African Stars Entertaimen (ASET).
Vivyo hivyo kwa Muumin Mwinjuma ‘Kocha wa Dunia’, alipita katika bendi kadhaa ikiwamo African Revolution ‘wana Tam Tam’ kabla ya kuja kuhama na kwenda kuanzisha bendi yake ya Double M Sound kisha akaicha bendi yake na kwenda kufanya kazi katika bendi kadhaa.
Khalid Chokoraa, Jose Mara na Kalala Junior waliondoka katika bendi zao Twanga Pepeta na FM Academia na kwenda kuanzisha bendi yao ya Mapacha Watatu.
Hata hivyo, Chokoraa na Kalala Jr wakarejea Twanga.
Hii imejirudia wiki hii. Papii Kocha na Msafiri Diouf wamezihama bendi zao mpya ambazo walikwenda na kuwa viongozi na kurudi walikotoka.
Na sio hao tu wapo wengine kama Dogo Rama, Mulemule FBI na wengine wengi ambao wamehama bendi zao na kwenda bendi nyingine katika nenda-rudi.
Mwanaspoti limezungumza na wasanii hao wa dansi kutaka kujua ‘nenda rudi’ hizo za kwenye bendi sababu ni nini.
Msafiri DioUf
Msafiri Diouf aliachana na bendi ya Twanga Pepeta Aprili 2024 na kwenda kuanzisha bendi aliyoipa jina la VDS ‘Chama la Wana’.
Mwanaspoti liliwahi kuongea na Diouf baada ya kuchana na Twanga Pepeta, bendi ambayo aliitumikia kwa muda mrefu na kwenda kuanzisha bendi yake ya VDS ambapo alisema kuwa, ameondoka Twanga Pepeta kwa hiyari yake na sio kwamba amefukuzwa, ila amejiona amekua hivyo anahitaji kujiongoza.
Lakini Novemba 7, 2024 Diouf alionekana kwenye jukwaa la Twanga Pepeta walipokuwa wakifanya shoo kwenye ukumbi wa Small Planet, Tabata Dar es Salaam.
Mwanaspoti lilimuuliza Diouf kulikoni jukwaa la Twanga na vipi kuhusu bendi yake ya VDS, ambapo alisema: “Mimi Twanga Pepeta ni nyumbani, kurudi nyumbani sio kosa. Na uzuri wakati naondoka Twanga Pepeta nilipewa baraka zote na Asha Baraka na hata kwenye kusajili bendi yangu ya VDS Asha Baraka alichangia kunipa msaada.
“Kuhusu VDS Band ‘Chama la Wana’, sina jibu kwasasa, kikubwa kazi iendelee Twanga Pepeta.”
Papii Kocha
Jina lake kamili ni Johnson Nguza ‘Papii Kocha’. Ni mtoto wa nguli wa muziki wa Dansi nchini; Nguza Viking au Babu Seya. Baada ya kutoka jela Desemba 9, 2017, Papii alikuwa mwanamuziki wa kujitegemea huku akiendelea na shughuli zake nyingine.
Ilipofika mwaka 2021 alikuwa mmoja wa waanzilishi wa bendi ya Tukuyu Sound akiwa kama Mkurugenzi wa bendi hiyo akishirikiana na Kalala Junior mtoto wa mwanamuziki Mkongwe Hamza Kalala.
Tukuyu Sound iliendelea kufanya vizuri hadi ilipofika Agosti 2023, Papii aliachana na bendi ya Tukuyu Sound na kujiunga na bendi ya Town Classic kuwa kiongozi wa bendi kwa lengo la kuongeza nguvu katika bendi hiyo.
Mwanaspoti lilipata kuongea na Papii na kumuuliza kulikoni ameihama bendi ya Tukuyu ikiwa bado ipo ya moto yaani inafanya vizuri, ambapo alisema lengo ni kwenda kuboresha zaidi Town Classic na pia kutoka na kupewa pesa nyingi kutoka kwa aliyekuwa bosi wa bendi hiyo Patrick Kessy ‘Kilimo Kwanza’ (ambaye baadaye alifariki dunia Novemba 2023).
“Watu saa hizi wanaangalia pesa Rhobi, mtu unaletewa pesa nyingi na kutimiziwa mahitaji yako yote unayotaka utakaa kuhama bendi? Hizi bendi zipo tu hatufanyii kazi sifa, tupo kutafuta pesa. Sasa bosi alinipatia pesa niende kuongeza nguvu kwenye bendi yake Town Classic kwanini nikatae?” alisema Papii wakati huo.
Sasa katikati ya wiki hii Novemba 25, 2024 kwenye ukurasa wa Instagram wa Town Classic Band imewekwa taarifa ya Thank You kwa Papii Kocha na kuandika ujumbe uliosomeka kuwa: “Papii Kocha amewaaga mashabiki wa muziki wa dansi na wadau wa Town Classic.”
Wakati huo huo kwenye kwenye magroup ya Dansi ya WhatsApp, Papii ametuma taarifa kwa umma iliyosomeka: “Taarifa kwa umma, Mimi Papii Kocha kuanzia leo tarehe 25, Novemba 2024, nimeondoka rasmi Town Classic Band, ila nitaendelea kuwa mwanafamilia, nawashukuru wadau na mashabiki wangu wote ambao mmekuwa pamoja na mimi kwa kipindi chote nilichotumikia Town Classic Band
“Pia nawashukuru wanamuziki na uongozi wa Town Classic Band, kwa kunipa ushirikiano tangu nilipojiunga na Town Classic Band, nawatakia kila la kheri na Mungu awaongoze katika kutimiza malengo, Papii Kocha Novemba 25 2024.”
Mwanaspoti lilimtafuta Papii kuzungumzia hili ambapo amesema ameachana na bendi hiyo kiroho safi na ameamua kupumzika tu.
Mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Nyoshi El Saadat amesema wasanii wengi kuhama ni tamaa tu.