HADITHI: Laana ya Fedha (sehemu ya 04)

Muktasari:
- Wakati nafika nyumbani nikaliona gari la Alhakim lipo barazani. Nikashituka sana. Miguu ilinitepeta kwa hofu. Nusura ningeanguka chini...
“KWA kweli sikumpenda, kwanza mzee sana.”
“Lakini ana pesa?’
“Pesa anazo. Ameniambia ataninunulia gari na hivi karibuni tutakwenda kufanya shopping Zanzibar kwa ndege.”
“Walichokosea wazazi wako ni kwamba hawakutaka kufahamu mawazo yako. Kwa vile wao ni wazazi wakaona watoe wao uamuzi.”
“Hilo ni kosa lakini siwezi kuwalaumu kwa sababu hivi sasa baba yangu hafanyi kazi lakini analipwa mshahara kila mwezi na Alhakim na ni kwa sababu yangu.”
“Sasa, hivi alivyokuona huku anahisi ni kwa nani wako?”
“Nadhani anashuku kuwa nina mtu wangu huku.”
“Akitugundua itakuwa vipi?’
“Sitaki agundue, ndiyo maana nimemkimbia na siku atakaponiuliza nitamwambia nilikuwa naenda kwa shangazi yangu.”
“Sasa utakuwa unafika huku kiwizi wizi tu?’
“Ndiyo hivyo.”
Macheo akatikisa kichwa kusikitika.
“Siwezi kuingilia uamuzi wa wazazi wako lakini ulichonieleza kimenisikitisha na kimeenda tofauti na matazamio yangu.”
“Matazamio yako yalikuwa nini?”
“Matazamio yangu si kuachana na wewe bali kukuoa tuishi tuzae watoto.”
Macheo aliponiambia hivyo aligusa ndoto zangu nikahisi moyo wangu ukipatwa na simanzi.
“Ndiyo hivyo,” nikamwambia huku nikihuzunika.
“Nafahamu itafika mahali nitakuwa sikuoni tena.”
“Hapana. Hata kama nitaolewa, kwako nitafika tu iwe iwavyo.”
Ingawa ulikuwa ndio ukweli wangu lakini nilitaka kumpa moyo Macheo baada ya kumuona akisikitika sana.
“Suala la maslahi nalo limegusa hapo.”
“Ni kweli,” nikamkubalia.
“Kuna kitu sikukielewa. Huyo mtu atakuoa wakati huu unasoma au…?”
“Anasubiri nimalize masomo.”
“Lini?”
“Hapo nitakapomaliza.”
“Kwa hiyo unataka uniambie kwamba ukienda kidato cha tano na cha sita atakusubiri tu?”
“Wao wana imani kuwa mwisho wangu ni kidato cha nne tu.”
“Kwa hiyo ukifaulu huendelei na masomo?”
“Nani? Nitaendelea na masomo. Anayetaka kunisubiri atasubiri akikata tamaa shauri yake.”
“Mara nyingi uchumba wa hivyo si mzuri. Lolote liinaweza kutokea hapo katikati.”
“Nalitokee tu, unioe wewe mpenzi wangu.”
“Siwezi kushindana na huyo mzee. Labda ashindwe mwenyewe.”
Siku zote ninapokwenda kwa Macheo ninashinda kutwa nzima, siku ile niliondoka mapema kwa sababu ya Alhakim.
Nilimwambia Macheo asinisindikize kwa kuhofia tungeweza kukutana na Alhakim akiendelea kuranda na mitaa kunisaka. Yule baba ana wivu si mchezo!
Nilitembea huku nikiangaza kila upande hadi nikafika kwenye kituo cha daladala nikasubiri. Daladala ilipofika nikaondoka.
Nikiwa ndani ya daladala nilikuwa nikimuwaza Alhakim, mtu ambaye alikuwa katika safari ya kuwa mume wangu. Tukiwa katika uchumba tu alikuwa tayari kupoteza muda wake kunichunguza mimi, atakaponioa itakuwa vipi? Nikawaza.
Kwa kweli alishaanza kunitia hofu. Nilichogundua ni kuwa Alhakim alikuwa na wivu mkali au niseme wivu uliopitiliza.
Niliwaza kwamba nitakapokuwa mke wake sitaruhusiwa kutoka nyumbani peke yangu. Na kama nitalazimika kutoka peke yangu ni lazima atakuwa akinifuata nyuma nyuma ili kuona kama nilikuwa ninakwenda safari niliyomuaga au ninakwenda safari nyingine.
Hayo hayakuwa maisha yaliyokuwa akilini mwangu, maisha ya kufuatana na mume kila mahali. Nitakuwa kama mtumwa wake nisiye na uhuru wa kuamua pa kwenda.
Kibaya zaidi ni kuwa Alhakim huyo huyo ndio amekuwa tegemeo kwetu. Wazazi wangu wanaona akinioa yeye ndio watakwamuka kiuchumi, ndiyo tutapata maendeleo, ndio maisha yangu na yao yatakuwa mazuri. Sikuwa na shaka yoyote kwamba hayo masuala ya wivu wake hayakuwa na uzito kwao.
Wakati nafika nyumbani nikaliona gari la Alhakim lipo barazani. Nikashituka sana. Miguu ilinitepeta kwa hofu. Nusura ningeanguka chini.
Niliwaza Alhakim amefutana nini nyumbani kwetu baada ya kunikosa kule alikokuwa akinifuata? Amefika kwetu kunishitakia au kunisubiri aniulize ni kwanini nilimchenga?
Makubwa! Badala ya kuingia nyumbani kwa kutumia mlango wa mbele, nilitumia mlango wa nyuma ambao Alhakim alikuwa hautumii.
Uwani sikukuta mtu nikaingia ukumbini ambako pia sikukuta mtu lakini nilisikia sauti ya baba akiongea sebuleni. Nikaingia chumbani kwangu kimya kimya.
Nilibana mlango kisha nikalala kitandani na kuendelea kuwaza.
Mara nikaisikia sauti ya mama ukumbini.
“Sikumbuki kama yumo au hayumo kwa sababu aliniambia anakwenda kwa mama yake mdogo anaumwa.” Nikamsikia mama anasema uongo kunitetea.
Hapo hapo mlango wa chumbani kwangu ukasukumwa nikafumba macho yangu kama vile nilikuwa nimelala.
Nikamsikia mama akiniita. “Esma…!”
Nikafumbua macho yangu na kumuitikia.
“Abee…!”
“Umelala muda huu?”
“Kichwa kinaniuma.” Nikasema uongo.
“Basi lala kama kichwa kinakuuma. Alhakim alikuwa anakuulizia.”
Mama akafunga mlango. Nkamsikia akisema huku akitembea ukumbini.
“Kumbe amelala…kichwa kinamuuma.”
Baada ya hapo sikuisikia tena sauti yake.
Sikuweza kufahamu Alhakim alipoambiwa nipo alisema nini wakati aliniona kule Tabata.
Niliendelea kubaki chumbani mpaka niilipolisikia gari la Alhakim limewashwa, ndipo nikatoka chumbani.
Nilikwenda uani nikamkuta mama akifua nguo.
Kwanza nilikwenda msalani, nilipotoka nikachukua mbuzi ya kukunia nazi na kwenda kukaa karibu yake.
“Kichwa kimetulia,” akaniuliza akiamini kuwa kweli kichwa kilikuwa kinaniuma.
“Kimetulia.”
“Ulikuwa umekwenda wapi na ulirudi saa ngapi?’
Kwa kudhani kwamba huenda Alhakim aliwambia kuwa aliniona Tabata, nikaona niseme ukweli kuwa nilikwenda huko.
“Nilikwenda Tabata kuchukua kitabu changu.”
“Kitabu cha nini?”
“Kitabu cha shule, nilimuazima mwananfunzi mwenzangu na kesho kinatakiwa shule.”
“Mbona hukuaga kama unakwenda Tabata?”
“Nilipomndoka hapa nyumbani sikuwa na wazo la kwenda huko. Nilikwenda mtaa wa pili kwa rafiki yangu. Sasa nikiwa huko ndiko nikapata wazo la kwenda Tabata.”
“Unazunguka sana mwanangu wakati umeshakuwa mchumba wa mtu.”
“Hata kitabu changu nisikifuate kwa sababu nimekuwa mchumba wa mtu!”
“Unadhani mwenyewe akikuona atafikiri nini?”
“Kwani amesema ameniona?”
“Hakusema hivyo lakini nakuuliza mimi kama akikuona atafikiri nini?”
“Afikiri nini kwani ameshanioa?”
“Hata kama, inakupasa uweke heshima na heshima ya mwanamke ni kutulia nyumbani kwao.”
“Sasa subiri nikwambie kitu mama. Huyu mzee ana tabia ya kunifuata fuata anaponiona.”
“Alikufuata wapi?”
“Ni mara nyingi. Ninaweza kuwa natembea nikashitukia ananifuata na gari lake. Hii leo pia alinifuata hadi Tabata nikamchenga.”
“Unasema kweli?”
“Nasema kweli. Ana tabia ya kunifuata fuata.”
“Si nimekwambia acha tabia ya kuzurura zurura. Anaweza kukuona. Sasa kama hivyo unavyosema amekufuata hadi Tabata na ndiyo maana alifika hapa na kukuulizia.”
“Lakini hakusema kama aliniona?’
“Hakusema, labda alitaka tu kufahamu kama umesharudi.”
“Sasa maisha haya ya kufuatana hadi lini?”
“Yule ni mwanaume lazima akufuate fuate, afahamu nyendo zako.”
“Sasa hapo atakaponiona si itakuwa shida.”
Inaendelea...