Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HADITHI: Laana ya Fedha (sehemu ya 03)

Muktasari:

  • Nikaondoka haraka katika eneo hilo. Nikiwa katika mtaa mwingine sasa nikielekea katika kituo cha daladala. Nikaliona tena gari la Alhakim nyuma yangu. Nikagundua kuwa Alhakim alikuwa akinichunguza.

ALHAKIM aliponishusha karibu na nyumbani kwetu nilijua nilimuudhi. Hapo nilipata fundisho la kutomuita babu katika maisha yangu.

Nilipofika nyumbani sikumficha mama. Nilimwambia kwamba Alhakim ameninunulia nguo na vitu vingine vyenye thamani ya shilingi milioni moja na laki mbili.

Mama akashangaa.

“Si unaona mwenyewe. Ndoa bado lakini anakugharamikia!” Mama akaniambia na kuongeza.

“Mimi nakushauri mwanangu kubali akuoe.”

Sikusema kitu. Nikapanga nguo zangu ndani ya kabati.

Siku za mwishoni mwa wiki ndizo siku ambazo hukutana na mpenzi wangu. Alikuwa anaitwa Macheo, mfanyakazi wa shirika la Bandari.

Macheo alikuwa mzaliwa wa Tanga. Aliwahi kuniambia alizaliwa Mwarongo eneo liliopo katika barabara ya Pangani kilometa kadhaa kutoka Tanga.

Elimu ya msingi alisoma Tanga lakini elimu ya sekondari na chuo alisoma Dar na akapata kazi hapo hapo Dar.

Wakati tunakutana na kuanza uhusiano alikuwa na miezi kadhaa tangu ameanza kazi yake.

Kwa vile alikuwa ndio anayaanza maisha na mimi bado ninasoma tuliweka mikakati ya kuoana siku za mbele baada ya mimi kumaliza masomo.

Lakini uhusiano wetu ulikuwa siri yetu mimi na yeye. Nyumbani kwetu walikuwa hawafahamu kitu.

Siku za mwishoni mwa wiki huondoka asubuhi na kwenda kushinda nyumbani kwake Tabata.

Kulikuwa na siku wazazi wangu wote wawili waliniweka kikao na kunieleza kwamba wameshachukua pesa za uchumba kutoka kwa Alhakim. Kwa hiyo baba alitaka nitambue kuwa nilikuwa mchumba wa mtu.

“Ukimaliza masomo tu mnaoana.” Baba akaniambia.

Nilikuwa nawaheshimu sana wazazi wangu kiasi kwamba nilishindwa kupingana nao kuhusu suala hilo. Kila nilichoambiwa nilikuwa ninaitikia tu.

Lakini sikuona sababu ya kuacha kwenda kwa Macheo kwa sababu nilikuwa nampenda. Kama kutakuwa na kitu ambacho kitatia doa katika ndoa yangu na Alhakim, ni uhusiano wangu na Macheo ambao niliamini hata nitakapoolewa bado utaendelea kuwepo.

Wakati wote nilikuwa nikimficha Macheo kuhusu suala la uchumba wangu na Alhakim. Lakini baada ya kufikiri sana nikaona nikampe ukweli. Nikafunga safari kwenda Tabata.

Kwanza nilipitia Kariakoo nikanunua vitu nilivyokuwa ninavitaka. Lakini wakati ninazunguka katika maduka nililiona gari la Alhakim lakini mwenyewe sikumuona. Gari hilo lilikuwa limeegeshwa kando ya barabara.

Nikaondoka haraka katika eneo hilo. Nikiwa katika mtaa mwingine sasa nikielekea katika kituo cha daladala. Nikaliona tena gari la Alhakim nyuma yangu. Nikagundua kuwa Alhakim alikuwa akinichunguza.

Sasa nifanye nini?

Nikafanya kama sikuliona gari hilo nikatembea haraka haraka kuelekea katika kituo cha daladala. Kwa bahati nzuri nilipofika tu daladala ikasimama. Nikaingia haraka na kukaa kwenye siti. Daladala ikaondoka.

Wakati nashushwa kwenye kituo cha Tabata nikaliona gari la Alhakim hatua chache nyuma ya daladala.

Nikasema. “Mama yangu we!”

Nikiwa nimesimama kando ya barabara nikiigiza kama ninasubiri magari yapite ndio nivuke barabara nilijiambia.

“Huyu mzee ameniamulia leo.”

Kwa pembeni mwa macho yangu nililiona gari la Alhakim bado limesimama nyuma ya daladala. Mahali liliposiomama, Alhakim alikuwa akiniona vizuri.

Bila shaka alikuwa anasubiri kuona ninaelekea wapi aendelee kunifuata.

Sasa nilithibitisha waziwazi kuwa Alhakim alikuwa ananifuatilia. Iliwezekana alishagundua kuwa nina mtu wangu mitaa ya huku ndipo alipoamua kuiandama daladala niliyopanda aone mwisho wangu.

Pale nilikuwa sina mbinu tena.

“Sasa nifanye nini?” Nikaiuliza nafsi yangu iliyokuwa imegwaya.

Nikawaza kwamba kama nitaendelea na safari yangu Alhakim ataendelea kunifuatilia na kugundua ninakwenda wapi.

Pia niliona kubadili mawazo na kurudi isingekuwa busara. Ingempa picha kuwa nimerudi baada ya kumuona yeye.

Bado angeweza kuniuliza nilikuwa ninakwenda wapi na kwanini nimeamua kurudi. Nisingekuwa na la kumwambia.

Sikuwa nimepata ufumbuzi. Nikaiona daladala inaondoka baada ya kushusha watu na kupakia wengine.

Niliwaza kwamba kama nitabaki pale pale huku daladala imeondoka, Alhakim angepata nafasi nzuri ya kunifuata na nisingeweza kumkimbia tena.

Nikaona niwahi kuvuka barabara kabla daladalaa hiyo kunipita. Nikavuka barabara. Ingawa hakukuwa na gari yoyote iliyokuwa inapita, nilipiga mbio hadi ng’ambo ya pili.

Sikutaka hata kugeuka kutazama nyuma, nikaingia kwenye vichochoro. Nilifahamu kwamba asingeweza kunifuata kwa gari kwenye vichochoro labda kama angekuwa na pikipiki.

Baada ya kukatiza vichochoro viwili, vitatu, nilichanganyika na watu wengine waliokuwa wanapita. Kwa vile nilikuwa nimezibwa nikatazama nyuma.

Moyo wangu ulishituka nilipomuona Alhakim akitembea kwa miguu kunifuta.

“Huyu mzee ana tatizo gani?” Niliwaza kwa hamaki.

Maisha yale ya kuchungwa nilikuwa siyataki.

Nikaurudisha mbele uso wangu haraka na kuongeza mwendo. Kama atagundua namkimbia yeye shauri yake. Nani alimwambia anifuatefuate, nilisema peke yangu nikiwa nimechukia.

Nilikatiza tena kwenye vichochoro vingine nikatokea katika mtaa aliokuwa anaishi Macheo lakini sikwenda nyumbani kwake. Niliwaza kwamba kama Alhakim yuko nyuma yangu ataona nikiingia.

Niliipita nyumba ya Macheo ili kumpoteza Alhakim. Nikatokea mtaa mwingine. Nikasimama kwenye kioski na kununua vocha ya simu. Hapo nilikuwa namtega Alhakim kuona kama atatokea.

Baada ya kununua vocha na nilipoona simuoni tena ndipo nikarudi tena kwenye mtaa wa kina Macheo.

Hata hivyo, bado nilikuwa natembea huku natazama nyuma. Mzee nilishamchenga. Sikumuona tena.

Nilipoifikia nyumba yake nilisukuma mlango na kuingia ndani haraka haraka.

Macheo aliyekuwa ameketi sebuleni akitazama video za muziki alishituka alipoona ninaingia bila ya hodi.

“Vipi?” Akaniuliza huku akinitazama usoni.

“Poa tu,” nikamwambia na kuketi kwenye sofa.

“Mbona unatweta?’

“Kulikuwa na mzee ninayemkimbia.”

“Unamkimbia ana nini, kichaa?”

“Si kichaa, ni mzima na akili zake bali alikuwa ananifuatilia.”

“Anakufuatilia, anakufahamu?”

“Ndiyo nilikuwa nimefika kwako kukueleza kuhusu yeye, kumbe naye alikuwa ananifuatilia na gari. Nashuka tu kwenye daladala namuona. Nikamkwepa na kuingia kwenye vichochoro. Kumbe aliacha gari na kunifuata kwa miguu…”

“Sasa ana tatizo gani?”

“Baba yangu alikuwa anafanya kazi ya udereva kwake. Huyo mzee kila akifika nyumbani kumtazama baba baada ya kuumia mguu alikuwa ananiona. Akamwambia baba kuwa anataka kunioa. Baba akakubali akamwambia ampe shilingi milioni mbili za uchumba. Mzee amezitoa….”

Nikamuona Macheo akigwaya.

“Kumbe mwenzangu umeshapata mchumba!’

“Nifanye nini wangu? Wazazi wangu wamemtaka.”

“Duh! Sasa mbona unaendelea kufika kwangu?”

“Hutaki nifike tena baada ya kukwambia hivyo?”

“Hapana. Nimepata woga. Umekuwa mchumba wa mtu na mwenyewe anakufuatilia.”

“Huo uchumba wake hautaharibu uhusiano wetu.”

“Kweli?”

“Uhusiano wetu utaendelea tu. Kila mtu anataka mapenzi. Na mapenzi unayapata kwa yule umpendaye.”

“Kwa hiyo huyo mchumba hukumpenda?’

Inaendelea...