Gwiji aliyesahaulika Frank Humplick

Muktasari:

  • Frank Humplick alizaliwa tarehe 3 Aprili  1927, alikuwa mtoto wa pili wa Vicent Paul Humplick, Muaustria aliyeletwa nchini na serikali ya Kijerumani ili kuchora ramani ya  reli ya Tanga mpaka Moshi. Akiwa katika kazi zake , Vicent alitekwa na moja ya makabila alilokutana nalo na kufanywa mtumwa.

Kuna wasanii wengi waliotoa mchango wao mkubwa wa kisanii katika nchi hii katika awamu mbalimbali za historia ya nchi yetu. Mmoja wa wasanii hawa ni mwanamuziki Frank Joseph Humplick.

Frank Humplick alizaliwa tarehe 3 Aprili  1927, alikuwa mtoto wa pili wa Vicent Paul Humplick, Muaustria aliyeletwa nchini na serikali ya Kijerumani ili kuchora ramani ya  reli ya Tanga mpaka Moshi. Akiwa katika kazi zake , Vicent alitekwa na moja ya makabila alilokutana nalo na kufanywa mtumwa.

Aliachiwa baada ya vita ya kwanza ya dunia na serikali ya Waingereza ambayo ilikuwa imepewa mamlaka ya kutawala nchi hii ikamfidia kwa kumpa shamba karibu na shule ya Kilema kule Moshi.

Vicent umri wake ukiwa umeenda, alikutana na binti wa Kichaga aliyemuona akiwa anasoma katika shule ya misheni ya Kilema, na kuamua kumuoa na katika ndoa hiyo wakazaliwa Frank na dada zake wawili Thecla Clara na Maria Regina.

Mzee Vicent alifariki wakati Frank akiwa na umri wa miaka mitatu tu, lakini Mzee huyu alikuwa ameweka pembeni fedha zilizowezesha Frank na ndugu zake kusoma vizuri bila kuwa na matatizo yoyote, na hata pia kuwa na mtaji wa kuanzia maisha.

Frank alianza kujifunza muziki shuleni, alianza kwa kuimba katika kwaya ya shule, kisha kuanza kujifunza kupiga kinanda cha kanisani. Baadaye akiwa bado na umri mdogo alianza kujifunza kupiga gitaa, na kwa kutumia fedha zake akanunua gitaa lake la kwanza, katikati ya miaka ya 40, gitaa hilo aliliita ‘Mke wa Mangi’ na bado liko mikononi mwa familia yake.

Frank alianza kutunga na kupiga nyimbo zake na kuwashirikisha kuimba dada zake Thecla Clara na Maria Regina na hivyo muungano huo ukaja  kujulikana kwa jina la Frank na Dada zake.

Frank alitunga nyimbo nyingi sana za Kiswahili zilizotokea kupendwa sana Afrika ya Mashariki. Nyimbo hizo zilikuwa na maudhui mbalimbali yakiwemo, mapenzi, mafundisho ya maisha, vituko, vichekesho na kadhalika. Nyimbo kama Nyoka kabatini na Aeiou, zilikuwa nyimbo zilizopendwa na watu wa rika zote mpaka watoto, kutokana na tunzi hizo kuwa hadithi za kuchekesha.

Wimbo maarufu wa Harusi, ulikuwa maarufu kwenye kila harusi na hatimaye ulikuja kutambulika kama wimbo wa harusi wa Afrika Mashariki, wimbo huu uliorekodiwa miaka ya 50, ulikuwa na maneno mazuri sana kwa wanaooana.

Wimbo huu ulikuja kurekodiwa tena na Patrick Balisidya akishirikiana na kundi la Archimedes la Sweden, na pia kundi la Them Mushrooms la Kenya nalo liliurekodi wimbo huu, wimbo huu wenye umri wa karibu miaka sabini, bado uko hai na unatumika kwenye harusi mpaka leo. 

Kwa ushauri wa  Chifu Thomas Marealle wa Marangu, Frank alianza kuimba nyimbo kwa lugha ya Kichaga, aliweza kutoa santuri za nyimbo kama Efo Kulele, Kanfo Mshiki, Sharu Shechisia, Ngilekowo na nyingine nyingi.

Mpaka  hapo unaweza kuona mchango wa gwiji huyu katika utamaduni wa Tanzania kwa ujumla. Harakati za kutafuta Uhuru katika miaka ya 50 zilihitaji mchango wa wananchi wote waliokuwa na nia ya kuona nchi inakuwa huru, Frank Humplink akiwa na dada zake walitumia vipaji vyao na kutunga nyimbo za kuhamasisha wananchi kutafuta Uhuru.

Wimbo wake ulioitwa I am Democrat au vijana wa enzi hizo mara nyingine waliuita ‘Yes No’, ulifanya kazi ya kuhamasisha kutafuta Uhuru, na ukawa ni wimbo uliokuwa ukipigwa kabla ya mikutano ya Mwalimu Nyerere, wimbo huo ulikuwa na  baadhi ya maneno yafuatayo;

Uganda nayo iende,

Tanganyika ikichangaruka

Kenya na Nyasa zitaumana

Nasikia fununu wanavyoichanachana China,

 Kitisho!

I am a democrat I don’t want communism

English Yes No I don’t know Kizungu sikijui

Gavana wa Tanganyika wakati huo, Edward Twining, alipopata habari za wimbo huo akatoa amri kuwa wimbo huo upigwe marufuku na kukatengenezwa kikosi maalumu na kuanza kwenda nyumba kwa nyumba kusaka santuri za nyimbo hiyo na kuzivunja.

Pia Frank alitunga  wimbo mwingine maarufu  ulioimbwa  na yeye akishirikiana na dada zake, wimbo huo ulikuwa katika fumbo, uliitwa, Huo Mwamba. Wimbo huu ulikuwa maalumu kumsifu Mwalimu Nyerere, ambaye ndiye alitambuliwa kama Mwamba katika wimbo huo.

Ikumbukwe kuwa wakati huo ulikuwa ni wakati wa ukoloni, na ilikuwa ni hatari kuonekana unaipinga serikali, lakini naye aliona umuhimu wa kuchangia kwa njia yake kudai Uhuru.  Mzee Frank aliendelea kutumia muziki kuelimisha jamii yake hata katika miaka yake ya uzeeni. Tungo yake ya kuhamasisha kilimo bora ilikuwa na maneno haya;


Tupandikizapo mbegu

Tupande kwa mistari

Kufuatana na kinga maji

Iwe maridadi

Tupande na mitunda,

Kwa kupitanapitana

Hata miti mingine

Kwa matumizi ya kuni

Wimbo huu ulitumika katika kampeni za kuboresha kilimo katika maeneo ya Usambara.

Frank Humplick na dada zake wote sasa ni marehemu, Frank alifariki tarehe 25 Agosti 2007, kaburi la Frank na hata lile la baba yake Mzee Vicent yapo jirani na nyumba ya familia Lushoto.

Jina la Frank  limebaki midomoni mwa ndugu na marafiki wa karibu na ndio pekee wanaohadithiana kuhusu kazi kubwa aliyofanya gwiji huyu wakati wa uhai wake. Mungu Amlaze Pema Peponi.