Elyston Angay Arejea Dar, bendi tatu kukutana mkesha wa Valentine Day
Muktasari:
- Shoo hiyo itazikutanisha Twanga Pepeta chini ya uongozi wa Chaz Baba, Bogoss Musica inayoongozwa na Nyoshi Elsaadat, na Christian Bella na Malaika Band, katika jukwaa moja linalotarajiwa kuwaka moto wa burudani.
MASHABIKI wa muziki wa dansi, wanatarajiwa kupata burudani ya kipekee Februari 13, 2026, kwenye mkesha wa Siku ya Wapendanao (Valentine Day), ambapo bendi tatu kubwa hapa nchini zinakutana katika shoo moja kabambe itakayofanyika Ukumbi wa Las Carinyo uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Shoo hiyo itazikutanisha Twanga Pepeta chini ya uongozi wa Chaz Baba, Bogoss Musica inayoongozwa na Nyoshi Elsaadat, na Christian Bella na Malaika Band, katika jukwaa moja linalotarajiwa kuwaka moto wa burudani.
Mgeni mualikwa katika shoo hiyo ni msanii mkongwe Elyston Angay, kutoka Afrika Kusini, ambaye ana historia ndefu na yenye heshima kwenye muziki wa dansi Afrika Mashariki.
Elyston Angay aliwahi kuitumikia bendi ya Diamond Sound, maarufu kwa jina la “Kibinda Nkoi”, ambako alipiga nyimbo kadhaa zilizotikisa anga la muziki zikiwemo Kimalumalu, Neema na nyingine nyingi.
Kwa mujibu wa historia yake ya muziki, Elyston aliingia Dar es Salaam miaka ya 1990 akiwa chini ya MK Sound, bendi iliyokuwa ikiongozwa na Asha Baraka.
Baadaye ilipoanzishwa Diamond Sound, Elyston Angay aliteuliwa kuwa kiongozi na mpiga gitaa wa bendi hiyo katika miaka ya 1995 na 1996, kipindi ambacho Diamond Sound ilikuwa ikipiga ukumbi wa Silent uliopo Mwenge.
Baada ya hapo, aliondoka Tanzania na kuelekea Zimbabwe, kabla ya kuhamia Afrika Kusini ambako anaishi kwa sasa.
Shoo hiyo imeandaliwa na Lengos V.I.P kwa kushirikiana na Chamudata (Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuenzi na kukuza muziki wa dansi pamoja na kuwakutanisha wasanii wakongwe na chipukizi katika jukwaa moja.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya shoo hiyo, mmoja wa waratibu wa tamasha hilo, King Dodoo, amesema: “Hii ni shoo ya kihistoria inayowaleta pamoja magwiji wa muziki wa dansi, lengo letu ni kuwapa mashabiki burudani ya kiwango cha juu na wakati huohuo kuenzi mchango wa wasanii waliojenga tasnia ya muziki wetu, tunawahakikishia mashabiki usiku wa Valentine usiosahaulika.”
Mashabiki wa muziki wa dansi wanahimizwa kujiandaa mapema kwa shoo hiyo, inayotarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa ya burudani mwaka 2026 huku kiingilio kikiwa ni VVIP Sh1,000,000, VIP Sh500,000 na siti za kawaida Sh10,000.