Dully Sykes kutumia saa 2 jukwaani Tamasha la Deiwaka World

Summary


  • Tamasha la wakongwe wa muziki (Deiwaka World) linaanza rasmi leo na litakuwa likifanyika kila mwezi mara moja.

Dar es Salaam. Wakati wapenzi wa muziki wakihesabu saa kumshuhudia Dully Sykes akifungua dimba kwenye tamasha la wakongwe (Deiwaka World), mwanamuziki huyo amesema atatumia si chini ya saa 2 jukwaani akiimba.

Dully Sykes jioni ya leo ataanzisha safari ya Deiwaka World, tamasha linalowahusisha wasanii wakongwe nchini mahususi kwa ajili ya kuenzi kazi zao, lililoratibiwa na mkongwe wa Hip Hop, Joseph Mbilinyi (Sugu).

Tamasha hilo litafanyika kwenye kituo cha Utamaduni cha Ufaransa, jijini hapa kwa kiingilio cha Sh20,000.
Akizungumza na Mwananchi Digital katika mazoezi yake ya mwisho, Dully amesema amejiandaa kuimba nyimbo zake nyingi.

"Nitaimba kwa saa mbili mfululizo, uliachana na matukio mengine yatakayokuwa yakiendelea ukumbini, mashabiki watarajie kitu cha tofauti leo," amesema.

Mwanamuziki huyo aliyewahi kutamba na nyimbo kama Hunifahamu, Hi!, Salome na nyingine nyingi amepewa heshima ya kufungua dimba kwenye tamasha hilo la kila mwezi.

Akizungumzia fursa hiyo, Dully amesema mwanzo ilimpa hofu kwa kuwa kuna uzuri na ubaya wa kuwa wa kwanza.

"Nilipata hofu kidogo kwa kuwa unaweza kuanza vizuri, ukawa ni mfano bora kwa watakaofuata, pia unaweza kuanza vibaya, nilihofia nilipopewa heshima hiyo, lakini kwa kufanya shoo, niko freshi.

"Nimejipanga, mashabiki wangu wananijua na ninakwenda kutoa burudani ambayo itaacha historia, namuomba Mwenyezi Mungu niwe na mwanzo mzuri wa tamasha hili," amesema.

Dully ataimba laivu, akipewa sapoti na baadhi ya wasanii akiwamo Sugu, ambaye alifafanua kwamba kwenye tamasha hilo, mwanamuziki ambaye atapewa fursa ya kufanya shoo utakuwa ni usiku wake kama itakavyokuwa kwa Dully Sykes leo.

"Kutakuwa na historia yake, nyimbo zake na matukio mengine mengi yanayomhusu ukiachilia mbali burudani, lengo ni kuwaheshima na kuwaenzi wanamuziki wakongwe nchini," amesema Sugu.