Dora wa Juakali ampagawisha Sanjay Dutt

Thursday November 11 2021
dola pic
By Nasra Abdallah

Sanjay Dutt ambaye ni muigizaji maarufu kutoka nchini India ameonekana kupagawa na muigizaji wa nchini Tanzania Dora ambaye kwa sasa anatesa kwenye tamthilia ya Juakali.
Hilo limetokeaJumatano Novemba 10, 2021 wakati muigizaji huyo ambaye yupo nchini humo kwa mualiko maalum alipokutana na wasanii wa filamu na viongozi kutoka serikali wanaosimama sekta ya filamu.
Ilikuwa wakati Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa Nchini humo, Dk Emmanuel Ishengoma, alipokuwa akimkaribisha Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa kuzungumza na hadhira iliyokuwa imefika katika hafla hiyo iliyofanyika hoteli ya Hyatt jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo wakati Waziri huyo alipokuwa akikaribishwa na kiongozi huyo, alionekana kutomsikia na kuwa makini katika kumsikiliza  msanii huyo ambaye alikuwa mara kwa mara akimnyooshea kidole Dora na kumwangalia kwa muda mrefu hadi kugeukia upande aliokaa msanii huyo.
Mara baada ya Waziri Bashungwa kuinukana kuzungumza, ndipo alipotoa maelezo kuwa walijikuta katika mazungumzo ya muda na msanii huyo ambaye alitaka kumjua zaidi Dora, ambaye naye alimwelezea kuwa ni muigizaji.
Mwananchi ilitaka kufahamu kutoka kwa Dora namna alivyojisikia kutokana na tukio hilo, ambapo amesema kwake ni bahati kwani Dutt sio msanii mdogo ni wa kimataifa hivyo kwa yeye kutaka kumjua zaidi hiyo ni fursa nyingine kwake katika safari yake ya sanaa.
“Huyu sio msanii mdogo jamani ,naweza kujiita mimi ni mwenye bahati, kwani hapa ukumbini tulikuwa wasanii wengi kwa nini atake kunijua zaidi mimi, nimefurahi sana ukizingatia pia ni msanii ambaye nimekuwa nikifuatilia filamu zake,” amesema Dora.
Aidha amesema ana imani katika fursa zilizotangazwa kwa muigizaji huyo kucheza baadhi ya filamu na wasanii wa Bongo kabla hajaondoka, naye atakuwa mmojawapo na kueleza kuwa ujio wake ni hatua nyingine imepigwa katika tasnia ya filamu nchini humo kutambulika kimataifa na nchi kwa ujumla.

Advertisement