Dk Cheni awachongea mastaa wasiojali muda kwa mtoa maokoto

Muktasari:

  • Unajua kwenye hii kazi ya filamu, tamthilia na uigizaji kwa ujumla ni mnyororo  mtu mmoja akishindwa kutokea ina maana amekwamisha watu hata zaidi ya 10  wasiweze kufanya kazi yao, jambo ambalo pia litamchelewesha prodyuza kuwasilisha kazi yake kwa muda aliopangiwa

Dar es Salaam. Mkongwe wa filamu nchini Mahsin Awadh amesema watawaanika wasanii wanaochelewa eneo la kazi (location) wanaposhirikishwa kwenye filamu.

Dk Cheni amesema hayo kwenye uzinduzi wa  tamthiliya  ya 'Siri' itakayokuwa ikirushwa Azam Tv.

“Waigizaji mastaa hawatashiriki kwenye kazi zangu kwa sababu wamekuwa wasumbufu wa kuchelewa location au kutofika kabisa.

"Mimi niwaombe Azam ambao mnapokea kazi zetu, watu hawa tutakuwa tukiwaanika majina yao huko mbele ya safari ili wakija kwenu mkatae kufanya nao kazi nadhani itakuwa fundisho kwa wengine,"amesema  Dk Cheni.

Kufuatilia kauli hiyo ya Dk Cheni, mwigizaji Irene Paul ambaye ndiyo mtayarishaji wa filamu wa ‘Siri’, aliwaomba msamaha watayarishaji wa filamu kwa sababu na yeye ni miongoni mwa waigizaji wanaochelewa location au kutokwenda kabisa

Akilizungumzia hilo, Irene amesema ni kweli kuna hiyo tabia kwa waigizaji na yeye akiwa ni mmoja wao, lakini baada ya kuandaa tamthilia hiyo amegundua alikuwa akiwakosea sana watayarishaji.

"Naomba nitumia nafasi hii kuwaomba msamaa watayarishaji kwani nimejifunza kitu kupitia uandaaji wa tamthilia hii, mpaka kukamilika kwake nishagombana na watu kwa ajili ya suala la kuchelewa au kutokuja kabisa eneo la kufanyia kazi,"amesema Irene.

Kwa upande wa msimamimizi mkuu wa chaneli ya sinema zetu, Sofia Mgaza  amesema anayachukua malalamiko hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ikiwemo kuwapa elimu wasanii kabla ya kwenda kufanya kazi  kuhusu umuhimu wa wao kujali suala la muda.

"Unajua kwenye hii kazi ya filamu, tamthilia na uigizaji kwa ujumla ni mnyororo  mtu mmoja akishindwa kutokea ina maana amekwamisha watu hata zaidi ya 10  wasiweze kufanya kazi yao, jambo ambalo pia litamchelewesha prodyuza kuwasilisha kazi yake kwa muda aliopangiwa,"amesema  Sofia.

Baadhi ya wasanii akiwamo mkongwe  Jacob Steven, maarufu JB amezungumzia suala hilo kwa kusema anachokiona ni baadhi ya wasanii kutochukulia filamu kama kazi na kueleza kuwa kwake imekuwa tofauti na ndio maana hadi leo yupo kwenye tasnia.

Naye  Suzan Lewis, maarufu Natasha amesema sababu zinazochangiwa kutojali muda kwa wasanii ni baadhi yao kuingia  kwenye sanaa hiyo kwa malengo mengine ikiwemo kuuza sura au kutafuta umaarufu, lakini wakati huohuo ana kazi yake nyingine tofauti anayoipenda zaidi.

Akilizungumzia hilo mkali wa uigizaji nchini, Shamila Ndwangila, maarufu  Bi Star amesema tatizo hilo linachangiwa na baadhi ya wasanii kutopikwa vizuri wakati wanaingia kwenye uga huo.

Ametolea mfano  walivyopika wakatyi huo wakiwa kwenye kundo la Kaole. “Tulikuwa tunapewa  adhabu  ya kusimamishwa hata miezi mitatu kwa kosa la  kuchelewa, jambo ambalo leo limemjenga kila aliyepita pale kujua umuhimu wa muda kwa msanii.