Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Diamond, Vannesa Mdee watwaa tuzo nyingine Nigeria

 Naseeb Abdul  (Diamond Platinum) msanii aliyepokea tuzo ya msanii bora Afrika Mashariki

Muktasari:

Diamond na Vee Money walishinda tuzo hizo za kimataifa za All Africa Music Awards (Afrima) zilizotolewa usiku wa Desemba 27, huko Lagos nchini Nigeria.

HUENDA yakawa ni mafanikio ya kufungia mwaka katika sekta ya burudani nchini, baada ya Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Vanessa Mdee ‘Vee Money’ usiku wa kuamkia jana kutunukiwa tuzo kama wasanii bora Afrika Mashariki.

Diamond na Vee Money walishinda tuzo hizo za kimataifa za All Africa Music Awards (Afrima) zilizotolewa usiku wa Desemba 27, huko Lagos nchini Nigeria.

Vanessa alishinda katika kipengele cha Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki, na kuwashinda Wahu (Kenya), Muthoni The Drmmer (Kenya), Size 8 (Kenya), Kaz (Kenya) na Jackie Chandiru (Uganda) ambao pia walikuwa wakiwania tuzo hiyo na kujikuta wakiondoka mikono mitupu.

Kwa upande wa Diamond Platnumz alinyakua tuzo ya Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki, ambayo alikuwa akiwania sambamba na Dr Jose Chameleone (Uganda), Kidumu (Burundi), Maurice Kirya (Uganda) pamoja na Peter Msechu ft Amini (Tanzania).

Kati ya Watanzania watatu waliokuwa wakiwania tuzo hizo, Vee Money na Diamond Platnumz wote kwa pamoja, walikuwa wakiwania vipengele sawa huku kila mmoja akiondoka na tuzo hiyo kwa usiku mmoja.

Peter Msechu ambaye alihudhuria tuzo hizo akiwa ni msanii mwingine kutoka Tanzania aliyekuwa akiwania tuzo hizo kupitia wimbo wake ‘Nyota’ aliomshirikisha Amini, kwa bahati mbaya alishindwa kutwaa tuzo usiku huo ambayo ilikwenda kwa Diamond Platnumz.

Kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram, Msechu alionekana akiwa amebeba tuzo ya Diamond ambaye hakuweza kuhudhuria sherehe za tuzo hizo, kutokana na ziara yake ya kimuziki nchini Burundi ambako alifanya shoo usiku wa kuamkia leo.

Vee Money ambaye pia ni Mtangazaji wa Kituo cha Redio cha Choice FM na MTV Base, akizungumzia tuzo hiyo kupitia ukurasa wake wa Instagram, aliandika “Kwa Mungu kuna utukufu, asanteni sana kwa kunipigia kura. Ninawapenda”#BestFemaleEastAfrica#Tanzania,” aliandika.

Ushindi huo wa kishindo kutoka Tanzania, umewafedhehesha wanamuziki mbalimbali kutoka Afrika Magharibi, Kusini na Afrika Mashariki ambao wameonyesha wazi kuanza kuifikiria Tanzania katika mapinduzi ya muziki kwa mwaka 2015.

Mwanamuziki Davido ameendeleza hofu kwa wasanii wenzake, baada ya kushindwa kumuunga mkono msanii mwenza na rafiki yake Diamond Platnumz, mara baada ya kutajwa kuwa mshindi wa tuzo usiku huo.

Hata hivyo, Tanzania imeanza kung’ara katika muziki na kila tuzo inachukuliwa na Diamond Platnumz.

Video za wasanii wa Tanzania hivi sasa zinatazamwa na mataifa mengi zaidi ukilinganisha na Wanigeria ambao walikuwa wakiongoza na P Square, Davido, Iyanya, Wizkid, Waje na wengineo.