Diamond mambo yazidi kumnyookea Bongo

Muktasari:
- Staa huyo wa ngoma ya Nitafanyaje, aliyoipiga katika miondoko ya singeli, amesaini mkataba mpya wa kampuni ya SBC Tanzania Ltd baada ya ule wa awali kufikia tamati.
NYOTA wa muziki wa kizazi kipya nchini, Diamond Platnumz mambo yamezidi kumnyookea baada ya kusaini tena mkataba utakaomuungizia noti.
Staa huyo wa ngoma ya Nitafanyaje, aliyoipiga katika miondoko ya singeli, amesaini mkataba mpya wa kampuni ya SBC Tanzania Ltd baada ya ule wa awali kufikia tamati.
Diamond anakuwa miongoni mwa wanamuziki wakubwa duniani, ambao ni mabalozi wa kinywaji cha Pepsi, ambacho hapa nchini kinazalishwa na SBC akifanya nao kazi tangu 2018.
Mkataba huo mpya baina ya pande hizo mbili umetangazwa leo, Mei 21, 2025 ikiwa n8 siku kadhaa tangu kuwepo kwa maneno kutoka kwa baadhi ya watu wakidai msanii huyo hayupo kwenye mahusiano mazuri na kampuni hiyo.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Meneja Masoko wa SBC Tanzania, Jasper Maston, amesema mafanikio ya ushirikiano huo na mchango wa Mondi katika mafanikio ya kibiashara ya kampuni hiyo ndio sababu ya kuendelea kwao.
"Kwa miaka 24, kampuni imekuwa mstari wa mbele katika sekta ya uzalishaji na usambazaji wa vinywaji baridi Tanzania. Ikileta bidhaa bora, ubunifu, na nyakati za furaha kwa mamilioni," amesema Maston na kuongeza;
“Ushirikiano wetu na Diamond Platnumz ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kuhamasisha vizazi. Pamoja na Pepsi, tumeungana kuwasiliana na vijana wa Tanzania kupitia ubunifu, utamaduni, na kampeni zisizosahaulika. Ushirikiano huu sio tu kuhusu biashara ni harakati inayosherehekea fahari na ndoto za Watanzania."
Amesema ubunifu wa Diamond umeongeza sauti katika ujumbe wa bidhaa hiyo kama ishara ya nguvu za vijana, na fahari ya kitaifa.
"Diamond Platnumz anawakilisha ujasiri na uhalisia ambao Pepsi inasimamia. Uhusiano wake na watu, pamoja na ubunifu wake usioyumba, unalingana na dhamira ya SBC Tanzania ya kuwa na umuhimu na matarajio, tunabadilisha nyakati kuwa harakati na tuna mapya mengi yanakuja,” amesema na kumalizia
“Hatujawahi kuwa na mgogoro na Diamond. Kwa mwaka jana lengo letu lilikuwa ni kuitangaza zaidi chupa na logo mpya ndio maana katika mabango hatukumtumia. Kwenye mambo mbalimbali tulikuwa tunaendelea kufanya kazi kawaidia kama vile kwenye tamasha la Wasafi Festival na mengineyo,” amesema.
Mbali na hayo akizungumzia ushirikiano huo, Diamond amesema Pepsi imeendelea kuipa thamani tasnia ya muziki nchini.
“Tangu mwaka 2018 tunafanya kazi pamoja kwanza inaonesha ni uchaguzi sahihi. Naishukuru kwa kuendelea kuamini katika sanaa unajua zamani ilikuwa ngumu makampuni makubwa kama haya kuamini wasanii," amesema Mond na kuongeza;
“Lakini inaonesha nchi hii haina wasanii wa hovyo hovyo, hii inaonesha chapa zetu za muziki zina thamani, hadi kushirikiana na kampuni kubwa kama hii. Pia serikali imeweka miundombini mirahisi ya kupata fursa na kuwekeza."