Diamond aibua zogo jipya Dar
Muktasari:
- Mondi ameongea hayo katika uzinduzi wa tamasha hilo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Amell in Dar, akisema anamshukuru Mungu kwa kumpa afya njema na kuweza kuandaa tena tamasha, akimshukuru pia Rais Samia Suluhu kwa mchango mkubwa katika sanaa, na pia ndiye Rais wa kwanza nchini mwanamke lakini binafsi hakubahatika kulelewa na baba, badala yake alilelewa na mama pekee.
NYOTA wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, ameibua zogo jingine baada ya kuamua kukitonesha tena kidonda cha Mzee Abdul kwenye uzinduzi wa Wasafi Festival 2024 pale aliposisitiza amelelewa na mama tu yaani Sanura Kassim ‘Sandra’ au ‘Mama Dangote’ kama alivyowahi kusema awali alipomkana mdingi wake huyo.
Mondi ameongea hayo katika uzinduzi wa tamasha hilo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Amell in Dar, akisema anamshukuru Mungu kwa kumpa afya njema na kuweza kuandaa tena tamasha, akimshukuru pia Rais Samia Suluhu kwa mchango mkubwa katika sanaa, na pia ndiye Rais wa kwanza nchini mwanamke lakini binafsi hakubahatika kulelewa na baba, badala yake alilelewa na mama pekee.
Mwimbaji huyo akaenda mbali na kusema mama yake alihangaika na kusota naye hadi leo amesimama kuwa mkurugenzi wa taasisi mbalimbali, hivyo anawaamini na anawaheshimu wanawake kwani wana uwezo wa kufanya jambo kama alivyomshuhudia Mama Dangote na wengineo.
“Tamasha hili kwa 2024 litaanzia Ruangwa, nimshukuru Rais Samia Suluhu kuwa pamoja na wasanii, Tanzania tumebahatika kuwa na Rais wa kwanza mwanamke na niseme wazi, mimi nawaheshimu sana wanawake wapambanaji, binafsi sikubahatika kulelewa na baba nimelewa na mama tu peke yake, mama amehangaika nami, amesota na mimi weweee hadi leo,” alisema Chibu a.k.a Dangote.
Mbali na hayo, Mondi pia alisema; “Mimi ni Mtanzania nitakayewakilisha taifa, na ndoto yangu kubwa ni kuwa tajiri namba moja duniani, na mwaka huu natarajia kutambulisha bidhaa yangu mpya, hivyo nitaomba muendelee kunishika mkono.”
MIAKA MIWILI NYUMA
Kwa waanaokumbuka. Miaka miwili nyuma, Diamond Platnumz aliwahi kuweka bayana ukweli kuhusu baba yake mzazi.
Alizungumza katika mahojiano na Wasafi Radio, alisema licha ya kuishi vizuri na Mzee Abdul ambaye awali alifahamika kama baba yake mzazi, lakini aligundua baba yake mzazi ni mzee Nyange ambaye sasa ni marehemu.
“Nikiwa na kama miaka 11 hivi niliambiwa na mmoja wa majirani zangu kwamba, niende soko la Tandale, halafu muulizie Salum Bubu au Idd Nyange, nikafika akanipa Shilingi mia mbili na mchele, kwa sababu alikuwa anauza mchele wa ujumla,’’ alinukuliwa Diamond na kuongeza;
“Mwanzoni nilikuwa naona utofauti katika vitu vingi, lakini sikuweza kuelewa baadhi ya vitu kwa sababu ya utoto.”
Kabla ya hayo kulikuwa na gumzo mtandaoni kuhusu baba aliyefahamika kama mzazi wa Diamond kuwa si baba halisi wa mwimbaji huyo.
Gumzo hilo lilianza mara baada ya mama Dangote, yaani Sandra kuongea katika radio kuwa baba ambaye anadai Diamond amemtelekeza si baba wa kumzaa na baba yake Diamond ni marehemu, alikuwa anaitwa Nyange na si Abdul.
Mama huyo aliweka picha ya Diamond ikiwa pamoja na Nyange kuonesha jinsi wanavyofanana.
Hatua hiyo iliendelea kuzua mijadala katika mitandao ya kijamii nchini, haswa baada ya mzee Abdul kutoridhishwa na tukio hilo kwa madai ya kwamba aliukataa ujauzito.
‘’Kama niliukataa ujauzito, iweje nimlee Diamond miaka yote hiyo?” alihoji Mzee Abdul ambaye alimlea Diamond tangu akiwa mdogo na watu wengi kudhani kuwa ndiye baba yake mzazi.
Hata hivyo, Mwanaspoti juzi ilimtafuta Mzee Abdul na kumjulia hali sambamba na kumuuliza kama bado amekata tamaa kuhusu madai Diamond ni mtoto wake na pia kauli ya Diamond kuendelea kusisitiza kuwa amelelewa na mama yake tu.
Kinyonge, Mzee Abdul alisema alishamuachia Mungu na kufunga huo mjadala wa familia ya Diamond.
“Unataka sasa mimi niseme nini mwanangu. Nilishasema namuachia Mungu hili suala la Diamond na mama yake, na kama anasema amelelewa na mama yake tu, basi sawa ila mie nimeshafunga huo mjadala siku nyingi, acha nibakie tu sijashiriki chochote, maana mwanzo walisema mimi sio baba yake, pili kuwa mimi baba mlezi, sasa hivi wanasema amelelewa na mama yake tu basi... sawa kikubwa uhai,” alisema Mzee Abdul.