Diamond afunguka ishu ya WCB kukandamiza wasanii mikataba

Diamond afunguka ishu ya WCB kukandamiza wasanii mikataba

Muktasari:

  • Baada ya sakata linaloendelea mitandaoni kuwa lebo ya WCB inakandamiza wasanii, mkurugenzi wa lebo hiyo, Diamond Platnumz amesema, haoni tatizo kuchukua asilimia 60 ya mapato ya msanii wake.

Dar es Salaam. Baada ya sakata linaloendelea mitandaoni kuwa lebo ya WCB inakandamiza wasanii, mkurugenzi wa lebo hiyo, Diamond Platnumz amesema, haoni tatizo kuchukua asilimia 60 ya mapato ya msanii wake.

Amesema anafanya hivyo kwani mziki ni biashara inayohitaji uwekezaji mkubwa na mpaka msanii awe mkubwa inatumika kati ya Sh 400-500 milioni zinakuwa zimetumika kuwekeza kwa wasanii.

“Mziki ni biashara, unaona sisi tunavyochukua vijana walikuwepo katika malebo flani ila hawakuwa wakubwa.

“Ila wanapokuja kwetu sisi wanajua kuimba tunachukua kile anachofanya kuwa biashara kiweze kuingiza hela, ndio maana wasanii wa Wasafi wanakuwa wakubwa na matajiri,” amesema Diamond katika mahojiano yake na Kituo cha Kimataifa cha DW

“Biashara inapokuwa kubwa wengi wa vijana wanataka ile biashara aichukue yeye peke yake wakati ni uwekezaji nilifanya haya kwa kuwekeza mamilioni ya pesa zangu ndani yake,” amesema

Diamond amesema lakini sasa msanii anaposema wanataka kuondoka na biashara nzima siwezi kuruhusu hilo, napaswa kurejeshewa pesa zangu na faida pia.

Sakata hilo limeibuka kufuatia kuondoka kwa msanii Rayvanny wiki mbili zilizopita, ambaye Mwananchi inafahamu kuwa alilipa Sh 1 bilioni kama fidia ya sehemu iliyobaki katika mkataba wake wa miaka 10.

Mtayarishaji nguli wa muziki nchini, P Funk Majani ambaye alifanya vizuri  kwa kipindi cha miaka ya 90 na mwanzoni mwa miaka ya 2000 na lebo yake ya Bongo Records naye alitoa maoni yake kuhusu mikataba ya wasanii wanayosaini na WCB.

“Unajua kitu kimoja nachopenda uwe fair, usifanye biashara kuangamiza wenzio, ndio maana hujawahi kuona imetokea kwetu kwamba sisi tuna maelewano yetu na tunakula sambamba, wale wanamdidimiza msanii wanachukua asilimia kubwa halafu yeye anabaki na ndogo, akienda kuimba au kutumbuiza anakatwa hela kubwa, akiuza kwenye albam anakatwa hela kubwa” alisema P Funk na kuongeza.

“Mimi naona tujifunze fair play kwenye industry yetu zote ziwe za filamu, mziki, uchongaji, uchoraji, mitindo kila sekta tuwe na fair play tuelewe pia hizi haki tofauti au atleast kuwe na vyombo ambavyo vinaundika kulinda hizo haki,” alisema  

Akijibu tuhuma za P Funk mmoja wa mameneja wa WCB, Hamis Tale Tale “Babu Tale” hakutaka kuliongelea kiundani ila alisema P Funk ni mkongwe na anamheshimu na akasema ishu za mikataba ni ishu za ndani.

“Mheshimu mkongwe kasema tuachane nalo, namuheshimu sana P Funk, tumuache na mkataba haupo kwenye mic wala camera tumuache majani, ushawahi kumuona mtu amebandika mkataba kwenye mic au kwenye camera? Heshima ya Majani kwenye hii Industry ni kubwa tumuache,” alisema Tale na kuongeza.

Rayvanny anakuwa msanii wa pili kuondoka kwenye lebo hiyo ya WCB akitanguliwa na Harmonize aliyeondoka mwaka 2019.

Harmonize alikuwa msanii wa kwanza kusainiwa na WCB na alikuwa kwenye lebo hiyo kwa miaka minne.

Alipolazimika kuondoka, kuliibuka mjadala mitandaoni huku yeye mwenyewe akisema amediriki kutoa fedha nyingi ili kuachana na WCB.

Taarifa zinadai alitoa Sh 500 milioni kuvunja mkataba wake uliokuwa umebaki kati ya miaka 10 aliyokuwa amesaini.