Darassa kuburuzwa kortini

Muktasari:

  • Kampuni ya Baistar Advocate imewafungulia kesi ya madai ya Sh271.4 milioni, msanii Sharif Thabeet maarufu kwa jina la Darassa na mmiliki wa Mwailubi Lounge baada ya kuvunja mkataba wa kufanya tamasha jijini Mbeya.

Mbeya. Kampuni ya Baistar Advocate jijini Mbeya imefungua kesi ya madai katika Mahakama ya Wilaya ya Mbeya dhidi ya msanii wa kizazi kipya, Shariff Thabeet maarufu kwa jina la Darassa na mmiliki wa Mwailubi Lounge, Daniel Mwailubi kwa madai ya kuvunja mkataba wa kufanya tamasha.
Tamasha hilo la Beer Festive Season 28 lilitakiwa kufanyika Julai 30 mwaka huu.
Shauri hilo liliwasilishwa na mwanasheria wa kampuni hiyo, Baraka Mbwilo kwa niaba ya wateja wake, Arnold Kisheni na Seiph Wembe mbele ya Hakimu Mkazi Happiness Chuwa Agosti 24 mwaka huu.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Agosti 29, Mbwilo amesema awali shauri hilo lilipowasilihwa mahakamani, mdaiwa wa kwanza, Danny Mwailubi alipatiwa nakala ya madai na kutakiwa kupeleka utetezi wake ifikapo Septemba 5 mwaka huu huku Darassa akiendelea kutafutwa.
Amesema kutokana na usumbufu walioupata wamewasilisha madai ya fidia ya Sh71.4 milioni ikiwa ni madai halisi huku 200 milioni fidia ya madhara waliyoyapata pamoja na kuwataka kuomba msamaha usio na masharti na kulipa gharama za uendeshaji wa kesi Mahakamani.
Mbwilo ameeleza kuwa mnamo Julai 29 mwaka huu walalamikaji wakiwa Mpanda Mkoa wa Katavi waliona tangazo kwenye akaunti za Instagram za wadaiwa wakitangaza kuwepo kwa tamasha la Beer Festival Season 28.
Tangazo hilo ambalo liliambatana na picha ya msaanii Darassa kwa kiingilio cha 10,000 na bia moja ambalo lililotakiwa kufanyika Julai 30 na badala yake walivunja makubaliano baina ya wadaiwa  na wateja kwa msanii hiyo kutopanda stejini kama ilivyokuwa makubaliano.
 “Wateja wangu walisafiri kutoka Mkoa wa Katavi kuja kushuhudia tamasha hilo lakini walikaa mpaka alfajiri pasipo msanii kupanda stejini na wala Mmiliki wa Mwailubi Lounge kuwaeleza chochote,'' amesema.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Mkoa wa Mbeya, Happiness Chuwa amesema amepanga kusikilizwa kwa shauri hilo namba 25, Septemba 5 mwaka huu, huku wakimtaka mmiliki wa Mwailubi Lounge kupeleka utetezi wake Mahakamani na kumtafuta msanii wa Kizazi kipya maarufu kama Darassa.
Juhudi za kumtafuta Darassa na Mwailubi hazikufanikiwa baada ya simu zao kuita bila kupokelewa.