Country Wizzy, Casey kukinukisha Hip Hop Asilia
Muktasari:
- Tamasha hilo ambalo litafanyika kwa siku mbili Juni 28 na 29 mwaka huu limeandaliwa na Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Muziki cha Dhow Country Academy (DCMA) ambapo vijana watapata fursa kuonesha vipaji vyao ikiwemo Wanamuziki, Wasanii wa Kughani mashairi, Waandishi wa Sanaa za machata, Sanaa ya umanju, Wavunjaji na Sanaa ya upigaji wa midundo kwa midomo.
TAMASHA la Hip Hop Asili la mwaka 2024 linatarajiwa kufanyika Bagamoyo katika Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo (Tasuba) lengo ni kuleta muunganiko wa talanta za kitaifa na kimataifa katika utamaduni.
Tamasha hilo ambalo litafanyika kwa siku mbili Juni 28 na 29 mwaka huu limeandaliwa na Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Muziki cha Dhow Country Academy (DCMA) ambapo vijana watapata fursa kuonesha vipaji vyao ikiwemo Wanamuziki, Wasanii wa Kughani mashairi, Waandishi wa Sanaa za machata, Sanaa ya umanju, Wavunjaji na Sanaa ya upigaji wa midundo kwa midomo.
Mkurungezi wa miradi wa Tamasha la Festival Hip Hop Asili, Matei Babu amesema wanamuziki na wasanii wa kughani mashairi wameshirikiana kuunda mchanganyiko wa pekee wa Hip Hop na Muziki wa asili wa nchi za majahazi Ili kuwapa wapenzi wa tamasha ladha ya Muziki wa kipekee isiyoweza kusahulika.
“Tamasha hili litatoa burudani zenye utamaduni wa Hip Hop Afrika Mashariki ambapo burudani ya Muziki wa Rap kutoka kikosi cha wasanii wakiwemo Malim Nash, Country Wizzy, Machalii Watundu, Sinaubi Zawose na Casey kutoka Ufaransa wakishirikiana na Harley Tz, Prisca Hilonga, Slim C na Low-key Picasso,” amesema Babu.
Ofisa wa Utamaduni na michezo,Etienne Pellausy amesema tamasha hilo litawaweka vijana pamoja na kuwakilisha mawazo yao kupitia sanaa pamoja na kujitangaza.
Pellausy amesema utaalamu wa sanaa ya upigaji midundo kwa mdomo watashirikiana kati ya wasanii wa Tanzania na Uganda lengo kujifunza na kutengeneza uhusiano wa kitamaduni Afrika Mashariki.
“Kwa kuzingatia kutambuliwa kwa mashindano ya Breaking kama mchezo wa Olimpiki tamasha la Hip Hop Asili kwa kushirikiana na StreetOff limekuwa mwenyeji wa mashindano ya mchezo huo Afrika Mashariki ambapo itajumuisha washiriki kutoka Uganda, Rwanda, Burundi, Congo na Tanzania watashindana.” amesema Pellausy