Cosota: Ukusanyaji wa mirabaha ni utaratibu wa kisheria

Muktasari:
- Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (Cosota) imesema ukusanyaji wa mirabaha ni utaratibu wa kisheria na miongozo mbalimbali.
Dar es Salaam. Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (Cosota) imesema ukusanyaji wa mirabaha ni utaratibu wa kisheria na miongozo mbalimbali.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Februari 22,2022 na Ofisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki wa Cosota, Doreen Sinare alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu mchakato wa ugawaji mirabaha inayodaiwa kulalamikiwa na moja ya taasisi inayojiita Creative Industry Network Tanzania (CNIT), wakishirikiana na Shirika la Twaweza kuwa haukuwa wa haki.
“Hoja zao tulizipokea kwa njia ya barua, lakini wakati tukijiandaa kutoa majibu, Februari 19,2022 tukaona taarifa yao kwa vyombo vya habari ikiwa na maudhui yaleyale ,”amesema Doreen.
Amesema wamelazimika kujitokeza kujibu hilo, kwa kuwa taasisi zote mbili zinaonekana kuwa na maslahi mengine ya kiharakati, huku akitaka waelewe kwamba suala la mirabaha sio la kiuanaharakati.
Doreen ameeleza kuwa wanachama wote wa Cosota wenye maswali , hoja, ushauri au maoni kuhusu mirabaha iliyotolewa, walipatiwa maelezo.
Tukio la ugawaji mirabaha lilifanyika Januari 28, mwaka huu, katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na Sh312 milioni zilikusanywa kutoka kwenye kazi 5,924 huku wasanii 1,123 wakinufaika na mgao huo.
Moja ya hoja za CNIT katika mchakato huo, wamesema mirabaha hiyo ilikusanywa kwenye redio saba pekee.
Akijibu hilo, Doreen amesema halina ukweli kwa sababu ukusanywaji wa mirabaha hiyo umefanywa kwenye vyanzo mbalimbali ukiachilia TV na redio, zipo baa, hoteli na kumbi mbalimbali za starehe.
Wakati kuhusu hoja ya kuwa mirabaha ililipwa kwa wanamuziki tu, Doreen amesema “sio wasanii tu walionufaika katika mgao huu,bali wapo wadau wengine wakiwemo watayarishaji.
Katika hili amefafanua kuwa kazi za Sanaa zina utofauti wake kisheria na kutolea mfano sheria na kanuni za hakimiliki zinaruhusu wasanii wa filamu na fani nyingine kuingia mikataba ya moja kwa moja na watumiaji wa kazi zao ambapo kwa kufanya hivyo nao hulipwa mirabaha.
Hoja nyingine ilikuwa ni kokosekana kwa uwazi na haijulikani wapi Cosota huwasilisha taarifa za hesabu zake.
“Dai hili ni la ajabu kwani Cosota kama zilivyo taasisi zingine za serikali huripoti taarifa zake kwenye bodi inayoisimamia taasisi na hesabu zake hukaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.