Burna Boy anavyopindua meza kwa Diamond Afrika

MSHINDI wa Grammy kutokea nchini Nigeria, Burna Boy tayari amefanikiwa kukwea hadi nafasi ya kwanza kama mwanamuziki aliyetazamwa zaidi (most viewed) katika mtandaoni wa YouTube ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika.

Kwa matokeo hayo, Burna Boy ameivunjilia mbali rekodi ya Staa wa Bongofleva kutokea WCB Wasafi, Diamond Platnumz ambaye aliongoza kwa zaidi ya miaka minne na sasa ameshuka hadi nafasi ya pili.

Utakumbuka Burna Boy alianza kuvuma Afrika mwaka 2012 baada ya kuachia ngoma yake, Like to Party kutoka kwenye albamu yake, L.I.F.E (Leaving ana Impact for Eternity) iliyokuja kutoka Agosti 12, 2013.

Albamu yake ya tano, Twice As Tall (2020) ilishinda tuzo ya Grammy kama Albamu Bora ya Muziki Duniani, huku akiweka rekodi kama msanii kwanza Nigeria kuwania Grammy mara mbili mfululizo baada ya albamu yake, African Giant (2019) kufanya hivyo awali.

Na sasa Burna Boy amefikisha ‘views’ zaidi ya bilioni 2.32 YouTube na kumpiku Diamond ambaye ana ‘views’ bilioni 2.28 Diamond anasalia kuwa kinara ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ila Kusini mwa Jangwa la Sahara tena.

Ikumbukwe Wizkid wa Nigeria amesalia nafasi ya tatu akiwa na ‘views’ bilioni 1.78, kisha Davido (Nigeria) - bilioni 1.43, Rema (Nigeria) - bilioni 1.31, Ckay (Nigeria) - bilioni 1.26, Mr. Flavour (Nigeria) - bilioni 1.16 na P Square (Nigeria) - bilioni 1.13.

Hata hivyo, bado Diamond anaendelea kuongoza kwa wafuasi (subscribers) YouTube Kusini mwa Jangwa la Sahara akiwa nao milioni 8.1, huku Burna Boy akiwa na milioni 4.2.

Burna Boy amekua kwa kasi YouTube kuliko Diamond, hiyo ni kutokana kujiunga na mtandao huo Januari 13, 2018 wakati Diamond alijiunga Juni 12, 2011, hivyo wamepishana miaka saba na Burna Boy kutumia miaka mitano kupindua meza na kuwa kinara. 

Licha ya Diamond kutangulia miaka saba mbele, amekuja kupitwa kutokana na kushindwa kutengeneza video za muziki zenye namba kubwa, badala yake amekuwa na video nyingi za matukio mbalimbali hadi matangazo ambazo ndizo hasa zilikuwa zinambeba. 

Utakumbuka hadi leo hakuna video ya wimbo ambao Diamond kafanya pekee yake (solo) iliyofikisha ‘views’ milioni 100, zote ambazo zimefanya hivyo kawashirikisha wasanii wengine tena wakubwa kwake kimuziki au kwa wakati huo walikuwa wanafanya vizuri zaidi.

Diamond ana nyimbo tatu zilizofikisha ‘views’ zaidi ya milioni 100 ambazo ni Yope Remix akishirikiana na Innoss’B, Inama akimshirikisha Fally Ipupa na Waah! akimshirikisha Koffi Olomide, wasanii wote aliowashirikisha ni kutokea DR Congo.

Video za nyinbo ambazo Diamond kafanya pekee yake na kufanya vizuri YouTube kwa kiasi chake ni Jeje - ‘views’ milioni 87, Sikomi (mil. 63) na The One (mil. 44), hivyo tunaweza kusema Diamond amekuwa akibebwa zaidi na kolabo anazofanya na wasanii wengine.

Hii ni tofauti kabisa na Burna Boy ambaye amekuwa akitengeneza ngoma kubwa mwenyewe na video zake zinafanya vizuri, mfano kuna On The Low (mil. 350), Ye (mil. 245), Last Last (mil. 227) na Gbona (mil. 103).

Ikumbukwe hata video za Diamond ambazo zimefikisha ‘views’ zaidi ya milioni 100, hakuna iliyofanya hivyo ndani ya mwaka mmoja ila Burna Boy kafanya hivyo mara tatu kupitia nyimbo zake kama For My Hand, On The Low na Ye.

Katika orodha ya video 10 za muziki zilizotazamwa zaidi YouTube Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa muda wote, Burna Boy kaingiza video mbili, On The Low na Ye, huku Diamond akiwa ametupwa nje katika orodha hiyo baada ya ngoma kama Calm Down ya Rema,  Love Nwantiti ya Ckay na  Joro ya Wizkid kufanya vizuri.

Kitendo cha Burna Boy kumshusha Diamond, ni safari yake ya kuwa namba moja Afrika kwa kila kitu, hadi sasa ndiye mwanamuziki aliyesikilizwa zaidi (most streamed) katika mtandao wa Boomplay Music akiwa na ‘streams’ zaidi ya bilioni 1. Anaongoza Afrika kuwa na wafuasi wengi Spotify ambao ni zaidi ya milioni 6, huku akiwa na wastani wa kupata wasikilizaji (monthly listeners) zaidi ya milioni 17 kwa mwezi. Burna Boy ndiye mwanamuziki wa kwanza Afrika kushinda tuzo za BET kwa mara tatu mfululizo, alifanya hivyo mwaka 2019, 2020 na 2021 na kwa jumla ameshinda tuzo nne za BET sawa na Wizkid na ndio vinara kwa Afrika.

Albamu yake ya sita, Love Damini (2022) yenye nyimbo kali kama Kilometre na Last Last, ndio albamu ya Afrika iliyofanya vizuri zaidi Billboard 200 ikitawala chati za Billboard Marekani, Uholanzi, Uingereza na Ufaransa. Na ameweza kushirikiana na wasanii wakubwa duniani kama Beyonce, Major Lazer, Rita Ora, Ed Sheeran na kadhalika