BONGO MUSIC FACTS: Zuchu amtosa Rayvanny dakika za jioooni!

Muktasari:
- Ametoa EP moja, I Am Zuchu (2020), ameshinda tuzo tatu za AFRIMMA 2020 & 2022 na tuzo tano za TMA 2022, huku akitumbuiza katika majukwaa makubwa Afrika kama Soundcity MVP Awards na Trace Awards. Huyu ndiye Zuchu.
NDANI ya miaka minne katika Bongo Fleva, Zuchu amefanikiwa kuwa mwimbaji mwenye ushawishi mkubwa kisanaa, kimauzo na kichapa kitu kinachomtofautisha na wengi hata aliyowakuta katika tasnia hiyo.
Ametoa EP moja, I Am Zuchu (2020), ameshinda tuzo tatu za AFRIMMA 2020 & 2022 na tuzo tano za TMA 2022, huku akitumbuiza katika majukwaa makubwa Afrika kama Soundcity MVP Awards na Trace Awards. Huyu ndiye Zuchu.
1. Tuzo ya kwanza Zuchu kushinda katika muziki wake inatokea Marekani, African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2020 aliposhinda kama Msanii Bora Chupukizi ikiwa ni sawa na Harmonize aliyeshinda kipengele hicho mwaka 2016.
2. Zuchu anatazamwa zaidi YouTube nje kuliko Tanzania, mathalani mwaka uliopita alipata ‘views’ zaidi ya milioni 75 kutoka Kenya huku nyumbani kwao Tanzania akipata ‘views’ milioni 28 ikiwa asilimia 21 ya kile alichokipata Kenya.
3. Tangu kurejea kwa tuzo za muziki Tanzania (TMA) mwaka 2021, Zuchu ndiye msanii wa kike aliyeshinda tuzo nyingi ambazo ni tano, anafuatiwa na mshindi wa Bongo Star Search (BSS) 2018, Phina aliyeshinda nne, kisha Nandy aliyenyakua tatu.
Utakumbuka tuzo za TMA zilizoanzishwa mwaka 1999 na Baraza la Sanaa Taifa (Basata), tangu 2015 zilikuwa zimesimama, hivyo wakati zinarejea ndio ilikuwa mara ya kwanza kwa Zuchu, Phina na Nandy kushiriki.
4. Tangu kutambulishwa WCB Wasafi hapo Aprili 2020, Zuchu ndiye msanii pekee wa kike Bongo aliyeshirikiana mara nyingi zaidi na Diamond Platnumz wakitoa pamoja nyimbo nne, Cheche (2020), Litawachoma (2020), Mtasubiri (2022) na Raha (2024).
5. Zuchu ni msanii pekee wa kike aliyeshirikishwa katika EP ya kwanza kutoka kwa Diamond, First Of All (2022) iliyoachia na nyimbo 10 ambazo saba kati ya hizo zilitengenezwa na S2kizzy kutoka studio za Pluto Repulic.
6. Huyu ni msanii namba moja kusini mwa jangwa la Sahara ambaye anaongoza kwa kuwa na wafuasi (subscribers) wengi YouTube akiwa nao milioni 3.3 tangu ajiunge na mtandao huo hapo Januari 2019.
Hata hivyo, kwa Afrika nzima Zuchu ni namba tatu akiwa ametanguliwa na Sherine wa Misri mwenye wafuasi milioni 5.5, kisha Zina Daoudia kutoka Morocco mwenye wafuasi milioni 3.7.
7. Zuchu ndiye msanii wa kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kwa wimbo wake wa solo, Sukari (2021) kufikisha ‘views’ milioni 100 YouTube, pia akiweka rekodi kama msanii wa kwanza wa kike kufikia namba hizo.
8. Nyimbo za Bongofleva zilizotangulia kuweka rekodi hiyo ni Kwangwaru (2018) wa Harmonize na Diamond, Yope Remix (2019) wa Diamond na Innoss’B, Inama (2019) wa Diamond na Fally Ipupa, Waah! (2020), Achii (2023) zake Diamond akiwa na Koffi Olomide.
9. Tangu ametoka kimuziki, Zuchu hajamshirikisha msanii yeyote wa Bongofleva nje ya WCB Wasafi katika nyimbo zake, na waliofanikiwa kumshirikisha ni Jux (Nidhibiti) na Darassa (Romeo) pekee na nyimbo zote hizo hazijafanyiwa video.
10. Rayvanny alikuwepo katika wimbo wa Zuchu, Siji (2024) ila vesi yake ikachomolewa dakika za jioni kabisa kabla ngoma hiyo kutoka na hakupewa taarifa huku nafasi yake ikichukuliwa na Toss wa Afrika Kusini aliyesikika katika ngoma hiyo.
Hata hivyo, sio mara ya kwanza kwa Rayvanny kutolewa katika wimbo baada ya kurekodi, miongoni mwa nyimbo alizotolewa ni Riziki (2012) wa Tip Top Connection, Pombe Yangu (2013) wa Madee, Nitakupwerepweta (2015) wa Yamoto Band na Shikorobo (2015) wa Shetta.