Billnass ajilipua ishu ya afya ya akili

Muktasari:
- Staa huyo ambaye ni mume wa mwimbaji wa kike nchini, Nandy, ameliambia Mwanaspoti kuwa usupastaa una changamoto zake na kama msanii hajajiandaa na maisha ya umaarufu ni rahisi kupata tatizo la afya ya akili na kumvuruga kabisa katika ndoto zake kisanii.
MSANII maarufu wa Bongo Fleva, William Lyimo ‘BillNass’ ameshindwa kujizuia na kujilipua kuhusu ishu ya tatizo la afya ya akili kwa kuwataka vijana wadogo wenye vipaji wanaotamani kuingia kwenye tasnia ya muziki na sanaa kwa ujumla wajiandae kukabiliana na changamoto inayotokana na usupastaa.
Staa huyo ambaye ni mume wa mwimbaji wa kike nchini, Nandy, ameliambia Mwanaspoti kuwa usupastaa una changamoto zake na kama msanii hajajiandaa na maisha ya umaarufu ni rahisi kupata tatizo la afya ya akili na kumvuruga kabisa katika ndoto zake kisanii.
BillNass alisema mafanikio katika kazi hizo yanahitaji uvumilivu mkubwa kwa sababu tasnia hiyo imejaa changamoto nyingi.
“Huu ni kama ushauri wangu kwa vijana wadogo wenye vipaji wanaotamani kuingia katika tasnia ya muziki na sanaa kwa ujumla, kwanza wanatakiwa kumtanguliza Mungu mbele ya safari kwani, kuna changamoto na zinajumuisha vita, usaliti, ushetani na dhuluma kutoka kwa baadhi ya wadau wa sanaa wakiwamo mameneja, kampuni za usambazaji na hata lebo,” alisema BillNass na kuongeza; “Ingawa wengi huingia katika sanaa kwa matarajio ya utajiri na mafanikio, ukweli ni kwamba kuna hatari zaidi za kupatwa na msongo wa mawazo, magonjwa ya akili, kuchanganyikiwa na hata kupoteza maisha.”
Staa huyo wa ngoma kama Boda, Puuh, Mabosi Bye, Maokoto na nyingine alisema msanii ambaye hakujiandaa kukabiliana na changamoto hizo ni rahisi kuvurugwa na kushindwa kutimiza ndoto alizokuwa nazo, ndio maana anawakumbusha mapema wajipange wa wasirahisishe mambo tu.