Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Baada ya Bill Nenga, anafuata Alikiba kwa Nandy

Muktasari:

  • Nandy aliyetoka kimuziki chini ya Tanzania House Talent (THT) kupitia wimbo wake, Nagusagusa (2016), wasanii alioshirikiana nao zaidi hadi sasa ni Billnass na Alikiba huku kazi hizo zikifanya vizuri hasa katika majukwaa ya kidijitali.

STAA wa Bongofleva kutokea The African Princess Label, Nandy kwa miaka yake tisa ya umaarufu katika muziki ameshirikiana na wasanii wenzake wengi hadi kuiumba dunia yake kwa Billnass na Alikiba, mshindi wa MTV EMAs 2016. 

Nandy aliyetoka kimuziki chini ya Tanzania House Talent (THT) kupitia wimbo wake, Nagusagusa (2016), wasanii alioshirikiana nao zaidi hadi sasa ni Billnass na Alikiba huku kazi hizo zikifanya vizuri hasa katika majukwaa ya kidijitali.

Huyu ndiye Msanii Bora wa Kike kwa mujibu wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023, na tayari ametoa Extended Playlist (EP) tatu, Wanibariki (2021), Taste (2021) na Maturity (2022), pamoja albamu moja, The African Princess (2018).

Mwishoni mwa mwaka uliopita Nandy alitoa wimbo wake, Totorimi (2024) akimshirikisha Billnass ukiwa ni wa kwanza kuachia tangu wamefunga ndoa hapo Julai 16, 2022 ikiwa ni takribani miaka sita ya uhusiano wao ulioanzia huko Mbeya katika tamasha la Fiesta. 

Kwa ujumla mastaa hao ambao ni wazazi wa mtoto mmoja Naya, tayari wameshirikiana katika nyimbo tano ambazo ni Bugana (2019), Do Me (2020), Party (2021), Bye (2022) na Totorimi (2024) ambao video yake (visualiser) inaonyesha mjengo wao mpya.

Nandy ambaye tuzo yake ya kwanza kushinda ilitoka All Africa Music Awards (AFRIMA) 2017 kama Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki, katika video yake, Totorimi (2024) amempa nafasi dada wao wa kazi za ndani Memo uhusika na amefanya vizuri.

Vilevile Nandy ameingiza sauti za chini katika wimbo wa Billnass, Sina Jambo (2017), huku naye Billnass akitokea katika video ya wimbo wa Nandy, Napona (2022) kutoka katika EP yake, Maturity (2022) na kumshirikisha Oxlade kutokea Nigeria.

Kwa namna Nandy na Billnass wameshirikiana mara nyingi kimuziki, inatukumbusha ilivyokuwa kwa Lady Jaydee na Mwana FA ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Ikumbukwe Lady Jaydee, mwanamuziki aliyetoa albamu tisa, yeye na Mwana FA walitoa nyimbo kama Sitoamka (2002), Wanaume kama Mabinti (2003), Alikufa kwa Ngoma (2004), Hawajui (2005), Msiache Kuongea (2009) n.k.

Mbali na Billnass, Alikiba kutokea Kings Music ni msanii mwingine Bongo ambaye Nandy ameshirikiana naye sana katika muziki wakiwa tayari wametoa nyimbo tatu pamoja huku mbili kati ya hizo zikiwa za African Princess huyo.

Nandy ndiye alianza kumpa shavu Alikiba katika wimbo wake, Nibakishie (2020) ambao picha zilizopigwa katika utayarishaji wa video yake ziligeuka gumzo mtandaoni ukingatia wakati huo tayari alishaweka wazi uhusiano wake na Billnass.

Na mapema mwaka uliopita akatoa tena wimbo mwingine na Alikiba, Dah! (2024), huu ni miongoni mwa nyimbo za Nandy zilizopata mapokezi makubwa ndani ya muda mfupi, mathalani video yake imetazamwa zaidi mara milioni 17 YouTube.

Pia wimbo huu ambao Billnass ameshiriki kuandika kwa sehemu, ulitoka kwa ajili ya harusi ya aliyekuwa msemaji wa Yanga na Simba SC, Haji Manara na Zaiylissa, ndoa ambayo ishavunjika. 

Kwa upande wake Alikiba kupitia EP yake ya kwanza, Starter (2024) yenye nyimbo saba, ndipo amemshirikisha Nandy ambaye amesikika katika wimbo ‘Bailando’ uliofanya vizuri, hivyo kwa ujumla wawili hawa wametoa kolabo tatu pamoja.

Ikumbukwe Alikiba alikaa miaka 10 bila kumshirikisha msanii yeyote wa kike katika wimbo wake, tangu alipotoa kolabo yake na Lady Jaydee, Single Boy (2012), hakufanya hivyo hadi alipokuja kumshirikisha Sabaha Salum katika wimbo wake, Yalaiti (2023). 

Hata hivyo, kwa kipindi hicho Alikiba alikuwa akishirikishwa na wasanii wa kike kutoka ndani na nje, miongoni mwao ni Nandy (Nibakishie), Maua Sama (Niteke Remix) na Maud Elka (Songi Songi Remix) kutokea DR Congo.

Ukiachana na Billnass na Alikiba, pia Nandy amekuwa akishirikiana na wasanii wenzake wa kike, mathalani miaka ya hivi karibuni amesikika katika nyimbo za Lulu Diva (Cheketu), Mimi Mars (Pole), Maua Sama (Poa), Yammi (Lonely) n.k.

Na lebo yake ya The African Princess ni kwa ajili ya wasanii wa kike tu, tayari amemsaini Yammi ambaye alitoka na EP yake, Three Hearts (2023) iliyofanya vizuri hadi kuchaguliwa kuwania tuzo za TMA kama Msanii Bora Chipukizi 2023.

Hata hivyo, Yammi sio msanii wa kwanza Bongo kutambulishwa na lebo yake kupitia EP, kuna Zuchu alitambulishwa na WCB Wasafi kupitia EP yake, I Am Zuchu (2020) na Mac Voice aliyetambulishwa na Next Level Music (NLM) kupitia EP, My Voice (2021).

Tangu amesainiwa The African Princess label, Yammi ametamba na nyimbo kama Namchukia (2023), Tunapendezana (2023) na Tiririka (2023) ambao video yake tayari imetazamwa zaidi ya mara milioni 10 YouTube.