AY awaandalia sapraizi mashabiki Bongo Fleva Honors

Muktasari:

  • AY kesho Ijumaa atafanya shoo kwenye ukumbi wa Ware House, Oysterbay ikiwa ni muendelezo wa Tamasha la Bongo Fleva Honors ambalo hutuza magwiji wa Bongofleva.

Mwanamuziki, Ambwene Yesaya (AY) amesema amewaandalia sapraizi mashabiki wa tamasha la Bongo fleva Honors lililoingia msimu wa pili.

AY keshokutwa Ijumaa atafanya shoo kwenye ukumbi wa Ware House, Oysterbay ikiwa ni muendelezo wa Tamasha la Bongo Fleva Honors ambalo hutuza magwiji wa Bongofleva.

Akizungumzia shoo hiyo inayohusisha wasanii wakongwe wa Bongofleva, AY alisema itakuwa ni shoo ya tofauti akisisitiza kwamba itawapa sapraizi mashabiki watakaojitokeza.

"Nimekuwa nikifanya kazi na wasanii mbalimbali wa ndani na nje ya nchi tangu mwaka 2000 hadi sasa (2024) hivyo miongoni mwa niliofanya nao kazi watakuwapo siku hiyo na itakuwa na sapraizi kwa mashabiki wangu wa Bongo Fleva Honors," alisema AY.

Alisema, amejiandaa kufanya shoo ya 'laivu', ambayo mashabiki wataamua aimbe nyimbo ngapi, kwani hata 30 wakitaka ataimba.

Akizungumzia tamasha hilo, mratibu wake Joseph Mbilinyi amesema hivi sasa litakuwa likifanyika kila baada ya miezi mitatu tofauti na msimu wa kwanza lilipokuwa linafanyika kila mwaka.

"Sisi (Deiwaka World) kwa kushirikiana na Kings Empire na EFM tumeamua kulifanya kila baada ya miezi mitatu ili kumpa nafasi msanii atakayepafomu kujiandaa kwa kiwango kikubwa zaidi," alisema.

Alisema, msimu wa kwanza walioifanya kwa ushirikiano na Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa na Wasafi Tv mwaka 2023 kiliwapa fursa wasanii kama Dully Sykes, TID, Juma Nature, Jay Mo, Mr Blue, Gangwe Mob, Wagosi wa Kaya na Banana Zoro kutumbuiza mbashara.

"Msimu wa pili, tulianza na Mr Nice kisha Matonya na Ijumaa (kesho) ni AY, wengi tunafahamu mchango wa msanii huyu katika mafanikio ya muziki wa Bongo Fleva, hivyo shoo yake itakuwa ni zaidi ya shoo," alisema.

Meneja mkuu wa Ware House, Clara Premsingh (Keiiy) alisema milango itakuwa wazi mapema kwa mashabiki kuanza kuingia.

Kiingilio katika tamasha hilo ni Sh20,000 kwa viti vya kawaida, Sh50,000 kwa VIP na Sh3 milioni kwa VVIP ambayo ni meza ya watu wanane hadi 10.

Mkurugenzi wa mauzo na masoko wa ETV na EFM, Denis Sebo alisema tamasha hilo linatoa hamasa kwa wanamuziki wa zamani na kuwapa maua yao mapema wakiwa hai.

"Hili ni tamasha la kuwaenzi wasanii hawa wakiwa hai, wote tunafahamu ubora wa kazi zao, limekuja wakati sahihi kwa ubora sahihi, na kwa wasanii sahihi," alisema.