Alikiba kuachia albamu rasmi Oktoba 7, aipa jina la ‘Only One King’

Wednesday September 29 2021
kiba pic
By Nasra Abdallah

Hatimaye msanii wa muziki wa Bongofleva nchini Tanzania Alikiba, ametaja siku anayotarajia kuachia  albamu yake mpya ambayo ni  Oktoba 7.
Kiba ametangaza ujio wa albamu hiyo leo Jumatano Septemba 29,2021jijini Dar es Salaam, ambapo pia aliitambulisha kwa jina kuwa itaitwa  ‘Only One King’.
Ujio huo wa albamu, Alikiba alianza kuutangaza tangu mwishoni mwa mwaka jana, lakini hakuweka wazi kuwa ni lini haswa ataiachia.
Badala yake alikuwa akiachia nyimbo moja moja tangu mwaka umeanza na mpaka sasa ana nyimbo zisipungua nne huku zote zikiwa zinafanya vizuri.
Hii itakuwa albamu ya tatu  kwa msanii huyo ikitanguliwa na ‘Cinderela’ iliyotoka mwaka 2007 na kufuatiwa na ile ya  ‘Ali K 4real’ aliyoitoa mwaka 2009.
Katika nyimbo alizoachia ipo ya Jelous aliyoimba na msanii Mayorkun kutoka nchini Nigeria, ambayo ndio inaongoza katika nyimbo zake alizotoa mwaka huu kutazamwa mara nyingi youtube kwa kuwa na watazamaji milioni saba.
Ipo  pia nyimbo ya ‘Salute’ aliyomshirikisha Rudeboy naye msanii kutoka nchini Nigeria ambaye zamani walikuwa wanaunda kundi la P.Square.
Nyingine ni wimbo wa ‘Ndombolo’ alioimba kwa kuwashirikisha wasanii wa lebo yake ya Kings music akiwemo mdogo wake Abdukiba, K2GA na Tom Flavour.
Wimbo wa nne ni wa Infidele, alioachia Januari mwaka huu.

Advertisement