Alikiba, Harmonize mabalozi wa 'Safisha, Pendezesha' Dar

Dar es Salaam. Wasanii wa muziki wa Bongofleva, Ali Saleh 'Alikiba' na Rajabu Abdul 'Harmonize'  wameteuliwa kuwa mabalozi wa  'Safisha,Pendezesha' Dar es Salaam.

Hayo yamebainika leo Jumatatu Desemba 22, 2021 katika
uzinduzi wa mkakati wa usafi na uhifadhi wa mazingira mkoa wa Dar es Salaam uliopewa jina la 'Safisha, Pendezesha'  Dar es Salaam' na kufanyika ukumbi wa Mwalimu Nyerere.

Mkakati huo unakuja baada ya kufanyika kwa  shughuli ya kuwahamisha wamachinga katika maeneo yasiyo rasmi.

Maeneo hayo ni pamoja na barabara za waenda kwa miguu, hifadhi za barabara, maeneo ya shule na  taasisi za serikali na juu ya mitaro.

Akizungumza katika hafla hiyo, AliKiba, alipongeza shughuli ya kuwahamisha wafanyabiashara hao ilivyofanyika  na kuwataka wajue kwamba serikali ina nia nzuri kwani  hata wateja wenyewe wanataka kupata huduma katika sehemu iliyo safi.

Amesema kama balozi, anawahamasisha watu kuzingatia usafi na kuwa kama nchi za mbele ambazo ukipita unaona hata aibu kutupa taka na kuongeza kuwa hata yeye anaamini asingekuwa msafi watu wasingempenda.

Wakati Harmonize alisema anafurahi kuwa balozi, na atahakikisha anatumia nafasi yake kuifanya Dar es Salaam inakuwa safi,huku akitamani kuiona inakuwa kama nchi ya Australia.