Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Albamu ya Young Lunya ‘Mbuzi’ ni chapa ya hip hop

Muktasari:

  • Mradi huo unakuja miaka mitatu baada ya Lunya kufanya vizuri na wimbo wake, Mbuzi (2021) uliomuwezesha kushinda tuzo mbili za muziki Tanzania (TMA) 2021 kama Wimbo Bora wa Hip Hop na Msanii Bora wa Hip Hop.

Albamu mpya ya Young Lunya, Mbuzi (2024) yenye nyimbo 11 na kushirikisha wasanii 10 kutoka nchi nne tofauti, inatoa picha kamili kwanini amekuwa rapa mwenye ushawishi mkubwa wa kichapa nchini.

Mradi huo unakuja miaka mitatu baada ya Lunya kufanya vizuri na wimbo wake, Mbuzi (2021) uliomuwezesha kushinda tuzo mbili za muziki Tanzania (TMA) 2021 kama Wimbo Bora wa Hip Hop na Msanii Bora wa Hip Hop. Kwa mujibu wa Lunya, amekuwa akijiita Mbuzi yaani G.O.A.T akimaanisha the Greatest of All Time (Bora wa Muda Wote) kutokana na kuutumikia muziki huo kwa miaka zaidi ya 10 katika ubora usiochuja.

Mbuzi ni albamu ya kwanza kwa Lunya tangu kusaini RockStar Africa na Sony Music hapo Juni 2022 akiwa ni msanii wa kwanza wa Hip Hop Bongo kupata dili hilo kubwa la usimamizi na usambazaji wa muziki wake duniani.

Wasanii wa Tanzania walioshiriki albamu hiyo ni Marioo, Country Wizzy, Abigail Chams, Jay Melody, Mr. II Sugu, D Voice na Micky Singer na wengine kutoka nje ni Dutchavelli (Uingereza), Khaligraph Jones (Kenya) na Jay Rox (Zambia). Kwa kutambua ukubwa wa albamu hiyo tunaangazia nyimbo zake tatu zenye mahadhi ya Hip Hop. Hizi tatu tumezichagua kwa msingi wa moja aliyomshirikisha msanii wa ndani, nyingine wa nje na kuzingatia usawa wa kijinsia ila sio maana ni kali kuzidi hizo nyingine.


1. Watoto wa Juzi ft. Sugu & Country Wizzy

Katika wimbo ‘Watoto wa Juzi’, Young Lunya amekaa katika mdundo mmoja na kaka zake kimuziki, Mr. II Sugu na Country Wizzy kisha wote kushusha mistari ya majigambo kama ulivyo utamaduni wa Hip Hop kwa miaka yote.

Hatua ya Sugu ambaye ni Msanii Bora wa Hip Hop 2000 kwa mujibu wa TMA kukubali kushiriki katika wimbo huo ni wazi kwamba naye anaona kuwa Lunya anautendea haki muziki huo kwa sasa upande wa uandishi, miondoko na chapa.

Sugu ambaye ni msanii wa kwanza Bongo kununua gari aina ya Honda Accord Inspire baada ya kuamua kuuza  mwenyewe albamu yake ya nne, Nje ya Bongo (1999), ni mkongwe mwingine wa Hip Hop kufanya kazi na Young Lunya baada ya Profesa Jay.

Utakumbuka Young Lunya ambaye aliunda kundi la OMG na wenzake wawili Salmin Swaggz na Conboi, hapo awali aliwahi kushirikiana na wasanii wengine wa Hip Hop kama Joh Makini, Moni Centrozone, Rosa Ree, Nikki wa Pili, Msamiati, Rapcha, Frida Amani na kadhalika.


2. Natoka Na Nani ft. Khaligraph Jones

Ni ngoma ya mapenzi ambayo Young Lunya na Khaligraph Jones a.k.a OG au Omollo kutoka Kenya wanamfukuzia mrembo mmoja lakini hawataki hadi pale atakapojua wanatoka na nani kwa sasa ndipo wapate nafasi kwake.

Huu ni wimbo wa pili kwa Lunya kumshirikisha Khaligraph baada ya Stupid (2023) uliotoka muda mfupi baada OG kuteka mazungumzo kufuatia kauli yake kuwa muziki wa Hip Hop Tanzania umeshuka na kufafanua hilo kupitia ngoma yake, Bongo Favour.

Khaligraph, mshindi wa TMA 2022 kama Msanii Bora Afrika Mashariki, na AFRIMMA 2020 kama Msanii Bora wa Hip Hop Afrika, kama kawaida yake katika wimbo huu (Natoka Na Nani) ametumia lugha mbili, Kiingereza na Kiswahili kumshawishi mrembo huyo.

Ukiachana na Young Lunya, wasanii wengine wa Hip Hop Bongo waliowahi kufanya kazi na Khaligraph Jones ni pamoja na Nikki Mbishi, Rosa Ree, Roma & Stamina (Rostam), One The Incredible, Conboi, Young Killer, Country Wizzy, Mex Cortez na kadhalika.


3. Toxic ft. Abigail Chams

Baada ya Abigail Chams kuambiwa kuwa mpenzi wake ana mpenzi mwingine nje na anafanya mambo yasiyopendeza, basi katika wimbo huo ‘Toxic’, anatema nyongo na kusema msichana kama yeye hawezi kumpata hata akizunguka sana huko nje maana hakuna wa kufanana naye.

Juu ya mdundo wa Ammy, Young Lunya anamjibu Abigail na kumwambia aache mapepe kabla hajasikia kateka huko Magomeni na ‘jimama’ linalohonga biashara na fedha, na hapo ndio atajua anatoka na ‘gang’ ingawa hawajawahi kumuona na magenge.

Abigail ambaye naye yupo Sony Music na RockStar Africa, kwa hakika tangu mwanzo ameunogesha vilivyo wimbo huu kwa melodi tamu na matata kama alivyofanya katika nyimbo zake kama U & I (2022), Closer (2022), Nani? (2023), Milele (2023) na kadhalika.

Mbali na Lunya wasanii wengine wa Bongofleva waliowahi kumshirisha Abigail Chams katika nyimbo zao na kuzitendea haki ni pamoja na Harmonize (Leave Me Alone), Rosa Ree (Mulla), Platform (Zoba), Rayvanny (Stay) na Mimi Mars (Haina Maana).