Afya ya Mkubwa Fella yazidi kuimarika

Muktasari:
- Fella alisema kutokana na hali yake kuwa mbaya kwa matatizo hayo, alikata tamaa ya kupona na anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa sasa anaongea vizuri na anaendelea na mazoezi na Mungu akipenda atarudi sawa kama zamani.
MIEZI michache iliyopita, Mwanaspoti liliripoti hali ya kiafya ya Meneja wa msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, Said Fella 'Mkubwa Fella' alikuwa akisumbuliwa na presha na kupooza miguu, amefunguka kwa sasa ana furaha na amezidi kuimarika.
Fella alisema kutokana na hali yake kuwa mbaya kwa matatizo hayo, alikata tamaa ya kupona na anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa sasa anaongea vizuri na anaendelea na mazoezi na Mungu akipenda atarudi sawa kama zamani.
“Nina furaha kwani kwa sasa naendelea vizuri, hali yangu inaimarika kila siku na nimeanza kufanya mazoezi ya kutembea kila ifikapo jioni.
"Ukweli mimi nimeumwa sana yaani nimeumwa kweli hadi nikawa nimekata tamaa ya kupona, ila namshukuru Mungu sana hadi sasa naweza kuongea na wewe hivi na kutembea vizuru kwa kufanya mzoezi, ilikuwa balaa” alisema Mkubwa Fella.
Taarifa za kuumwa kwa Said Fella ‘Mkubwa Fella’ ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii kuwa amepoza miguu huku wengi wakidai Diamond amemtelekeza.
Mwanaspoti baada ya kupata taarifa hizo ilimtafuata nyumbani kwake Mbagala kata ya Kilungule, jijini Dar es Salaam na kuzungumza na baadhi ya ndugu zake ambao walidai hali yake haikuwa nzuri hata kuzungumza na mtu kwa muda mrefu.