2024 ukilinganisha sanaa yetu bongo, majuu na ukweli

New Content Item (1)
New Content Item (1)

MWAKA 2024 tukimsikia mtu anasema sitazami Bongo Movie kwa sababu hazina ubora kama muvi za Ulaya na Hollywood, Marekani tutamkumbusha akiumwa asiende hospitali za Tanzania na akitaka kutoka sehemu moja kwenda nyingine asitumie barabara za Tanzania akatumie za Ulaya na Marekani kwa sababu ni bora kuliko huku.

Tukimsikia mtu anasema nyimbo za Nandy na Zuchu za nini wakati hazina ‘kwaliti’ kama za Beyonce na Cardi, tutamkumbusha kwamba hata intaneti, umeme, maji na huduma zingine akazipate hukohuko kwa kina Beyonce na Cardi kwa sababu ukizilinganisha na kwetu za huko zina ubora zaidi.

Tutakuwa tunawakumbusha hivi kwa sababu ukweli ni kwamba kuna lawama wanapewa wasanii wetu kwa kuonewa. Mtu anataka Lamata atengeneze tamthilia kama Tyler Perry anazotengeneza Marekani. Kwa bajeti gani? Kwa wataalamu gani? Kwa uzoefu gani?

Mtu anataka filamu za Juma Saada ziwe na ubora kama James Cameron. Kwa pesa ipi? Kwa uzoefu gani? Unawezaje kutamani filamu kutoka kwenye kiwanda cha filamu chenye miaka zaidi ya 100 zinafanane kiwango na filamu kutoka kwenye kiwanda chenye miaka isiyozidi 20 na bajeti ndogo. Hizo ni ndoto za alinacha.

Kiwanda cha filamu cha Marekani maarufu kama Hollywood kina miaka zaidi ya 100 tangu kianzishwe. Hiyo ni sawa na kusema Hollywood ina umri mkubwa kuliko hata Tanzania ambayo imepata uhuru 1961.Na ukipewa filamu ya kwanza kutengenezwa Hollywood uitazame leo amini kwamba hutoboi hata dakika 10 utazima TV ukalale au utafute kingine cha kuangalia. Lakini baada ya wao kufanya kazi kwa miaka mingi, kujipa uzoefu, kukuza utaalamu wao kazi zao zikawa zinaendelea kila kukicha mpaka kufikia zilipo leo.

Lakini kwa sababu watu wanaokosoa sana kazi za sanaa za Bongo hawazingatii suala la muda ndiyo maana wanapata ya kuongea kiasi hiki.

Na ukitaka kuamini muda, uzoefu na utaalamu unatibu tazama filamu zetu za zamani. Filamu ambazo tulikuwa tunazatazama kwenye DVD zilikuwa na ‘kwaliti’ mbaya ukilinganisha na filamu za leo. Yote kwa sababu wataalamu wetu walikuwa hawajawa wataalamu na pia hawakuwa na vitendea kazi vya kutosha.

Tazama filamu za sasa. Picha zinaridhisha, sauti zinasikika, lokesheni zinaandaliwa. Kwa kifupi tumeendelea na tumepiga hatua kubwa ukifananisha na miaka ya mwanzoni mwa tasnia yetu.

Sasa kama ambavyo ukilinganisha huduma za kijamii za nchi zilizoendelea na nchi zinaondelea unaona ni vitu viwili visivyofanana, ndivyo vivyo hivyo ilivyo hata kwenye kazi za sanaa. Usitegemee video ya muziki ya Chid Benz kuwa na ubora mkubwa kuzidi video za Kanye. Pengine inawezekana lakini haitakiwi kuwa matarajio.

Lakini pia sio jambo ambalo litakuwa hivyo milele. Wasanii wetu wanakua, wanaongeza ujuzi, uzoefu na ubunifu na kuna siku watakuwa wanachuana sambamba na wasanii tunaowalinginasiha nao sasa hivi.