Konde Boy akubali yaishe kwa Kajala

Monday November 08 2021
Konde PIC
By Eliya Solomon

AKIWA kwenye mchakato wa kuachia albamu ya pili, nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Harmonize a.k.a Konde Boy amemuangukia aliyekuwa mpenziwe, Kajala Masanja akiomba msamaha kwa kilichotokea baina yao.

Harmonize, ambaye majina yake kamili ni Rajab Abdul Kahali alitumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kushea na mashabiki wake juu ya albamu hiyo inayokwenda kwa jina la High School yenye ngoma 20, ikiwemo Sandakalawe aliyoshirikiana na mkali kutoka Sauzi, Busiswa Gqulu.

Msanii huyo anayemiliki lebo ya Konde Music Worldwide, alimtaja Kajala kama mwanamke aliyemuonyesha mapenzi zaidi kati ya wote aliotoka nao na kuonyesha kujutia alichomkosea hadi kuachana kwao.

“Samahani kama nitamuumiza yeyote. Kajala alinijua vizuri, alikuwa anajua mimi ni mtu wa namna gani, napenda nini kwa wakati gani. Nadhani alikuwa ananifahamu vizuri.

“Sitaki kuingia sana ndani kuanza kuelezea ilikuwaje. Nataka kutumia nafasi hii kama mwanaume kumuomba msamaha kwa sababu chochote ambacho kimetokea najiona kuwa kama mimi ndiye nimesababisha. Sikupendezwa na kile ambacho kilitokea,” alisema Konde Boy.

Akiwa Los Angeles, California nchini Marekani alikoenda kikazi, Harmonize aliachia albamu ikiwa ni muda mfupi tu tangu aisikilize ‘live’ akiwa na mashabiki wake walioungana naye kwa njia ya mtandao usiku wa kuamkia juzi.

Advertisement

Hii ni albamu yake ya pili baada ya Afro East.

Kwenye High School, Konde Boy mbali na Busiswa Gqulu amewapa shavu wasanii wake wawili kutoka kwenye kundi lake la Konde Music Worldwide ambao Anjella na Ibraah, mkali wa Singeli, Sholo Mwamba naye ameshiriki kwenye album hiyo.

Advertisement