Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

'Kadansee la Mama' Lilivyokusanya kijiji, tatizo muda

Kadanse Pict

Muktasari:

Tamasha hilo ambalo lilishuhudia wasanii wengi mbalimbali wa Bongo Movies, Bongo Fleva na Taarabu pamoja na mashabiki wakifurika kwenye viwanja hivyo, lilikutanisha bendi za dansi 11.

LICHA ya Tamasha la  Muziki wa Dansi Tanzania 2025, 'Kadansee la Mama', kufana kwenye viwanja vya Leders Club Kinondoni jijini Dar es Salaam, usiku wa jana, Februari 1, wanamuziki wamelalamikia muda wa kutumbuiza kuwa mchache tofauti na walivyojipanga kutoa burudani.

Tamasha hilo ambalo lilishuhudia wasanii wengi mbalimbali wa Bongo Movies, Bongo Fleva na Taarabu pamoja na mashabiki wakifurika kwenye viwanja hivyo, lilikutanisha bendi za dansi 11 ambazo ni Msondo Ngoma, Sikinde Mlimani Park, Bogoss Musica, Twanga Pepeta, Tukuyu Sound, Mwenge Jazz, Mjengoni Classic, Nyuki Band ya Zanzibar, Muumini Mwinjuma na Specail Band, ToT Band na Fm Academia, huku kila moja ikipewa dakika 20 kwa mzunguko wa kwanza na dakika 10,   mzunguko wa pili.


Wasanii hawakubaki nyumbani

Baadhi ya wasanii wa fani mbalimbali walifika kwenye viwanja hivyo kupata burudani hiyo wakiwemo Asha Boko, Yusuf Mlela, Steve Nyerere, Mayasa Mrisho, Mishi Mziray, Mwanaheri, Fid Q, Meneja Kandoro wa Singeli, Ado Novemba mwimbaji wa muziki wa Injili na wengine wengi.


KAD 01

Dakika 20, lakini tamu

Ingawa bendi hizo zilipewa muda mchache wa kupanda jukwaani kutoa burudani, wanamuziki wa bendi hizo wamepongeza kuwepo kwa tamasha hilo licha ya kupewa muda mchache wa kutumbuiza.


Wakizungumza na mwanaspoti kwa nyakati tofauti, wamesema kwa jinsi walivyozoea kwenye shoo zao, muda uliotolewa jana haukuweza kukata kiu ya mashabiki zao na wapenzi wa burudani na kama litafanyika tena, wanaomba muda uongezwe kwani kawaida bendi zinapiga muziki muda mrefu tofauti na burudani nyingine.


Chaz Baba-Twanga Pepeta

"Kwanza tunashukuru sana kufanyika kwa tamasha hili. Ni muda mrefu sana tumelilia kufanyika kwa tamasha kubwa la namna hii. Hata hivyo, kuna kitu kimoja ambacho waandaaji hawakututendea haki, kutupa dakika 20 kila bendi, ukweli hii haijakaa sawa na haiwezekani dakika hizo 20 kupiga nyimbo hata tano ili mashabiki waridhike, muda ni mchache sana. Hata hivyo, tumepambana kubalansi kwenye kuimba jukwaanikwa hizo dakika 20. Nirudie tu tena kuwapongeza waandaaji, pia tamasha lijalo watupe hata dakika 45 au saa moja kwa kila bendi."


KAD 05

Patcho-FM Academia

"Kwanza nitoe pongezi kwa Katibu wa Basata kwa kutuletea hili tamasha. Tatizo muda waliotupa wa kupanda jukwaani ni mchache sana kwa mwanamuziki wa dansi, haiwezekani bendi ikapiga dakika 20 na mashabiki wakaridhika. Mie niwaombe tu tamasha hili litakapofanyika tena kwa mara nyingine watupe dakika za kutosha kwenye kutumbuiza, ila tumefurahi na kulipokea hili tamasha kwa mikono miwili."


KAD 03

Juma Katundu-Msondo ngoma

"Ukweli kwenye suala la muda tumebabwa sana, tena kwa nyimbo kama zetu ni ndefu sana, japo tumejitahidi kupiga na kukusanya kijiji cha watu, ila unaona kabisa bado mashabiki hawakuridhika kama wanavyokuwaga, mie nishauri tu, tamasha lingine likija bora wachague bendi chache na zipewe muda wa kutosha, lakini kwa hii ya dakika 20 za mwanzo na mzunguko wa pili dakika 10 hatukutendewa haki."


Kalala Junior-Tukuyu Sound

"Yaani kiukweli dakika 20 unawezaje kupiga nyimbo na mashabiki wakaridhika? Muda ni mchache sana. Kiukweli hizi dakika 20 zimetupa sisi wakati mgumu sana wa kutumbuiza jukwaani, ila kwa kuwa zimewekwa, basi tumepambana nazo hivyo hivyo kwa tabu sana, bora hata wangetuwekea dakika 45."


KAD 04

Nyoshi El Saadat-Bogoss Musica

"Kwa hizi dakika 20 hapana kabisa ni chache, yaani ili kutaka dansi liinuke zaidi kwenye matamasha kama haya, tupewe muda mwingi wa kutosha ili kuonyesha 'live band' vizuri. Ila kwa kuwa ni mara ya kwanza, hii haina tabu sana najua waandaaji watakuwa wametuelewa kilio chetu cha muda, siku nyingine watarekebisha na kutupa muda wa kutosha, ila tamasha ni zuri na nimelipenda sana."


KAD 02

Kwa nini dakika 20, majibu haya hapa

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Dkt. Kedmon E. Mapana, mwandaaji wa Tamasha hili akishirikiana na Wizira ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo ametoa sababu ya kwa nini wameweka dakika 20 kwa kila bendi.

"Kwanza nizipongeze bendi zote kwa kufanya vizuri katika tamasha hili la 'Kadansee la Mama', pili mashabiki kwa kufika kwa wingi. Hii imetupa matumaini ya kufahamu kumbe  dansi linapendwa. Kuhusu kutoa dakika 20 kwa kila bendi, ni ili kila bendi itumbuize na kwa mashabiki waendelee kuwapo uwanjani mwanzo hadi mwisho wa tamasha, maana tungesema tunaweka kila bendi saa mbili au moja tusingetoboa kwa muda huu wa saa 9 usiku bendi zote zikamalizika, hapa tungepiga hadi asubuhi saa 2, kuwa na bendi 11 jukwaani sio mchezo."

"Kingine ni kulitangaza tamasha hili kwa wadau, ili kupata kulitambua kwanza, sababu lengo letu ni kutaka kulifanya  endelevu, hivyo wanamuziki wasilalamike sana, pia tumepokea maoni yao na tutayafanyia kazi kwa kipindi kingine," amesema Mapana.

Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amesema haamini macho yake kwa umati wa watu waliojitokeza katika tamasha hilo, hiyo imeleta faraja dansi linapendwa na kwa mwaka huu watafanya matamasha matano hadi Desemba.

"Kiukweli kwa umati huu uliokusanyika nasema kuanzia sasa hadi Desemba tutafanya matamasha matano ya muziki wa dansi, kwani imeleta faraja dansi kumbe bado linapendwa na halijalala," amesema Hamisi Mwinjuma.