Jux: Mimi na mademu dam dam

Muktasari:
Mwimbaji Jux kawaandalia shoo mashabiki zake wa kike ambao hupata wakati mgumu kumuona kwa karibu akiwa jukwaa.
Mwanamuziki wa Bongofleva, Juma Jux amefichua kuwa moja ya vitu vigumu kwake ni kuwa singo na ndiyo maana hana kawaida ya kuchelewa kuanzisha mahusiano mapya
Jux amesanuka hayo ikiwa imepita zaidi ya miezi miwili tangu aachane na aliyekuwa mpenzi wake, Mthailand, Nnayikaa, ambaye pia alikuwa naye muda mfupi baada ya kuachana na Vanessa Mdee.
“Mimi moyo wangu mdogo, siwezi kukaa muda mrefu bila mahusiano, hata safari hii nimejitahidi sana, mpaka mwenyewe najishangaa, sijui hata kwa nini imekuwa hivi” amesema.
Zaidi Jux ameweka wazi mapenzi yake kwa wanawake kiasi kwamba Agosti 29 atafanya shoo maalum ambayo wataruhusiwa kuingia wanawake tu. Shoo hiyo itakuwa na idadi maalum ya wahudhuriaji itafanyika Dar es Salaam, katika Hotel ya Hyatt.
“Nimeamua kufanya hivi kwa sababu licha ya kwamba nina mashabiki wa kiume pia, lakini wengi zaidi ni wa kike na wamekuwa wako na mimi katika e kila nyakati.” ameeleza.
Pia amesema sababu zingine zilizofanya yeye na timu yake waje na wazo hilo la shoo ya wanawake tupu inayoitwa “King of Hearts” ni kuwapa nafasi mashabiki zake wengi ambao ni wanawake wanakosa fursa ya kuhudhuria katika matamasha yake ya mchanganyiko kwa sababu za kimazingira.
“Kwa mfano, wanaume wana nguvu na uwezo wa kulazimisha kupata nafasi za kukaa mbele karibu na jukwaa, lakini wanawake wanashindwa kwa hiyo katika shoo hii itakuwa fursa ya kuwa nao karibu bila kizuizi chochote”anasema Jux.