TASWIRA YA MLANGABOY : Wanachama mabadiliko katiba Yanga yasimlenge mtu

Friday February 7 2020

Wanachama mabadiliko katiba Yanga yasimlenge mtu,Uongozi wa Yanga,mwenyekiti Dk Mshindo Msolla, wadhamini wa Yanga, GSM,

 

By Andrew Kingamkono

Uongozi wa Yanga chini ya mwenyekiti Dk Mshindo Msolla umeitisha mkutano mkuu wa dharura wa wanachama wake Februari 16, 2020.

Katika mkutano huo moja ya ajenda kubwa zaidi ni suala la mabadiliko ya katiba yake ili kuifanya Yanga kwenda kisasa katika mfumo utakaoweza kuwa na tija kwa klabu hiyo kongwe.

Wakati mkutano huo ukiitishwa tayari wadhamini wa Yanga, GSM wamemleta mtaalamu kutoka Ureno Antonio Pinto kutoka Benfica kuja kutoa mafunzo ya namna bora ya kufikia lengo hilo.

Hakuna ubishi uamuzi wa GSM kumleta Mreno Pinto kutoa elimu na kuonyesha njia nzuri ya kupitia ili kuleta tija kwa suala hilo ni jambo la kusifika na kulitakia kheri.

Hata hivyo katika mkutano mkuu huo viongozi wa Yanga wanapaswa kutumia akili ya ziada na kutoa elimu ya kutosha kwa wanachama hao wakati wanapokwenda kufanya mabadiliko ya katiba hiyo.

Kwa sababu katiba ya Yanga ilishafanyiwa mabadiliko tangu 2010, ya kuifanya timu hiyo kuwa kampuni inayojitegemea japokuwa tatizo lilikuwa ni utekelezaji wa katiba hiyo.

Advertisement

Katiba ya Yanga ya 2010 inayotambuliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Baraza la Michezo Tanzania (BMT), ibara ya 56, ibara ya 56, ibara ya 56 inatambua suala la klabu hiyo kubadilika kuwa kampuni ya umma na siyo mali ya mtu mmoja au kikundi.

Ibara ya 56 yenye kichwa cha habari, Kampuni ya Umma ya Yanga inaonyesha jinsi klabu hiyo itakavyofuata utaratibu wa kubadilika na kuingia katika mfumo wa kampuni.

Ibara ya 56 (1), inaeleza kuwa kutakuwa na kampuni itakayojulikana kama Young Africans Corporation Limited itakayosajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni ikiwa kampuni ya umma yenye hisa.

Ibara ya 56(2), “Wanachama wote ambao katika tarehe ya marekebisho ya katiba ya mwaka 2007 wako hai, watakuwa, kwa nguvu ya uanachama wao, wanahisa katika kampuni kwa kiwango cha idadi ya hisa watakazopata kwa mujibu wa mwafaka wa Yanga uliofikiwa Juni 6, 2006.

Ibara ya 56 (3) inasema, “Klabu itamiliki hisa zilizo sawa na asilimia hamsini na moja (51) ya hisa zote zilizopo katika kampuni.

Ibara ya 56 (4) inasema,” Mkutano mkuu wa uchaguzi utachagua wanachama wawili ambao siyo miongoni mwa viongozi wa klabu kuwa wajumbe wa bodi ya wakurungenzi wa kampuni kwa ajili ya kuwakilisha masilahi ya klabu kwenye kampuni.

Kutokana na hali hiyo hakuna shaka kwamba Pinto atakuwa amepewa muogozo huo wa katika ya awali ili atakapokuwa anategeneza mpango wake anajua ni njia ipi ya kupita.

Lakini wanachama wanatakiwa kujua mapungufu ya Katiba ya 2010, katika kuifanya Yanga kujiendeleza wenyewe ili wanapofanya mabadiliko ya katiba mpya wajue ni wapi wanakwenda.

Changamoto ninayoiona kilichokwamisha kufanikiwa kwa mapendekezo ya katiba ya 2010, bado yapo hivyo kunahitajika elimu ya kutosha kwa wadau wote wa Yanga ili mapendekezo ya Katiba ya 2020 yawe na tija.

Mkutano wa Februari 16, usibadilishe katiba ya Yanga kwa lengo la kulenga kikundi au mtu fulani kwa vile ninavyoijua Yanga hakuna kitakachofanyika.

Nia njema ya GSM inaweza kugeuka uwanja wa vita kwa sababu nakuumbuka Yusuf Manji alisimamia mabadiliko ya katiba ya 2010 yakafanikiwa, lakini utekelezaji wake ulikuwa mgumu.

Baadaye Manji aliamua kuanzisha kampuni, Yanga Yetu Limited aliyoimiliki kwa asilimia 99 na kukodisha timu na nembo ya klabu hiyo kwa kipindi cha miaka kumi, hapo likazuka zogo hadi sasa.

Historia inaonyesha mwaka 1986 na 1987 kulitokea mgogoro uliozaa makundi ya uongozi uliojiita Yanga-Ukuta na wanachama waliojiita Yanga-Katiba.

Mgogoro mwaka 1996 baada ya kuzuka kundi la wanachama waliojiita Mau Mau ambao hatimaye ulikuja kuzaa makundi ya Yanga Kampuni, Yanga Asili na Yanga Academia.

Nasema haya kwa nia njema kabisa ili kuisaidia Yanga na mpira wa Tanzania ni wajibu wa GSM na uongozi wa Yanga kujifunza kwa migogoro yote inayotokea katika klabu hiyo inapofika suala la katiba.

Pia, wanachana wa Yanga wanajukumu la kuisoma vema katiba yao ya sasa ili wanapokwenda katika mkutano huo wawe na kitu wanachokijua ili kufanya marekebisho bora.

Wanachama wasifanye kosa na kuangalia shida za klabu za leo na kutatua tatizo la leo tu wakasahau kwamba mabadiliko hayo yanaweza kuwafunga kwa muda mrefu.

Ni lazima asilimia 51 ya wanachama ionekana na nafasi yao ipo wapi katika uamuzi, pia mwekezaji mkubwa haki na faida zake zinapatikana vipi. Pia, wanapaswa kujua thamani hali ya klabu yao kwa sasa je hiyo asilimia 49 ya wawekezaji anakuwa mtu mmoja au wawili au tatu vyote vijulikane wazi bila ya ujanjaujanja itasaidia kufukia lengo zuri la GSM na uongozi kuifanya Yanga ijitegemee kiuchumi.

Advertisement