Ubora wa ligi hutegemea soka la nchi husika

Saturday June 1 2019Ali Mayay

Ali Mayay 

By Ali Mayay

Siku zote elimu ya kijiweni huwa ni muhimu kwa kuwa vijiweni kuna mchanganyiko wa watu wenye elimu, taaluma na uzoefu katika sekta mbalimbali, hivyo hata mijadala ya soka huchangiwa na watu wenye weledi mkubwa.

Juzi nilikuwa kijiweni na jamaa zangu, ilitokea wakati kukawa na mjadala kuhusu maendeleo ya mchezo wa soka hapa nchini. Mjadala ulijikita katika tathmini ya ubora wa mechi za Ligi Kuu kwenye mataifa mbalimbali kwa kulinganisha na ligi yetu, ambapo mwezi huu ligi nyingi duniani zinaelekea ukingoni na kufungua dirisha la usajili wa wachezaji kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao utakaoanza Agosti.

Katika mjadala huo wadau wengi waliochangia, walisema ni vema na sisi tukawa na utaratibu wa kufanya kama wanavyofaya wenzetu wa Mataifa ya Ulaya, ambao kwa kiasi kikubwa hufanya tathmini ya msimu uliomalizika.

Taratibu zote hizo hufanyika na kuwekwa kwenye kumbukumbu kupitia maandiko, kwani njia bora ya kutunza kumbukumbu ni kuweka kwenye vitabu ndio maana Mataifa ya Ulaya yamefanikiwa kuzifanya ligi za mataifa hayo kuwa maarufu na kutokana na kufuatiliwa na watu wengi zaidi duniani kuliko ligi nyingine katika mabara yote na timu zao za taifa kufanya vema.

Katikati ya mjadala huo, kijana mmoja alisema hakuna kitu kipya ambacho hakijawahi kufanyika katika dunia ya sasa, hivyo ni vema tukaangalia wenzetu waliondelea kama vile Ligi Kuu ya soka England walifanyaje kisha tukaiga kila kitu kinachoweza kufanyika hapa Bongo.

Alivyosema hivyo tu, mzee mmoja aliinuka na kusema ukitaka kuiga ni lazima ujue malengo ya yule unayetaka kumuiga kwani inawezekana kabisa malengo yake yakawa ni tofauti na yale unavyodhania wewe.

Advertisement

Alisema Ligi Kuu England ina asilimia 24% tu ya wachezaji wa Kiingereza huku asilimia 76% wakiwa ni wageni, Liverpool ikiwa na wachezaji 10 wazawa kati ya 29, hivyo kuwa na asilimia 34% ya wazawa huku asilimia 66% wakiwa ni wageni.

Hali hiyo ipo kwa Tottenham ambayo ina wachezaji tisa wazawa kati ya 29 hivyo kuwa na asilimia 31 % ya wazawa huku asilimia 69% ikiwa ni wachezaji wageni na Chelsea ikiwa na wachezaji saba ambaoni wazawa kati ya wachezaji 28, hivyo kuwa na asilimia 25 ya wazawa huku wageni wakiwa asilimia 75%

Baadaye mjadala huo, kila mtu aliondoka, akiwa na mtazmo wake huku wengi wakisema ni bora kuanza na umaarufu kwanza kama walivyofanya Waingereza.

Maendeleo ya ndani yatakuja tu mbele ya safari kwani hata Uingereza pia katika mashindano ya kimataifa bado haijafanikiwa kama mataifa mengine. Ndio maana wanaendelea kupambana na kuhakikisha wanapata mafanikio.

Tanzania inayo nafasi ya kuendelea kujifunza kutoka kwa mataifa ya wenzetu ili kufikia hatua ambazo wenzetu wanatembea.

Katika hilo tunapaswa kuangalia uwezekano wa wachezaji wa kigeni katika timu zetu wako asilimia ngapi kwa kila timu.

Je, wachezaji hao wana faida gani katika kuendeleza na kukuza soka la Tanzania ili tuweze kupiga hatua mbele ya safari.

Kwa muda kumekuwa na mjadala mrefu kuhusu idadi ya wachezaji wa kigeni katika Ligi Kuu ya Tanzania. Wengine wakisema tuwe na wachezaji watano tu, kama ilivyopendekezwa kwenye Azimio la Bagamoyo.

Lakini wengine walikuwa wanataka kila timu iweze kusajili wachezaji wa kigeni saba tu.

Ukizingatia sasa klabu zenye uwezo wa kusajili nyota wa kigeni zinaruhusiwa kusajili wachezaji 10 ambao wanaruhusiwa kucheza katika mchezo mmoja.

Na kelele zinazopigwa na watu wanaotaka wachezaji wa kigeni wabaki kuwa 10 ni kwamba wanaleta changamoto kwa wachezaji wa ndani.

Je, tangu tumeanza kuruhusu wachezaji hao 10 kuna wachezaji wetu wemeweza kujifunza na kupata mafanikio makubwa kupitia kwao?

Mfano Emmanuel Okwi, Amiss Tambwe, Donald Ngoma na Thabani Kamusoko tangu wamekuja hapa Tanzania tunaweza kjivunia kuwa kuna wachezaji wanaoweza kufikia viwango vyao? Hilo ni suala la kutafakari na kufanya uamuzi wa maana kuhusu mustakali wa soka letu kama unaweza kuendelezwa kutokana na idadi ya wachezaji wa kigeni wanaokuja nchini.

Au tunaweza kubaki tu na umaarufu kwa ligi yetu kujaza wachezaji kutoka kila nchi katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wakati timu yetu ya taifa ikiwa inasuasua katika kupata mafanikio. Nasubiri mrejesho kutoka kwenu.

Advertisement