STRAIKA WA MWANASPOTI : Nawapa siri ya kuwa kocha mzuri, fanya hivi

Wednesday October 30 2019

Kocha,Liverpool FC,Van Dijk ,Kocha jurgen Klopp ,tuzo ya mchezaji bora Ulaya,Chelsea FC,Man United,

 

By Boniface Ambani

Mengi huongewa sana pale kocha wa kigeni anapotua kwenye nchi yoyote kuifundisha klabu ya nchi husika.

Wengi hufika mbali na kuwaambia ukweli juu ya klabu, mfano ataambiwa umerithi klabu yenye wachezaji wabovu na wenye viwango vya kawaida, hivyo tunakupa mikoba hii kuhakikisha jahazi linaibuka kwani lilikuwa linazama.

Hiki ndio kipindi kikubwa makocha hupitia na utakuta timu inafungwa kila mara.

Hata hivyo, kwangu ni tofauti. Ujio wa kocha kwenye tiomu mpya huwa nautazama kwa mtazamo na nawaambia makocha wa aina hiyo, wasiingiwe na kiwewe, shughuli hii sio ya kufanya kwa haraka.

Cha kwanza ni lazima ukutane na wachezaji na kuwapa nafasi kwenye mazoezi ili kujua uwezo wao na kujua ni aina gani na nani utamtumia ili kuweza kuisimamisha timu inayoonekana kutaka kuzama.

Lazima uanze kwenye upande wa beki na kuchunguza kiundani kikosi chako na kufahamu eneo hilo linataka nini ili uweze kupaimarisha endapo kuna mapungufu makubwa na mwisho uunde safu imara ya kusaidia kuokoa meli inayotaka kuzama.

Advertisement

Hapa sasa unaweza ukasjili wachezaji sita kwa maana ya golikipa, walinzi wa pembeni wawili, walinzi wa kati wawili, na kiungo mkabaji mmoja ambao kwa namna moja au nyingine ni muhimu kuwepo kikosini.

Hao ni lazima kwa vyovyote vile uwafanyie kazi wiki ya kwanza yote kabla haujafikiria kuanza kutafuta washambuliaji.

Kumbuka lazima uimarishe kwanza safu yako ya ulinzi. Katika soka kuna usemi usemao. “Walinzi/mabeki na mlinda lango watakushindia mataji, washambuliaji ni wa kukushindia mechi tuu”.

Kwa hivyo inamaanaisha ni lazima uimarishe ngome ya ulinzi kabisa kabla ya kuanza kufikiria kutafuta washambuliaji. Iwapo utajaliwa kuangalia kikosi chako ndani ya wiki moja na ugundue huna wachezaji wanao kuridhisha, basi jambo la kwanza la kufanya ni lazima uingie sokoni utafute hasa mabeki kwa wakati.

Nikiwapa mfano mzuri tu. Wakati Manchester United ilikuwa inashinda mataji, ilikuwa na walinzi wakati wawili wazuri mno, Nemanja Vidic na Rio Ferdinand.

Ilikuwa ni kazi ngumu kuwapita watu hawa. Sasa itazame Man United kipindi hiki.

Pale Liverpool kuna Van Dijk na kwa sasa mambo yametulia pale Anfield. Ni kwa sababu wamepata kiungo ambaye ametuliza ngome hapo katikati na hana presha na Kocha jurgen Klopp kwa sasa ana furaha wakati wote kutokana na kazi nzito ya mshindi huyo wa tuzo ya mchezaji bora Ulaya.

Kwa sasa Klopp anachokitaka ni ushindi wa Ligi Kuu England na kwa nionavyo, msimu huu taji ni lake kwani mpaka sasa hajapoteza mechi hata moja ya ligi na ndio wanaoongoza kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Hata hivyo, kwa upande wa Manchester City, ngome yao ya beki naona kama imeyumba. Sijui kwa nini.

Hata hivyo, unaweza ukahusisha na kuondoka kwa mlinzi wa kati Vincent Kompany na tangu ameondoka ni wazi Pep Guardiola hajapata mpadala wake

Hadi sasa imeshapoteza mechi mbili msimu huu na hii inaweza ikawaponza mwisho wa msimu kwenye kuwania ubingwa. Tatizo kubwa liko kwa Manchester United na Arsenal. Ni wazi makocha Ole Gunner Solskjer na Unai Emery wameshindwa kupata mabeki bora wa kati.

Kwa upande wa kiungo mkabaji ukipata wachezaji mfano wa Patrick Viera na Ngolo Kante una uhakika wa kuisimamisha ngome ya kati vizuri, ingawa mara nyingi imekuwa ni nadra kuwapata lakini sio vibaya ukaingia sokoni kujaribu.

Baada ya kumaliza kuimarisha beki na kiungo sasa unahamia kwenye washambuliaji na shida kubwa ya makocha ndio hapa.

Wengi hukimbilia kununua washambuliaji na kuacha mabeki. Hakikisha unaanza na beki ili kuimarisha safu hiyo ndio mwisho umalizie na washambuliaji.

Natumai hapo nimewaibia siri ambayo wengi hawafahamu katika masuala ya kisoka. Unahitaji kuzuia kwanza. Hata nchi kabla ya kuenda vita inajitendea haki kwa kuweka vizuizi mipakani kote. Tukutane wiki ijayo.

Advertisement