MTAA WA KATI : Maurico Pochettino alipoamua kujifelisha makusudi

Wednesday June 5 2019

 

By Said Pendeza

SIO lazima kuwa na digrii kulijua hili. Haihitaji maarifa makubwa sana kutambua haukuwa wakati mwafaka. Lakini, Mauricio Pochettino ameamua kujifelisha mwenyewe. Kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya si kitu kinachokuja mara kwa mara hasa kama timu yenyewe unayoinoa ni Tottenham Hotspur.

Labda uwe Barcelona au Real Madrid. Hata huko pia kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya si kitu chenye uhakika wa kutokea kama asubuhi na jioni.

Hivyo, Pochettino alipaswa kuwa na heshima kwa fursa aliyopata ya kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Amefanya dharau. Ameponzwa na dharau yake.

Kwenye mchezo wa fainali, Pochettino amepuyanga, ameshindwa kufanya maamuzi sahihi. Unacheza fainali, tena dhidi ya kikosi bora kabisa kama Liverpool, bado unaingia uwanjani kufanyia majaribio wachezaji. Lazima uadhibiwe.

Ni kitu cha wazi kabisa, hakikuhitaji elimu ya ukocha kumtambua Harry Kane hakuwa fiti kuanza mechi hiyo.

Kama alihitaji kumtengenezea rekodi kuwa amecheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, basi angemwanzishia benchi. Kane hakuwa fiti.

Advertisement

Kwenye fainali, Pochettino alihitaji kuwa na mshambuliaji aliyekuwa kwenye utimamu wa akili na mwili.

Pengine, alikuwa timamu kiakili, lakini mwili ulikuwa bado. Ametoka kwenye majeruhi ya muda mrefu.

Hakucheza mechi yoyote kujiweka fiti. Kuingia moja kwa moja kwenye fainali hapo Pochettino alicheza kamari.

Jurgen Klopp aliingia kwenye mtego huo. Alimwaanzisha Roberto Firmino kwenye fowadi. Mbrazili huyo naye hakuwa fiti kwa sababu alikuwa majeruhi kwa muda mrefu.

Lakini, baada ya muda Klopp alilifahamu hilo na kumtoa Firmino akamwingiza Divock Origi, aliyekuja kufunga bao la pili la uhakika wa ubingwa.

Sawa, pengine Pochettino hakukurupuka kwenye uamuzi wake, labda aliwaza na kujiuliza sana kama amwanzishe Kane au asifanye hivyo, uamuzi wake wa kumwanzisha, lilikuwa kosa kubwa.

Hakuwa yule Kane aliyezoeleka, hivyo kina Virgil van Dijk na Joel Matip walikuwa na kazi nyepesi ya kuifanya.

Ningekuwa Pochettino ningeanza kilichocheza na Ajax. Ningewaanzisha Lucas Moura na Heung-min Son pale kwenye fowadi. Uharaka wa wachezaji hao ungesababisha matatizo makubwa kwa mabeki wa Liverpool. Alikuwa na Erik Lamela pia kwenye benchi. Alikuwa na Fernardo Llorente ambaye angeweza kuwamudu mabeki wa Liverpool wanaotumia nguvu. Lakini, wote hao Pochettino aliwaacha kwenye benchi na kuchagua kucheza fainali ya mchezaji asiyekuwa fiti. Mbaya zaidi alimwaacha kwa dakika zote za mchezo.

Hakujifunja kutoka kwa mpinzani wake, Klopp, ambaye alihitaji dakika 10 tu kwenye kipindi cha pili kumtoa Firmino.

Spurs ilikaa na mpira, lakini ilikuwa doro kwenye fowadi yake. Kane hakuwa kwenye zile harakati zake zilizozoeleka. Dele Ali na Christian Eriksen nao hawakuwa kwenye mchezo mzuri. Hilo pia lilikuwa tatizo jingine.

Hivi ndivyo Pochettino alivyoshindwa kuheshimu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo atasubiri kwa miaka mingi ijayo kurudi tena kwenye mechi kama hiyo kwa timu yake ya Spurs.

Hakutaka kuwafanya Arsenal wateseke, ambao pia tangu walipocheza fainali mwaka 2006 hadi sasa hawajawahi tena.

Tangu mara ya mwisho, Arsenal ilipocheza fainali ya michuano hiyo ya Ulaya, Manchester United imeingia fainali mara tatu, Chelsea mara mbili, Liverpool mara mbili. Hivyo, Pochettino alipaswa kutambua tu kwa timu yake kufika fainali ilikuwa zali la mentali, hivyo alipaswa kutumia silaha zake zote nzima kumalizia msimu vyema.

Amejifelisha mwenyewe. Lakini, yote kwa yote pongezi kwao Liverpool, pongezi kwa Klopp, ambaye alionekana kuhitaji kushinda fainali hiyo baada ya mwaka jana kushindwa mbele ya Real Madrid.

Klopp aliona amekosea kwa Firmino, akamtoa haraka kumwingiza Origi, aliyeingia kumaliza mechi na sasa ubingwa unasherehewa huko Merseyside.

Advertisement