MTU WA PWANI : Kina Mbwana Samatta, Wanyama waiamshe Cecafa

Muktasari:

Ni mashindano ambayo tangu enzi na enzi yamekuwa na mfumo uleule wa uendeshaji ambao umekuwa hauna matokeo makubwa na chanya kwa nchi wanachama na badala yake yamekuwa yakiishia kutia hasara vyama na mashirikisho ya mpira wa miguu yaliyopo katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Mashindano ya Chalenji yanayoshirikisha nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa mwaka huu yanaanza rasmi mwishoni mwa wiki hii huko nchini Uganda.

Unapozungumzia Chalenji, unaamanisha mashindano makongwe zaidi ya soka barani Afrika ambapo sasa yanatimiza miaka 93 tangu yalipoanzishwa mnamo mwaka 1926.

Safari hii mashindano haya yatashirikisha jumla ya timu tisa za Taifa zilizopangwa katika makundi mawili nazo ni wenyeji Uganda, Burundi, Eritrea, Somalia, Djibout, Tanzania Bara, Sudan na Kenya.

Awali mashindano hayo mwaka huu yalipangwa kushirikisha nchi 12 lakini ghafla, timu za Taifa za Ethiopia, DR Congo na Sudan Kusini zikatangaza kujitoa kwa sababu tofauti ikiwemo ukata na kubanwa na ratiba za mashindano mengine. Ikumbukwe kuwa kabla ya uamuzi huo, tayari taifa la Rwanda lilishatangaza kutoshiriki mashindano hayo wala yale ya wanawake chini ya umri wa miaka 17 lakini pia haikupeleka timu yake ya taifa ya vijana chini ya miaka 20 kwenye mashindano ya Cecafa kwa vijana wa umri huo na hata pia kwa mashindano ya wanawake yaliyomalizika wiki iliyopita.

Kujitoa au kutoshiriki kwa baadhi ya mataifa ambayo yalipaswa kuwemo hakupaswi kutazamwa kwa jicho la kawaida na badala yake tafakuri ya kina inahitajika kufanywa na Cecafa juu ya hicho kilichotokea.

Kwa taswira ya nje inaweza kuonekana mataifa hayo yatashindwa kushiriki kwa sababu ya ukata ama kubanwa na ratiba za mashindano mengine lakini kiukweli ni idadi kubwa ya mataifa yanayounda Cecafa hayayaoni mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na baraza hilo kuwa yana tija.

Ni mashindano ambayo tangu enzi na enzi yamekuwa na mfumo uleule wa uendeshaji ambao umekuwa hauna matokeo makubwa na chanya kwa nchi wanachama na badala yake yamekuwa yakiishia kutia hasara vyama na mashirikisho ya mpira wa miguu yaliyopo katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Kwa muda mrefu yameendelea kukosa wadhamini wa kutoa fedha zinazoweza kuboresha ufanisi wa uendeshaji wake na badala yake yamekuwa yakiendelea kutegemea fedha kutoka kwa mlezi ambaye ni Rais wa Rwanda, Paul Kagame na michango ya nchi wanachama.

Hiyo inapelekea kuwepo na zawadi kiduchu kwa washindi wa vipengele mbalimbali jambo linalopelekea nchi zikinai na zione kama kushiriki kwao ni sehemu ya kupoteza muda na rasilimali.

Hakuonekani kama kuna juhudi kubwa na za dhati ambazo zimefanyika za kuhakikisha kampuni kubwa ambazo ziko ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati zinashawishika kuwekeza fedha katika kuyadhamini mashindano hayo ili kuyapa thamani stahiki kulingana na ukongwe, ukubwa na hadhi yake.

Hii ni tofauti na mashindano yanayoandaliwa na kanda nyingine za soka barani Afrika ambayo yamekuwa na msisimko wa hali ya juu na yamekuwa yakifuatiliwa kwa ukaribu na kundi kubwa la watu katika maeneo mbalimbali duniani.

Pamoja na kutokuwa na umri mrefu kulinganisha na Cecafa, mashindano ya Baraza la Soka kwa nchi za Kusini mwa Afrika (Cosafa) na yale yanayoandaliwa na Umoja wa Vyama vya soka Afrika Magharibi (Wafu) yameonekana kupiga hatua kubwa na kuzinufaisha nchi shiriki.

Kwanza zimekuwa zikipata kiasi kikubwa cha fedha kwa zile ambazo zinafanya vizuri lakini zinapata faida nyingine ya kuwaweka sokoni wachezaji kutokana na uwingi wa mawakala ambao hujitokeza kuyafuatilia tofauti na ilivyo kwa Cecafa Chalenji.

Ndio maana timu ambazo zimetoka katika kanda hizo ni vigumu kuona hazishiriki kwa sababu zinafahamu kuwa zitapoteza fursa muhimu kupitia mashindano hayo.

Mashirikisho na vyama vya soka kwa nchi ambazo zinashiriki Cosafa na Wafu, yanakuwa yako tayari kutoa kila yaliyonacho ili kuhakikisna timu zao zinashiriki mashindano ya kanda hizo kwa sababu yanakuwa na uhakika wa kunufaika nayo.

Lakini hilo ni tofauti na hayo ya Chalenji ambayo licha ya kutokuwa na fungu kubwa la fedha, mfumo na uendeshaji wake umekuwa ni uleule kila kukicha na hakuna ubunifu mpya jambo linalowapa ugumu watu kuyapa uzito mashindano hayo.

Ni lazima sasa Cecafa ianze kujiweka katika daraja la juu na kuanza kwenda sambamba na kanda nyingine za soka barani Afrika.

Kama kina Mbwana Samatta na Victor Wanyama wamefanikiwa kula sahani moja na wachezaji kutoka Afrika Magharibi, Kaskazini na hata Kusini huko Ulaya, Cecafa inapaswa kuiga kutoka kwao.