MTAA WA KATI : Maisha yanakwenda kasi sana asikwambie mtu

Tuesday April 7 2020

Maisha yanakwenda kasi sana asikwambie mtu,Raheem Sterling,Anfield,LIGI KUU ENGLAND YASIMAMISHWA,MWANASPORT,

 

By Said Pendeza

MAISHA yanakwenda kasi. Mambo yanatokea kwa haraka sana. Kuna hili jambo la Raheem Sterling, litatokea?

Jambo la Sterling ni kurudi Liverpool. Itawezekana, haiwezekani ni kitu cha kukisubiri. Lakini, kitu hicho kinatafsiri kasi ya maisha.

Hii leo, Sterling anataka kuachana na Man City arudi Liverpool?

Kasi ya maisha. Miaka mitano iliyopita, Sterling alithubutu hata kugombana na Liverpool ili kutimiza ndoto za kwenda kuichezea Man City. Lakini, sasa miaka mitano tu, imepita anaelezwa mpango wa kurudi Anfield. Kweli maisha yapo kasi. Hilo lina maana kubwa kwamba, ubabe na utawala umehama.

Hakuna ubishi kwa sasa Liverpool ni kivutio cha kila mchezaji. Maisha yamebadilika. Lakini, kitu cha kujiuliza, je Liverpool wanamhitaji Sterling kwa sasa? Je, Man City si timu tena ambayo inaweza kutimiza matakwa ya Sterling au kile alichokuwa akikitaka kubeba taji la Ligi Kuu England ameshakitimiza, hivyo haoni tena sababu?

Ni jambo lenye maswali mengi. Lakini, yote kwa yote kinachotokea ni kasi ya maisha tu. Man City ya sasa iliyomfanya Sterling alazimishe kwenye kujiunga nayo, inaachwa pointi 25 na Liverpool. Inashindwa kufika mbali kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Liverpool yenyewe inabeba bila ya shida.

Advertisement

Jurgen Klopp anaweza kushawishika na hilo la kumrudisha Sterling. Anafahamu watu kama Xherdan Shaqiri wataondoka na mapengo yao ni lazima yazibwe. Kitu kama hicho kinachotokea kwa Sterling kwa sasa ndicho ambacho kimekuwa kikisemwa kuhusu Philippe Coutinho. Kwa muda mrefu anahusishwa na mpango wa kurudi Anfield.

Mambo ya wakati. Sterling na Coutinho wote walilazimisha njia zao za kutoka Anfield. Sterling wakati anakwenda Man City, alidaiwa kwamba hata Liverpool wangeweka mshahara wa Pauni 900,000 kwa wiki mezani, asingesaini dili jipya. Hilo ni jibu la wazi kwamba hakuwa tayari kuendelea kubaki kwenye timu hiyo.

Aliona Pep Guardiola ametua Man City basi kungekuwa na mambo mazuri huko. Alijua atakwenda Etihad kubeba ubingwa wa ligi na Ulaya.

Sawa haukuwa uhamisho mbaya kwake, kwani akiwa Man City ametimiza lengo la kubeba ubingwa wa ligi. Tena sio mara moja, amebeba mataji mawili.

Lakini, ghafla kule alikotoka Liverpool wamebadilika na kucheza soka la kiwango cha juu. Wanasumbua kila timu kwenye ligi msimu huu na msimu uliopita wametoka kubeba ubingwa wa Ulaya.

Wakati hilo likiendelea Anfield, huko Etihad mambo magumu zaidi, timu inakumbana na adhabu ya kufungiwa kucheza misimu miwili kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Man City wamekata rufaa, lakini wakishindwa hiyo ina maana watakuwa na misimu miwili bila ya soka la Ulaya, itakuwaje?

Pengine hilo ndilo linalomfanya Sterling afikirie kurudi Liverpool. Kwa sababu anafahamu ataendelea kutamba kwenye Ligi Kuu England kwa misimu kadhaa na kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya pia. Lakini, ukweli atakuwa na wakati mgumu kuwabadili mashabiki wa Liverpool. Wanamwona kama ni mtu anayepelekeshwa na mafanikio.

Mwenyewe amekiri kwamba ana mapenzi na Liverpool. Kuna ukweli kwenye hilo ni jambo analolifahamu mwenyewe.

Lakini, yote kwa yote hili linatoa tafsiri halisi ya jinsi maisha yanavyokwenda kasi.

Sterling anataka kurudi Liverpool. Coutinho anataka kurudi Liverpool. Neymar anataka kurudi Barcelona. Pesa na mataji si kitu cha maana kwao na kufikiria kurudi walikotoka, walikoona kwamba kuna vitu hawavipati.

Advertisement