MTAA WA KATI : Karibu Arteta ulingoni, tunasubiri utuduwaze

Muktasari:

Arsenal imepoteza ile hamu na uchu wa kutaka kushinda mechi. Hawajioni kuwa wao ni washindi tena. Lakini, hilo limetokana na matokeo yao ya miaka ya karibuni.

KARIBU mzigoni Mikel Arteta. Una kazi moja kubwa, kutuduwaza.

Sasa kazi ni kwake, utatuduwaza kwa namna ipi. Kuiporomosha zaidi Arsenal au kuipandisha juu kuliko hata alipoicha Arsene Wenger mara ya mwisho alipoondoka. Ni chaguo lake Arteta. Ukweli usiokuwa na kificho, Arsenal wapo vibaya. Tena vibaya kwelikweli.

Inahitaji muda mwingi wa kuirudisha timu kwenye ubora. Kitu kinachoisumbua timu hiyo si wachezaji.

Kama ni wachezaji, basi Arsenal ina kikosi kizuri sana. Kwenye timu yenye Pierre-Emerick Aubameyang, Alexandre Lacazette, Mesut Ozil, Granit Xhaka, Lucas Torreira unawezaje kupata matokeo ya kufungwa hovyo? Shida ya Arsenal ni saikolojia tu, morali na kuona kama vile wao ni watu wa kufungwa hovyo.

Arsenal imepoteza ile hamu na uchu wa kutaka kushinda mechi. Hawajioni kuwa wao ni washindi tena. Lakini, hilo limetokana na matokeo yao ya miaka ya karibuni. Kushindwa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu kadhaa iliyopita, kumewafanya Arsenal kuanza kujiona kama wao si timu inayoshindania vitu vikubwa tena. Ni maradhi ambayo yanawasumbua wachezaji wa timu hiyo.

Arteta sasa anahitaji kuliondoa hilo kwanza kwenye akili za wachezaji wake. Kuwarudisha kwenye ari ya ushindi na kutambua wao ni timu kubwa.

Kitu kizuri ni kwamba kwa miaka mitatu aliyokuwa na Pep Guardiola atakuwa amejifunza mengi hasa ya kuwafanya wachezaji kurudi tena kwenye morali na kupambana pindi mambo yanapokuwa magumu.

Hakuna ubishi, Guardiola alimwaamini sana Arteta. Taarifa zinasema kwamba ndiye fundi wa kusoma timu pinzani na kuisoma timu yake na kupata suluhu kitu gani timu yake inapaswa kufanya kushinda mechi.

Huo ndio ubora wake. Lakini, yote kwa yote atahitaji wachezaji wa Arsenal kucheza kwa ajili yake. Kuunga mkono kile anachokisema na kwenda kukifanyia kazi kwa vitendo ndani ya uwanja.

Baada ya kutua tu huko Emirates, ameweka wazi kwamba mchezaji ambaye hatakuwa tayari kukubaliana na falsafa zake, basi ataonekana hafai kuendelea kuwapo Arsenal. Safari ya kuelekea mlango wa kutokea itamhusu.

Anataka kumwona Ozil kwenye kiwango bora kwenye mechi zote. Sio Ozil wa Norwich mkali, lakini Ozil wa Man City hovyo. Wachezaji wajitolee kwa kiwango bora katika kila mechi.

Hicho ndicho ambacho Pep amekuwa akikifanya kwa wachezaji wake kuwasisitiza akiwataka wacheze kwa ubora muda wote na ndio maana wamepata mafanikio waliyopata.

Kitu kingine ambacho Arteta amekuja nacho Arsenal ni ile kumshirikisha kila mtu aliyepo Arsenal kuhusu timu.

Huko Man City, Guardiola aliifanya Man City kuwa ya kila mtu hadi mfagiaji kwenye timu. Man City iliposhinda na kubeba ubingwa, alijiona kuwa ni sehemu ya mafanikio hayo kwa sababu alishukuriwa kwa kuvifanya vyumba kuwa kwenye mazingira safi na wachezaji kutuliza akili yao kupata ushindi.

Hilo ni jingine ambalo Arteta ametua nalo Arsenal. Kwenye mazoezi yake ya kwanza, watu wote kwenye benchi lake la ufundi walihusika mazoezini, wakitoa maelekezo na kushiriki. Team work.

Kitu kingine kizuri kwake Arteta ni kwamba uchanga wake kwenye kiti hicho hatamulikwa sana na vyombo vya habari. Ataachwa ajaribu kila analoliweza kama anavyooachwa Frank Lampard huko Chelsea au Ole Gunnar Solskjaer katika kikosi cha Man United.

Makocha wote hao wanaonekana kuwa wanachanga, kwamba wanahitaji kupewa muda zaidi wa kuwekekeza falsafa zao kwenye timu.

Idadi ya mechi ambazo Ole amepoteza Man United na jinsi kikosi chake kinavyocheza, angekuwa kocha mwenye uzoefu kama Jose Mourinho au Carlo Ancelotti, angeshafunguliwa mlango wa kutokea muda mrefu sana.

Hilo ni jambo jingine litakalomfanya Arteta aende kuwa na muda mwingi wa kuitengeneza Arsenal yake anayoitaka. Tusubiri tuone kile atakachokuja kutufanyia.

Karibu Arteta utuduwaze kwa sababu kuna kitu kikubwa kuhusu yeye, alipita chini ya Wenger, kisha akafanya kazi na Guardiola, wote ni makocha wa pasi nyingi na mpira wenye urembo kwenye kuutazama.