MTAA WA KATI : Ballon d’Or, La Liga ni suti na tai tu

Tuesday December 3 2019

STEPHEN -Warnock - Ballon d’Or-Kylian -Mbappe-Liverpool- Real Madrid - Barcelona-

 

By Said Pendeza

STEPHEN Warnock anafikirisha. Amesema kitu kuhusu Kylian Mbappe na uwezekano wa kwenda Liverpool. Amesema hawezi kwenda.

Si kwamba Ligi Kuu England haivutii wachezaji wazuri. Si kwamba huko kwingine watalipwa pesa nyingi zaidi. Hapana, ni kwa sababu moja tu, Ballon d’Or.

Kila mchezaji, anapocheza soka la kiwango cha juu kabisa kipimo chake kikubwa ni kushinda Ballon d’Or.

Hicho ndicho kilichomwondosha Eden Hazard Chelsea.

Ndicho kitakachomwondoa Paul Pogba na ndicho kitakachomzuia Mbappe, Neymar na pengine Antoine Griezmann kwenda Ligi Kuu England katika kipindi hiki ambacho wanaamini wanaweza kubeba Ballon d’Or. Kuna ukweli kwenye hilo.

Kwamba Ballon d’Or inahusiana na Real Madrid na Barcelona. Mbappe kwenye kiwango bora kabisa huko PSG.

Advertisement

Imekuwa hivyo pia kwa Neymar, lakini inavyoonekana ni ngumu kubeba tuzo hiyo kama wapo nje ya ardhi ya Hispania. Neymar alikuwapo kwenye ardhi ya Hispania, lakini kwa muda huo alikuwa nyuma ya kivuli cha Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Sasa anataka kurudi huko kwenda kutimiza lengo lake la kunasa tuzo hiyo. Mbappe naye njia itakuwa moja ya kwenda kushinda Ballon d’Or.

Ndicho anachokisema Warnock ukitaka kubeba tuzo hiyo ama ukacheze Madrid au Barcelona.

Usiku wa jana Jumatatu kulikuwa na sherehe za kutolewa tuzo hizo huko Paris, Ufaransa.

Lionel Messi wa Barcelona alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kutamba kwenye tuzo hiyo mbele ya mshindani wake Virgil van Dijk.

Sijui kama Van Dijk wa Liverpool alishinda kuvunja utawala wa Hispania au Messi aliendeleza ubabe.

Huko nyuma, kabla ya mwaka 2008 ndipo tuzo hiyo ilikuwa ikinaswa na mchezaji asiyecheza soka lake Hispania. Lakini, baada ya hapo, kwa zaidi ya muongo mmoja, La Liga imetawala Ballon d’Or.

Ligi nyingine kubwa ya Ulaya kuwahi kutawala kwenye tuzo hizo ni Bundesliga. Ilipobeba mara sita mfululizo, lakini hiyo ilikuwa muda mrefu sana uliopita, miaka ya katikati mwa sabini hadi mwanzoni mwa themanini.

Bila shaka Messi atakuwa ameongeza pengo la La Liga kutamba kwenye Ballon d’Or. Mabao 45 na asisti 17 ndani ya mwaka mmoja wa 2019 zilikuwa zikimpa nafasi kubwa ya kushinda. Usiku wa Jumapili alifunga bao dhidi ya Atletico kunogesha sherehe yake ya Jumatatu kwenye tuzo.

Kwenye tuzo za usiku wa jana, Messi si peke yake aliyekuwa mchezaji wa kutoka kwenye La Liga.

Kulikuwa na wachezaji wengine saba, Hazard, Karim Benzema, Griezmann, Joao Felix, Marc-Andre ter Stegen na Frenkie de Jong.

Kila mmoja kwa kile alichokifanya ndani ya mwaka kilistahili kutajwa kuwania tuzo hiyo.

Kilikuwa ni kitu cha kusubiri tu, Ballon d’Or ingeendelea kutua kwenye La Liga kwa mwaka wa 11 mfululizo?

Kutokea kwa hilo kutafanya njia ya wanasoka wengi wenye ndoto za kuja kubeba tuzo hiyo siku moja, safari yao iwe ya njia moja tu, kwenda kucheza kwenye La Liga, ndiko inakopatikana tuzo ya Ballon d’Or.

Advertisement