VIBE LA WIKI : Kipindi cha wajanja wa mjini kupiga pesa ndo hiki

Saturday June 1 2019Joseph Damas

Joseph Damas 

By Joseph Damas

BONGO bana kuna kila aina ya watu unaambiwa. Kila mtu mjanja na hakuna anayetaka kuonekana mlugaluga hata kama kaingia mjini jana usiku.

Sio kwamba anapenda kuonekana hivyo, lakini aina ya maisha na utaratibu wa kuishi ndio unatusukuma kuwa hivyo. Si unajua tena, yaani hapa kwenye Jiji la Makonda unachotakiwa kuja na akili zako tu na usijali sana kuhusiana na tabia utazikuta hukuhuku.

Kikubwa ambacho unaweza kukifanya unapokuwa tayari umeingia Dar es Salaa ni kuchagua unataka kuwa na tabia gani, kisha unaanza nayo na maisha yanasonga. Ndio kwani kitu gani buana, Bongo kuna tabia nyingi sana ni wewe tu kuchagua kusuka ama kunyoa.

Sasa iko hivi. Soka ndio mchezo unaopendwa na watu wengi duniani kuliko michezo mingine yote duniani. Kutokana na hilo asikwambie mtu kwenye soka kuna fedha ndefu na kuna wajanja wamejiegesha huko kwa ajili ya kupiga hizo pesa.

Yaani kuna watu wametengeneza mrija na fedha inamwagika kama maji huku wakiwa wamekunja nne majumbani ama wamejiweka kwenye hoteli kubwa wakipanga dili. Kama unabisha shauri yako ama tumia dakika tano kuperuzi ishu za Mino Raiola ama Jorge Mendez ambao, wanaogelea kwenye utajiri wa maana kupitia soka.

Wenyewe hawachezi na pengine hawajui hata kupiga danadana, lakini wanasikilizwa na kupewa heshima kubwa na wachezaji wa maana kama Paul Pogba, Kocha Jose Mourinho, Cristiano Ronaldo na mastaa wengine kibao.

Advertisement

Wenyewe hawana kazi kubwa zaidi ya kupanga mambo na kuuza maneno. Yaani wanasimama mbele ya wachezaji na makocha kwa ajili ya kuwauza kwenda kufanya kazi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Wana maofisi kwenye nchi mbalimbali Ulaya na hupiga pesa mara mbili kwa mwaka, yaani miezi kama hii na ile ya Januari, ambako dili za usajili za wachezaji hufanyika. Anyway achana na kina Mino na Mendez ambao, ndio wamewafanya Pogba na Ronaldo kuwa na jeuri duniani kwa kuwatengenezea dili za maana za kuwapa utajiri.

Hapa Bongo nako kuna watu wamechangamka sana katika dili za usajili. Wako wengi lakini wanaovuma ni wachache ambao wamesimika mizizi huku wengine wakiwa bado nyuma nyuma, lakini wanapiga pesa ndefu tu. Sasa harakati za usajili wa wachezaji ndio zinazidi kupamba moto na wajanja hawa ndio wako kazini.

Wanajaribu kupitia njia walizopita kina Mino japo hawajazimasta sana...Si unajua shule tena inahusika sana hapa. Kwa sasa wajanja hawa wameanza kuhamisha wachezaji wakiwatafutia timu hasa zile zilizonona kama Simba, Yanga, Azam na KMC ambazo si hapa wachezaji wake wanapanda ndege na wanakula vizuri.

Hapa ndipo utaanza kuona watu wanajitokeza na kudai ‘wachezaji fulani nawamiliki mimi hivyo, kama mnawataka basi njooni mezani tuzungumze.’ Yaani misheni town ashakuwa wakala tena wa soka?

Siku zote hawakuwa wakifahamu mchezaji anakula nini na familia yake ama anasumbuliwa na majanga gani, lakini sasa hivi ndio wanajitokeza. Wajanja hawa wengi wanajua kuzoza na wakishaweka bando kwenye simu, basi kazi hufanyika kwa kasi sana na wakati mwingine hata mchezaji mwenyewe hamfahamu.

Hiki ndio kipindi ambacho wachezaji wanapigwa kwa kusainishwa mikataba ya hovyo kwa sababu ya kutofahamu na kuwa na uelewa mdogo wa masuala ya kisheria. Wapo wachezaji ambao wameshapigwa sana na wameanza kuwa wajanja kuwahusisha ndugu wa karibu ndani ya familia kusimamia masuala yao ya kisheria ikiwemo dili zote za usajili.

Lakini, wengine ambao bado hajashtuka wamekuwa wakipigwa sana asilimia 10 na kupigwa bao wakati wa kujadili maslahi na haki nyingine muhimu. Kwani, mnadhani kwanini Ibrahim Ajibu aliondoka Simba kwa hasira na kwenda upande wa pili kipindi kile? Sitaki kurudia mambo haya. Lakini, wajanja hawa pia hawawapigi wachezaji tu, hadi klabu zishakutana na haya majanga ya kuuziwa mbuzi kwenye gunia.

Yaani mchezaji analetwa hapa kwa mbwembwe zote lakini, hawezi hata kupiga danadana.

Wapo wasomi wengi ambao, wanaweza kuwa sehemu ya mafanikio ya wachezaji kwa kusimamia haki zote ili kudhibiti wimbi la wajanja ambao kila kukicha linazidi kuota mizizi kwenye sekta ya michezo. Haina kificho, wachezaji ama wanamichezo wengi elimu ni utata hivyo wanahitaji watu wa kuwaongoza kwenye masuala mbalimbali.

Ronaldo hajaingia darasani lakini kwa kutambua hilo ameajiri wataalamu ambao akili zao zinachemka ili kumtajiri na amefanikiwa sasa inakuwa vipi wewe ukwame. Amkeni nyie mnamalizwa.

Advertisement