STRAIKA WA MWANASPOTI : Huu ndio ushauri wangu kwa Yanga kuhusu Yikpe

Muktasari:

Kuna pia wale kwa kweli hawana lolote la maana walilofanya klabuni, na klabu zikaamua kuwaachilia katika dirisha hili dogo ili kuwapa nafasi wachezaji wengine kujaza mapengo ambayo wameyaacha. Hata hivyo, hasa nikigusia katika masuala ya usajili katika klabu ya Jangwani yaani Yanga, ni vizuri hasa katika usajili wa dirisha hili dogo wajaribu kutafuta wachezaji wenye hadhi.

NI mengi yamefanyika katika soka letu kanda ya Afrika Mashariki tangu msimu wa 2019/20 ulipong’oa nanga. Wachezaji walisajaliwa wapige shughuli yao.

Kuna wale kwa kweli walipiga shughli yao kikamilifu wakaondoka kutafuta lishe nzuri kwingine na kuna ambao walisalia kuendeleza shughuli za klabu.

Kuna pia wale kwa kweli hawana lolote la maana walilofanya klabuni, na klabu zikaamua kuwaachilia katika dirisha hili dogo ili kuwapa nafasi wachezaji wengine kujaza mapengo ambayo wameyaacha. Hata hivyo, hasa nikigusia katika masuala ya usajili katika klabu ya Jangwani yaani Yanga, ni vizuri hasa katika usajili wa dirisha hili dogo wajaribu kutafuta wachezaji wenye hadhi.

Wachezaji ambao kwa kweli wanastahili kupiga huo uzi wa kijani na njano. Nakumbuka mwanzo tu wa msimu nilijaliwa kuwa katika jiji kuu la Tanzania, Dar es Salaam, wakati Yanga ilipotambulisha wachezaji wake wapya kwa mashabiki wao.

Mechi ilikuwa ni kati ya Yanga na Kariobangi Sharks. Ni mechi ambayo nilipata fursa kamili ya kuweza kuitazama kuanzia mwanzo hadi mwisho. Sikufurahishwa na kikosi hicho kabisa. Nilitoa maoni yangu kama mchezaji aliyewahi kukipiga Yanga na vilevile kama mchambuzi wa masuala ya kisoka.

Nililaumu kikosi hicho kwa kukosa viwango kamilifu vya kuweza kufanya makubwa katika Ligi Kuu nchini Tanzania na pia mashindano ya Afrika. Wengi waliteta mitandaoni, lakini wale wachache walinisikiza, walikubali. Dirisha dogo la usajili ndio hili hapa. Ni dirisha ambalo lazima wale wachezaji wanaosajiliwa wawe wa viwango vya juu kabisa. Wachezaji hasa wa kigeni ambao wanaosajiliwa lazima wafanyiwe majaribio angalau kuthibitisha na kuhakikisha wako katika hali nzuri ya kiafya. Wachezaji wengi utakuta labda ni majeruhi na kadhalika. Labda viwango vipo chini mno.

Kwa hiyo ni lazima wachunguzwe. Yanga ipo mbioni kumsajili Yikpe kutoka Gor Mahia. Wazo langu ni kwamba lazima kocha wa Yanga akamfanyie majaribio kwanza.

Kulingana na uchunguzi wangu wa kindani ni mchezaji ambaye ambaye ana masharti mengi na klabu ya Yanga pia lazima iweke masharti yake mezani. Upande wa nidhamu, hasa ya mazoezi ni lazima nati zikazwe. Ni mchezaji asiye mbaya vile, lakini lazima ajue anakuja kufanya nini.

Majaribio ya wiki moja yanafaa kwake kabla ya kumsajili moja kwa moja. Viungo wachezeshaji wanaotafutwa lazima pia waangaliwe kwa karibu.

Usajili kama huu sio usajili tu, ni usajili ambao unafaa kusaidia klabu kwa ukubwa wake. Kumbuka unaziba ulegevu. Haufai kuleta ama kusajili wachezaji ambao pia watakuja kuua klabu kabisa uanze kuwaza kwamba afadhali hata ningebakisha wale walikuwepo. Muda bado upo hadi Januari 15.

Natumaini makocha ama jopo na ufundi litaweza kupata muda wa kumchunguza vyema. Kila la heri Dar es Salaam Young Africans na klabu nyingine zote ambazo zipo mbioni kusaka wachezaji kwenye dirisha hili dogo.

Nchini Kenya dirisha dogo litafunguliwa Januari Mosi hadi Januari 31. Kazi ipo kwa makocha. Yangu ni kuwatakia kila la heri. Siku njema.