TIMUA VUMBI : Hili la mabao ya ‘offside’ sasa limekuwa kero kubwa

Muktasari:

Timu kugoma kuingia vyumbani inaweza kuwa ni jambo la kawaida kwa maana ya kwamba sio geni kwani tumeshuhudia hata mechi za kimataifa zinazocheza nchini ama nje ya nchi timu hugomea kuingia vyumbani wakiwa na hofu ya kuhujumiwa kwa madai ya kupuliziwa dawa.

LIGI Kuu Bara inaendelea ambapo ni mzunguko wa pili sasa, Simba ndio wanashikilia usukani wakifikisha pointi 50, Azam wanafuata wana pointi 37 huku Yanga wakishika nafasi ya tatu ambapo wamekusanya pointi 31 kabla ya mechi yao ya jana Jumatano dhidi ya Lipuli FC.

Mechi za msimu huu zimekuwa na malalamiko mengi yanayoelekezwa kwa waamuzi katika kufanya maamuzi yao wakati wa mechi husika, kwani asilimia kubwa ya timu hulalamika mara mechi zinapomalizika.

Achana na tuhuma zinazotolewa pindi timu zinapogoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji.

Hizi ni tuhuma ambazo hazijathibitishwa zaidi ya kuzungumzwa tu na hakuna aliyesikika kufuatilia hilo na kuthibitisha zaidi ya kuona faini hutolewa kwa baadhi ya timu zinazogoma kuingia kwenye vyumba hivyo.

Timu kugoma kuingia vyumbani inaweza kuwa ni jambo la kawaida kwa maana ya kwamba sio geni kwani tumeshuhudia hata mechi za kimataifa zinazocheza nchini ama nje ya nchi timu hugomea kuingia vyumbani wakiwa na hofu ya kuhujumiwa kwa madai ya kupuliziwa dawa.

Hilo ni kosa na ndio maana timu hupigwa faini, lakini ni nadra kuthibitisha tuhuma hizo hata kama walalamikaji wakizisemea.

Ukiachana na hilo, ligi ya hapa nchini msimu huu unaoendelea umekuwa na aibu hasa kwa waamuzi kulalamikiwa kuwepo na vitendo vinavyoashiria baadhi ya timu kubebwa hasa kwa kupewa faida ya maamuzi yasiyo sahihi.

Simba ni miongoni mwa timu inayolalamikiwa zaidi hasa kwa mabao yao mawili kwenye mechi mbili tofauti likiwemo la Meddie Kagera dhidi ya Namungo waliposhinda bao 2-1 na John Bocco alilofunga

walipowakabili Polisi Tanzania na kuibuka na ushindi wa bao 2-1, mechi zote zilichezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba wanalalamikiwa juu ya mabao hayo mawili kwamba mwamuzi katika mechi hizo aliyakubali mabao hayo ambayo wachezaji waliyafunga ikiwa wameotea. Mwamuzi ndiye mtu wa mwisho kuamua kuwa kuna bao ama hakuna, hivyo mpira ukiwekwa kati basi hakuna namna ya kukubaliana na maamuzi yake.

Lakini si mabao hayo ya Simba pekee ndiyo yanalalamikiwa, kuna baadhi ya mechi pia zinalalamikiwa kuamuliwa ndivyo sivyo ikiwemo mechi ya Coastal Union dhidi ya JKT Tanzania ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mechi hiyo inalalamikiwa na mashabiki kwamba penalti waliyopewa Coastal ilikuwa ni kama kuibeba timu hiyo kwani haikupaswa kutolewa adhabu kama hiyo.

Tumewasikia makocha wengi wengi wakilalamika juu ya uamuzi unaotolewa na waamuzi hao kwamba unamiza baadhi ya timu pinzani zinapokutana iwe kwa kutambua sheria 17 za soka ama kutokuwa na uzoefu kwenye uchezeshaji wa mechi.

Lakini, kikubwa ambacho kinapigiwa kelele ni juu ya Simba ambao wanaonekana kubebwa kuliko timu zingine zote na yote hayo ni kwa vile tu ya ukubwa wa jina ndiyo maana makosa yanaonekana zaidi

kwani kila mmoja anaangalia Simba wanafanya nini kipindi hiki.

Mbaya zaidi hata wenye timu wenyewe hawafurahishwi na kiwango cha timu yao hivyo wanakuwa na hofu juu ya matokeo yao wenyewe kwamba wanashinda ila si kwa kiwango ambacho wachezaji walipaswa kukionyesha uwanjani kutokana na ukubwa wa Simba.

Hivyo basi, hofu ya Wanasimba pia huenda inachangia kwa kiasi kikubwa mashabiki kuwa na mashaka zaidi juu ya waamuzi kwenye mechi zao na ndiyo maana inaonekana ndiyo timu pekee inayobebwa kwa kiasi kikubwa.

Lakini, yote kwa yote wasimamizi wa soka nchini ambao ni Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Bodi ya Ligi (TBPL) wanapaswa kuwa makini na haya malalamiko kwani wanasema lisemwalo lipo na kama halipo linakuja.

Ni aibu kubwa waamuzi kuendelea kuboronga halafu wao wakakaa kimya pasipo kufanyia uchunguzi mkubwa wa nini kinasababisha waamuzi hao kuboronga maana huwa wanawapa adhabu za kuwaonya tu ikiwa na maana nao wamegundua tatizo, basi wanapaswa kukomesha tatizo kwa kujua chimbuko.

Chimbuko lao kama wanajua sheria na ni wazoefu basi kuna shida kwa waamuzi ama pengine waamuzi wanaowatumia kwasasa hawajui vizuri sheria za soka, hivyo wanahitaji kujifunza zaidi.

Kuepusha kero na fedheha kwa klabu na shirikisho na hata kwa waamuzi wenyewe basi inahitajika kuwepo na tiba ya moja kwa moja.