TIMUA VUMBI : Hili la Ruvu Shooting na Prisons lijadiliwe kikanuni

Thursday February 13 2020

mechi ya Ruvu Shooting na Prisons,Uwanja wa Mabatini ,a gari la wagonjwa uwanjani,

 

By Mwanahiba Richard

JUZI mechi ya Ruvu Shooting na Prisons iliyokuwa ichezwe kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani haikuchezwa kutokana na wenyeji kushindwa kupeleka gari la wagonjwa uwanjani kwa zaidi ya dakika 30.

Timu zote ziliingia uwanjani na kusubiri mchezo huo kuanza kwa zaidi ya dakika 30 ambapo gari hilo liliingia baada ya dakika ya 35 ambapo ni kinyume cha kanuni za ligi hiyo.

Kanuni (2.12) inaeleza wazi kwamba kila klabu ya Ligi Kuu ina wajibu wa kuhakikisha linakuwapo gari la wagonjwa (ambulance) na vijana waokota mipira (ball boys) uwanjani katika kila mchezo wake wa nyumbani timu yake inapocheza. Iwapo huduma hizo hazitakuwapo, msimamizi watazuia mchezo kuchezwa na timu mwenyeji itapoteza mchezo huo.

Kwa maana hiyo timu ngeni itapaswa kupewa ushindi wa pointi tatu na magoli matatu ambapo Prisons ilitakiwa ifanyiwe hivyo.

Taarifa zinaeleza kwamba, baada ya mwamuzi kuingia uwanjani na kukagua timu hakuona gari la wagonjwa ndipo alipomfuata kamisaa wa mchezo huo kumweleza ambapo walichukua jukumu la kuwauliza wenyeji kuhusu hilo.

Jibu walilopewa ni kwamba gari hilo la wagonjwa lipo na kuonyeshwa gari aina ya pickup ambapo mwamuzi alilazimika kwenda kulikagua na kubaini kwamba halikuwa gari la wagonjwa hivyo alirudi kutoa taarifa kwamba asingeweza kuendelea kuchezesha mechi hiyo kwasababu hapakuwa na gari la wagonjwa jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za ligi.

Advertisement

Imeelezwa kwamba baadaye ikiwa ni dakika ya 35 gari hilo la wagonjwa liliingia uwanjani lakini tayari mwamuzi alikuwa amewaita viongozi wapande zote mbili, Ruvu na Prisons wakiwamo manahodha wa timu hizo.

Kikao hicho cha muda mfupi kilikuwa ni kupewa uamuzi wa mwamuzi huyo kwamba hataweza kuchezesha mechi hiyo kwa mujibu wa kanuni huku mwamuzi huyo akimweleza kamisaa wa mchezo ambaye pia aliliridhia uamuzi huo.

Baada ya uamuzi huo imedaiwa kwamba uongozi wa Ruvu ulitoa sababu ya kwanini gari lilichelewa kuingia uwanjani ikiwa na maana kwamba Prisons walitoa ‘fair’ mechi ipangwe siku nyingine ambapo sababu yao ni kwamba gari lilipeleka mgonjwa.

Kauli hiyo ya Ruvu ilikuwa ni kama kujikanganya wenyewe kwani mwanzo walisema gari lipo na walimwonyesha mwamuzi huyo pickup ambayo ilikataliwa kwamba si gari la wagonjwa na baadaye wakaja na kauli nyingine kuonyesha kwamba hawakuwa na uhakika na kile walichosema mwanzo ama walivurugwa kupokwa pointi.

Msimamo wa Prisons kwenye kikao hicho imedaiwa waligoma kutoa ‘fair’ na kwamba waache kanuni ifanye kazi kutoa maamuzi halali kwao na ndicho kitu wanachokisubiri kutoka Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka nchini (TFF) ambao ndio walioweka kanuni hizo.

Kikubwa ni kwamba, sioni sababu ya kupepesa macho kwenye hili, maana liko wazi na kila mdau anafahamu, uzembe wa watu wachache usiwagharimu wengine, kikao kitakachokaa kuamua hili kutoa uamuzi sahihi kwa mujibu wa kanuni kama zilivyofanyiwa baadhi ya timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL)

Kanuni zimetungwa, mwamuzi ameamua kwa kufuata kanuni, sidhani na sitegemei kama kutakuwapo na upindishwaji wa kanuni juu ya hilo, huu mpira sasa unapaswa uendeshwe kwa kuzingatia kanuni na sheria zake zile janja janja za kubebana sasa siziwepo kila mmoja avune kile alichokipanda.

Hivi karibuni TFF imeshuhudiwa ikitoa adhabu kwa waamuzi wanaoboronga kwenye mechi hivyo hata hili linapaswa kusimamia kanuni hiyo maana mwamuzi na kamisaa wote walikubaliana kwa mujibu wa kanuni kuwa mchezo huo hauwezwi kuchezwa kwasababu wenyeji walishindwa kupelekea gari uwanjani kwa wakati.

Mbaya zaidi wenyeji walipoulizwa kabla walionyesha pickup kuwa ndilo gari la wagonjwa kitu ambacho si sahihi na ndiyo maana mwamuzi aligoma kuwa pickup hiyo haiwezi kuwa gari la wagonjwa, hivyo Ruvu ni kama walitaka kudanganya na walikuwa hawajafanya maandalizi mapema ya kuwa na gari la wagonjwa.

Sioni sababu za kuipangia siku nyingine hiyo mechi bali hapo ni kutoa uamuzi wa kikanuni maana kama Ruvu walikuwa na sababu ya msingi basi hakukuwa na haja ya kutamka mara ya kwanza kuwa gari la wagonjwa lipo na kuonyesha pickup.

Nadhani kama Ruvu wangekuwa wanahitaji ‘fair’ basi wangetoa taarifa mapema kuwa gari lao limepata dharura hivyo litachelewa kuingia uwanjani kama lolote litatokea basi wanaandaa gari ambalo litakuwapo kwa muda hadi lile litakapowasili, hapo wangefikiriwa.

Advertisement