MTAA WA KATI : Ghafla tu Top Six kila mechi imegeuka fainali

Muktasari:

  • Lakini wa pili Manchester City hadi wa sita kuna tofauti ya pointi tisa. Hiyo ilikuwa kabla ya mechi ya usiku wa jana Jumatatu baina ya timu ya Pep Guardiola na Wolves. Kumbuka, Guardiola ndiye aliyesoma kwa sasa wachezaji wake wataichukulia kila mechi ni fainali.

KWENYE Ligi Kuu England kwa sasa, kila mechi ni fainali. Ni fainali, hasa kwa wale vigogo wa Top Six.

Hakuna anayekubali kuwekwa chini hapo. Kila timu itasaka ushindi kwa namna yoyote ile. Kutoka timu inayoongoza Liverpool hadi timu inayoshika nafasi ya sita, Manchester United kuna tofauti ya pointi 16.

Lakini wa pili Manchester City hadi wa sita kuna tofauti ya pointi tisa. Hiyo ilikuwa kabla ya mechi ya usiku wa jana Jumatatu baina ya timu ya Pep Guardiola na Wolves. Kumbuka, Guardiola ndiye aliyesoma kwa sasa wachezaji wake wataichukulia kila mechi ni fainali.

Kubwa wanalotaka ni kupunguza pengo la pointi lililopo baina yao na Liverpool ili zibaki kuwa nne. Kutoka timu inayoshika nafasi ya nne, ambayo kimsingi ndiyo ya mwisho kwenye kupata zile zitakazocheza Ligi ya Mabingwa Ulaya hadi kufika namba sita, kuna tofauti ya pointi sita.

Yaani hapo, Chelsea ilipo kwenye Top Four ikitoka sare mbili tu kisha wenzake, Arsenal na Man United zikishinda, basi mambo yanakuwa tofauti. Hiki ndicho kinachofanya kila mechi kwenye Ligi Kuu England kwa sasa ionekana kuwa ni fainali kwa vigogo hao sita.

Liverpool inajaribu kuikimbia Man City. Lakini, kiungo wa wababe wa huko Etihad, Mbrazili, Fernandinho amesema hakuna kitu kinachotia presha kama kuongoza ligi na wanaokufuatia wakiwa karibu. Kimsingi ni kwamba kwa sasa Jurgen Klopp ndiye mwenye presha kuliko makocha wengine wote wanaokimbizana kwenye mchakamchaka huo wa kutafuta nafasi nne za juu.

Presha hiyo ndiyo inayowafanya makocha pia kuwaza namna ya kuboresha vikosi vyao hasa kwenye kipindi hiki ambacho dirisha la usajili wa Januari likiwa wazi.

Maurizio Sarri wa Chelsea anafahamu wazi kwa sasa ligi imekuwa ngumu zaidi kuliko mwanzo. Suala la kutokuwa na uhakika wa mabao linamtia kizunguzungu na ndio maana anahangaika walau ampate straika Gonzalo Higuain kwenda kusaidia kumaliza tatizo hilo.

Presha yake kubwa ipo kwa Man United na Arsenal. Man United ndio inayomtisha zaidi kwa sababu tangu Ole Gunnar Solskjaer achukue timu hiyo, wachezaji wamekuwa wakicheza kwa kujitolea kwa zaidi ya asilimia 100.

Ole ameiongoza Man United kushinda mechi sita mfululizo tangu alipochukua mikoba hiyo mwezi uliopita. Wameshinda mechi tano kwenye Ligi Kuu England na moja kwenye Kombe la FA, ambako mechi yao ijayo kwenye raundi ya nne ya michuano hiyo wamepangwa kukutana na Arsenal huko Emirates. Juzi Jumapili ulikuwa mtihani wa kwanza kwa Ole wakati walipokwenda kucheza na Tottenham, lakini ushindi wa ugenini huko Wembley, umeonyesha kwamba kocha huyo yupo siriazi katika kuifanya Man United inakamata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Swali linakuja, nani ataondoka hapo kwenye Top Six? Kwa hali ilipofika kwa sasa, Top Four bado haina mwenyewe. Ligi ndio kwanza imechezwa mechi 22 na kuna mechi 16 hazijachezwa, ambazo ni sawa na pointi 48 hizo.

Liverpool kwa sasa inaongoza ligi ikiwa na pointi 57. Hiyo ina maana kwenye pointi hizo 48 zinazotafutwa hadi sasa, wao wamezidi pointi tisa tu. Kwa maana hiyo ligi bado mbichi. Ligi bado tamu.

Hakuna bingwa tayari na hakuna mwenye uhakika wa kuwamo ndani ya Top Four hadi mwisho wa msimu. Uhakika pekee wa kukufanya uendelee kubaki kwenye nafasi uliyopo ni kuendelea kushinda hadi mwisho. Lakini, kitu kigumu ni kwamba timu hizo za Top Six nyingine bado hazijamalizana zenyewe kwa zenyewe. Hapo ndipo panapokuja utamu halisi.

Mwanzoni, ligi ilionekana kama ni mbio ya Liverpool na Man City tu. Timu nyingine iliyokuwa ikitia presha ni Spurs.

Lakini, kasi ya Man United kwa sasa imeleta mvuto mpya kwenye mchakamchaka huo. Man United yawezekana isifikiriwe kwenye mbio za ubingwa, lakini bila ya shaka inawafanya makocha Klopp na Guardiola kukuna vichwa wakati watakapokabiliana na Ole.

Hiki ndicho kinachofanya mvuto wa ligi kukolea utamu, kuwa na hadhi ya fainali kwa kila mechi inayochezwa kwenye Top Six kutoka sasa hadi mwisho wa msimu.