Msikie Nchimbi, Umewahi kula ugali wa mafuta!

Muktasari:

  • VIPO vyakula vya aina mbalimbali duniani, lakini umewahi kusikia au kula ugali uliopikwa kwa kuchanganywa na mafuta ya kupikia?

VIPO vyakula vya aina mbalimbali duniani, lakini umewahi kusikia au kula ugali uliopikwa kwa kuchanganywa na mafuta ya kupikia?

Hata hivyo, katika harakati za kutafuta maisha mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Ditram Nchimbi amejikuta akikumbana na chakula hicho nchini Rwanda anakoichezea Etincelles FC inayoshiriki Ligi Kuu.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Nchimbi aliyeichezea Yanga kati ya 2020-2022 anasema baada ya kutua nchini humo kuanza maisha katika timu hiyo kilichokuwa kinamsumbua ni aina ya upishi akitolea mfano ugali wanauchanganya na mafuta, hivyo kwa mara ya kwanza alijikuta tumbo linamsumbua, ilhali maharage yanakaangwa kama njugu na supu yake inatengwa tofauti.

“Baada ya kula kwa mara ya kwanza ugali tumbo lilinisumbua nikaamua kujipikia mwenyewe kwa sababu nimepewa nyumba ya kuishi. Kuhusu lugha Kiingereza na Kiswahili havizungumzwi sana, wanatumia Kinyarwanda na Kifaransa,” anasema mchezaji huyo.

“Asilimia 80 ya vyakula vinavyopatikana Mkoa wa Mbeya na huku Rwanda vipo nikienda sokoni lazima niwaambie nahitaji mchele wa Tanzania, nje na hapo unapewa wa kwao ambao hauna ladha.”

Anasema timu anayoichezea ni ya halmashauri kama KMC na Mbeya City na anaamini angekuwa anacheza klabu kubwa asingekuwa anakumbana na changamoto ya chakula, kwani angekuwa anawekewa vyakula vya aina zote.

Nchimbi anasema hali ya hewa ya Rwanda haina tofauti na Tanzania kama ilivyo baridi la Mkoa wa Mbeya, lakini baada ya kutua nchini humo changamoto ilikuwa kwenye chakula na lugha wanayozungumza wakazi wa huko akimaanisha Kinyarwanda na Kifaransa. “Uendeshaji wa timu hatujatofautiana na Tanzania mazoezi ni mara moja kwa siku, baada ya kumaliza kila mtu anakwenda anakoishi, tunalipwa mshahara kwa wakati isipokuwa siku moja kabla ya mechi  ndio tunakutana kambini,” anasema.

 UKIZINGUA JELA

Kuna jambo ambalo straika huyo amejifunza na anajipa tahadhari kama binadamu anayeweza kufanya makosa kwa bahati mbaya akisema sheria za Rwanda zimenyooka na zinasimamiwa ipasavyo na ikitokea mtu kafanya kosa kwenda jela ni rahisi.

“Rwanda hakuna kujuana hata ukiwa na ndugu yako mkubwa serikalini kosa ni kosa ukizingua sheria inafuatwa bila kuangalia nani ni nani, hivyo  watu wanaishi kwa ustarabu,” anasema.

“Kwanza barabara zina taa kila sehemu ni nchi ndogo ila iko salama, kwani kila mtaa unakutana na askari, hivyo inakuwa vigumu kufanya uhalifu wa namna yoyote kwa sababu inakuwa rahisi kuonekana.

“Huwezi kumuona bodaboda (akiendesha) bila helment (kofia ngumu), akikamatwa na kama abiria wake naye hakuvaa wote wawili wanakwenda jela. Kwa ufupi wanajitahidi kuishi kwa taratibu na sheria za nchi.”

NIYONZIMA KAHUSIKA

Nchimbi aliyewahi kucheza kiungo wa zamani wa Yanga, Haruna Niyonzima anasema timu anayoichezea licha ya meneja wake kumtafutia dili hilo,  lakini Niyonzima alihusika kwa asilimia kubwa.

“Baada ya meneja kupata dili la timu hiyo Niyonzima akapata taarifa akawaaminisha mimi ni mchezaji mzuri, kwani kaka yake ni makamu wa rais wa timu hiyo, hivyo akanihakikishia nitaishi vizuri na ndivyo ilivyo naishi bila shida na isitoshe ni timu ya nyumbani kwao alikozaliwa,” anasema

“Niyonzima ni mchezaji aliye na moyo wa tofauti anapenda wenzake wafanikiwe. Pia amenifunza kuishi vizuri na watu mfano ningeishi naye vibaya Yanga huenda angeweza kusema nisisajiliwe.”

Anasema kaka yake Niyonzima alimwambia anahitaji akawasaidie timu isishuke na tayari hilo limefanikiwa na imesalia mechi moja msimu kumalizika, huku akiwa amecheza michezo minne na kufunga bao na asisti moja. “Sijacheza mechi nyingi. Wakati nakuja huku nilikuwa nimekaa nje kwa miezi sita, hivyo sikuwa kwenye ufiti unaotakiwa ingawa nilikuwa nafanya mazoezi binafsi. Ninachokifurahia timu imesalia Ligi Kuu nikiwemo kikosini, kuliko tungeshuka daraja kingekuwa kitu kibaya kwangu,” anasema.

KILIMO KAANZA ZAMANI

Nchimbi anasema kuna baadhi ya Watanzania wanapenda kumzungumzia mtu kwa mabaya na wakati flani yeye alikuwa anaposti picha za zamani zikimuonyesha yupo shambani au anaendesha bodaboda, akaanza kuzushiwa kwamba ameishiwa.

“Kilimo cha biashara nimeanza kukifanya kabla sijajiunga na Yanga. Kazi yangu ni kutafuta pesa siwezi kuangalia soka pekee ndio maana baada ya kumaliza shule nilikwenda kusomea ufundi magari nikatoka hapo kabla sijajiunga na Majimaji 2013 nikafanya kazi ya bodaboda,” anasema.

Anapoulizwa alikuwa anapata kiasi gani kwa siku wakati anaendesha bodaboda? Nchimbi anajibu: “Nilikuwa sikosi Sh7,000 na hapo nilikuwa napewa saa nne ya kupiga mishe. Nilipogundua watu wanapenda mabaya nikawa natuma picha mara nipo shamba, nipo kwenye bodaboda halafu nazifuta. Nikikaa muda kidogo natuma tena wanaanza kusema nimeishiwa, wakati wakinisema vibaya nafanya mambo mengine ya kimaisha.

“Nafanya mambo yangu kwa siri. Kilimo kinaendelea vizuri nina heka zangu huko mikoani nifanya shughuli hizo. Baada ya kuondoka Yanga maisha yangu yalikuwa safi tu, ila kwenye mitandao niliamua kuwapa furaha yao ya kile walichotarajia kuniona nacho.”

SOKA NA KONEKSHENI

Mchezaji huyo anasema asilimia kubwa ya vitu anavyomiliki vimetokana na soka na kuna wakati anapata koneksheni ya maisha ya watu ambao anakutana nao kwenye mchezo huo. “Nikitaka kuishi Dar es Salaam siwezi kupanga, nikienda Songea nakaa kwangu, nikienda Tunduru kijijini kuna kibanda, hivyo sehemu zangu  muhimu nimejenga vibanda,” anasema.

“Naipambania leo na kesho ya wanangu ndio maana nimesema hata mishe za boda nimewahi kuzifanya zamani. Nimesomea ufundi ili tu kujijenga kiuchumi.”

Akizungumzia tofauti ya Tanzania na Rwanda kisoka, mchezaji huyo anasema: “Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa, hivyo ni rahisi wachezaji kupata pesa nyingi na ndio maana wageni wengi wanapenda kucheza. Ushindani (pia) upo juu kwani wanajua wanaonekana na nchi mbalimbali, Rwanda udhamini wake ni mdogo na hakuna hamasa kama nyumbani.”