TASWIRA YA MLANGABOY : Bila ya Serikali kuweka bajeti, aibu timu za taifa ni yetu

Muktasari:

Wanariadha wa Tanzania wamefanya vibaya katika Michezo ya Afrika mwaka huu hiyo yote ni kwa sababu ya kukosa maandalizi mazuri tangu awali.

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amemuomba Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kuziangalia timu za taifa za michezo mbalimbali kwa kuweka bajeti.

Karia aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wadau mbalimbali wa soka nchini katika maadhimisho ya miaka miwili ya uongozi wake TFF.

“Bado vyama na mashirikisho ya michezo nchini yana changamoto ya fedha, hivi karibuni timu ya netiboli imekwama kusafiri (kwenda Afrika Kusini kwenye mashindano ya Afrika) kutokana na ukata.

“Bado vyama na mashirikisho mengi nchini yana changamoto hiyo, nimemuomba Waziri Mwakyembe ikiwezekana ajaribu kuyaangalia katika bajeti ijayo.”

“Sisi soka tunaendelea sababu ya hamasa ya mchezo, tunapata wadhamini na ruzuku tunayoipata tunaitumia vizuri, lakini kwenye vyama vingine vingi vya kitaifa fedha ni tatizo.” Mwisho wa kunukuu.

Hivi karibuni timu ya taifa ya mchezo wa netiboli Taifa Queens ilishindwa kwenda Afrika Kusini kushiriki mashindano ya Afrika kwa sababu ya kukosa fedha.

Wanariadha wa Tanzania wamefanya vibaya katika Michezo ya Afrika mwaka huu hiyo yote ni kwa sababu ya kukosa maandalizi mazuri tangu awali.

Kauli hiyo ya Karia imenikumbusha miezi minne iliyopita wakati ule Taifa Stars ilipofuzu Afcon 2019 Misri, viongozi wetu wengi wa kisiasa akiwemo wabunge wakiongozwa na Spika, Job Ndugai, Waziri Mwakyembe na wengine wengi walivyoisapoti.

Spika Ndugai aliporudi kutoka Cairo alisema jambo alilojifunza Afcon ni wenzetu kutenga bajeti kwa ajili ya timu za taifa na kuitaka serikali kupelekeza muswada bungeni ili waupitishe ili kusaidia maandalizi.

Suala la bajeti kwa timu za taifa ni jambo kubwa linalopaswa kutazamwa kwa umakini wa aina yake kama kweli tunataka mafanikio ya timu zetu.

Serikali haiwezi kukwepa jukumu na wajibu wa kuweka bajeti za timu za taifa na hii isiwe kwa timu za soka tu, bali kwa michezo yote.

Naamini inapofika suala la timu ya taifa si jambo la TFF, RT, TOC au shirikisho lolote, ni jambo la Tanzania na ndiyo maana wachezaji wale wanapoondoka wanakabidhiwa bendera ya taifa.

Hiyo ni ishara kwamba wanaokwenda kule wanabeba jukumu la taifa na wanamichezo hao ndiyo wanaobeba taswira ya taifa letu.

Ikiwa bajeti inasomwa bila ya hata senti moja kwenda kwenye michezo unategemea michezo itakua vipi hapa nchini, kwani tunavyofahamu vipaumbele ndio nguvu ya serikali ilipowekwa.

Wizara iliyopewa jukumu la kusimamia michezo inajifanya kama haitambui ugumu unaowakuta wanamichezo wa Tanzania wakati kila kitu kiko wazi na kinaonekana namna wachezaji wa Tanzania walivyo kwenye mazingira magumu.

Mbali na kutumia fedha ya bajeti, sidhani kama Serikali inashindwa kuwabana wawekezaji wanaochimba madini yetu na kuondoka nayo ili waisaidie japo kwa uchache sekta hii ili siku moja Tanzania iweze kuwa nchi ya mfano kwenye anga za michezo kimataifa.

Hatuna sababu ya kuvisukumia lawama vyama wakati watu walio juu yao wameshindwa kuonyesha kuleta msukumo wa wazi kwa kuwataka kubadilika na tukiendelea hivyo ni wazi tutakuwa na mabadiliko ya kisiasa kwa kuja na makabrasha mengi na mipango mingi, lakini utekelezaji ukiwa hakuna jipya.

Zipo timu nyingi zinakwenda kupambana nje kuliwakilisha Taifa, lakini nguvu kubwa inatoka katika vyama na siyo serikali sasa hili ni vyema likaangaliwa kwa mapana yake ili kuepuka kasumba ya yanapotokea mafanikio ndiyo viongozi wa serikali wanakuwa hodari kutafuta mashati mazuri na suti kwenda kuwapokea katika viwanja vya ndege wakati kumbe walikuwa na nafasi nao kutumia nafasi yao kuweza kuleta mafanikio zaidi.

Watanzania wanataka kuona msukumo wa kweli kutoka katika serikali yao kuwekeza kwa vitendo kwa kuanzia na kuweka bajeti kwa ajili ya timu za taifa ili wanamichezo wetu wanapotaka kwenda kushiriki katika mashindano ya kimataifa wasigeuke ombaomba au kama watoto yatima.

Naelewa mamilioni ya vijana wa Tanzania wanategemea michezo kuendesha maisha yao, ambapo bila wanasiasa au serikali kuisapoti michezo nchini au kampuni kujitokeza na kuwekeza kwenye michezo na rasilimali watu kukubali kufanikisha, hatuwezi kuona mabadiliko kwenye michezo.

Mwisho ni vyema Waziri Mwakyembe katika bajeti yake ijayo kuwe na bajeti za timu za taifa kwa sababu kuna mashindano mengi yanakuja mbele.

Hatuwezi kutegemea kupata mafanikio bila ya Serikali kupitia BMT kuweka bajeti kwa timu zetu katika maandalizi.