STRAIKA WA MWANASPOTI : Afrika Mashariki tusiamini katika mambo ya ushirikina

Muktasari:

  • Mtu atakudanganya atakupeleka kwa babu aende akutibu ili uwe kifaa hatari. Hamna kitu kama hicho.

SIKU ya leo nitaongelea kuhusu vitu ambavyo nimekuwa nikiviona vikifanyika katika mchezo wa soka.

Ushirikina umezidi kukita mizizi katika soka letu jambo ambalo nalikemea katika nguvu za Mwenyezi Mungu. Nimekuwa nikiona klabu kadhaa na baadhi ya wachezaji wakishiriki katika mambo ya ushirikina.

Ni upuzi mtupu. Ushirikina hauna nafasi yoyote katika soka wala mchezo wowote ule hapa duniani. Siri ya kushinda ni kufanya mazoezi kwa bidii, kusajali wachezaji wa viwango na kuweka miundo mbinu kamili ya kusaidia wachezaji kushinda mechi.

Mtu atakudanganya atakupeleka kwa babu aende akutibu ili uwe kifaa hatari. Hamna kitu kama hicho.

Hiyo ni saikolojia tu ambapo mtu anacheza na akili yako. Kama hujui kucheza soka hujui tu hata utafanye nini na utendelea kuwa hujui kama hutafuata miiko ya mchezo huo.

Tusijidanganye kuwa kuna kitu ambacho babu anaweza kukifanya na wewe ukaonekana kuwa bora uwanjani. Tunazunguma suala hili katika kipindi hiki ambapo timu za taifa nne za ukanda huu wa Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza zikiajiandaa kwenda Misri kushiriki Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON). Timu hizo ni Uganda, Tanzania, Kenya, Burundi Hatutegemei katika kuona mambo ya ushirikina kwenye fainali hizo ambapo Kenya na Tanzania zipo kwenye kundi moja.

Siri pekee ya kukufanya uwe bora ni kufanya mazoezi kwa bidii na kujiweka mbali na anasa. Nakemea jambo hili kwa sababu unakuta klabu ambazo zimekomaa tu katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki zinapenda kujihusisha na huu upumbavu wa kishirikina.

Utakuta klabu ama wachezaji kadhaa wanapelekwa kwa babu yao ili kuwapa dawa za kuweza kufanya vizuri uwanjuani.

Utakuta timu wakati wa kwenda uwanjani kucheza mechi unaambiwa eti haiwezi pita njia fulani. Ooh hawaezi ingia katika chumba cha kubalishia nguo uwanjani.

Utawakuta wachezaji wanabadilishia nguo sehemu nyingine tofauti na iliyowekwa kwa ajili ya kitendo hicho.

Ni upuzi mtupu. Upuuzi kabisa. Huwa tunafanya makosa sana kuendekeza mambo haya katika jamii zetu. Katika enzi hizi, karne hii bado wachezaji na viongozi wanafikiria kuhusu ushirikina? Shida tupu. Klabu nyingi zinafikiria kuwahusisha waganga kuwasadia kushinda mataji. La, haiwezekani. Kuna siri kadhaa ambazo zinasaidia timu kushinda mataji ambazo ni:

1: Kusajili wachezaji wenye viwango. Angalia Manchester City. Kocha Pep Guardiola amewasajili wachezaji wenye viwango vikubwa.

2: Tafuta kocha ambaye atakuja na benchi la ufundi. Angalia Manchestyer City. Pep Guardiola ni kocha ambaye kila klabu inamtamani kuwa naye.

3: Wafurahishe wachezaji.

Wape kila kitu wanachokihitaji ili wapate morali ya ushindi. Watapambana tu kama kutakuwa na mishahara posho za kuvutia.

4: Wape vifaa vya mazoezi na viwanja vizuri vya kufanyia mazoezi. Matokeo utayaona mwenyewe uwanjani. Kama timu ina vifaa na kocha mzuri kwanini isipate ushindi na kuzoa mataji?

Bado kuna mambo mengi tu ya kufanya kwa timu ili iweze kuwa bora na kufanya vizuri. Timu zetu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki zikiwa na viongozi makini, basi soka letu litaimarika na kuwa bora zaidi.

Kwa hivyo nawaomba wachezaji, viongozi na hata mashabiki wa soka waondokane na dhana za ushirikina kwa kutimiza majukumu yao katika mchezo wa soka. Wachezaji waachane kabisa na ujinga wa kukimbilia kwa mababu,ujinga wa kucheza na mahirizi viwanjani ama mazoezini, wakome kabisa.

Klabu zinapoteza pesa nyingi sana katika mambo ya kijinga kama haya, pesa ambazo zingelipwa kwa wachezaji na kuwaongezea morali ya kufanya vizuri zaidi. Angalia timu zinakataa kuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo kutokana na imani za kishirikina na kupigwa faini kubwa sana na vyama vya soka, hii ni akili gani sasa.

Binafsi nimecheza soka na nikamaliza, nimekuwa mfungaji bora mara kadhaa na sijawahi kutumia hivi vitu vya kishirikina. Nilimuweka Mwenyezi Mungu mbele na kuachana na mambo mengine. Ukimwamini Maulana Mwenyezi Mungu mengine yatatendeka kwa uwezo wake.

Lakini njia za ushirikina ni za shetani na hazifai. Utahitaji shetani akusaidie kwa shughli zako za kimaisha?

Congo (zamani ikiitwa Zaire) ilipeleka jopo la waganga mechi za Kombe la Dunia ikajikuta ikipigwa mabao 9-0 mbona ushirikina haukuwasaidia .

Nigeria iliwahi kupeleka waganga katika Kombe la Dunia lakini hata kwenye hatua ya makundi haikupita. Nakemea pepo la ushirikina katika soka letu. Hapa ni mazoezi tu. Viwango tu, basi. Mengine tuachane nayo. Hatuwezi kuomba Mungu atusaidie katika shughli kila siku na wakati huohuo tunakimbia katika shughli za ushirikina. Ni Mungu unaomba ama Ni shetani? Siku njema.