MTU WA PWANI : Tshishimbi ni mbabe wa ndani na nje ya Uwanja

Friday April 3 2020

 Tshishimbi ni mbabe wa ndani na nje ya Uwanja,USAJILI wa Papy Tshishimbi ,Yanga akitokea Mbabane Swallows,

 

By Charles Abel

USAJILI wa Papy Tshishimbi haukuwa na mbwembwe sana kwa mara ya kwanza pindi aliposaini mkataba wa kuitumikia Yanga akitokea Mbabane Swallows.

Alifika katika kipindi ambacho mastaa kadhaa wa Yanga ndio walikuwa wameteka hisia za mashabiki, wapenzi na wanachama wa klabu hiyo na yeye hakuhesabika kama miongoni mwa samaki wakubwa majini wakati huo.

Isingekuwa rahisi kwa Tshishimbi kuingia kibabe ndani ya Yanga ambayo ilikuwa ina kikosi kinachomjumuisha nahodha na beki kipenzi, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Thaban Kamusoko ‘Rasta’, Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Amissi Tambwe. Ikumbukwe kwamba ni wakati huo, Yanga ilikuwa imetoka kumnasa mshambuliaji kipenzi cha Simba, Ibrahim Ajibu ambaye usajili wake pekee ungetosha kuufunika ule wa Tshishimbi kwanza kutokana na kiwango bora cha nyota huyo ambaye kwa sasa amesharejea katika timu yake ya zamani lakini pia Yanga walikuwa wametoka kuwapa pigo watani zao, Simba. Baada ya kutamba akiwa na jezi ya Mbabane Swallows hasa katika mechi dhidi ya Azam FC pale Azam Complex ambayo ni wazi kwamba ndio iliwashawishi vigogo wa Yanga kumsajili, Tshishimbi aliingia katika himaya mpya ambayo ni tofauti na alikopitia.

Lakini msimu mmoja tu aliotumikia mkataba wake ndani ya Yanga, ulitosha kumtambulisha na kumfanya awe miongoni mwa nyota mastaa na wenye mvuto mkubwa katika kikosi cha timu yake huku akiwafunika hata wale ambao aliwakuta wakati anasajiliwa. Ikawa ni vigumu kwa mtu kuielezea Yanga pasipo kulitaja ama kulihusisha jina la Tshishimbi kutokana na mchango mkubwa ambao aliutoa kikosini akicheza katika nafasi ya kiungo wa ulinzi na wakati mwingine ushambuliaji.

Kwa sasa Tshishimbi ni staa mkubwa ndani ya kikosi cha Yanga na ndiye nahodha wao akirithi mikoba ya Ibrahim Ajibu ambaye anaitumikia Simba.

Kuna jambo ambalo linaendelea kumhusu Tshishimbi na klabu yake katika kipindi cha wiki mbili za hivi karibuni hasa likihusu hatima ya kiungo huyo ndani ya kikosi cha Yanga wakati mkataba wake wa mwaka mmoja ukiwa unaelekea ukingoni.

Advertisement

Yanga wanasumbuana naye wakihitaji aongeze mkataba mpya huku Tshishimbi mwenyewe akionekana kuwaringia kwa kuwatajia dau kubwa la ada ya kusaini mkataba na pia akitaka kupandishiwa kiwango cha mshahara tofauti na kile anacholipwa hivi sasa.

Tshishimbi anaamini kuwa anastahili kupata fungu kubwa la fedha kutoka Yanga kutokana na mchango na ubora alionao kikosini kulinganisha na wachezaji wengine wa timu hiyo.

Presha imekuwa kubwa kwa Yanga kuliko Tshishimbi mwenyewe na anaonekana hakuwa na haraka ya kusaini mkataba mpya kwa sababu anaamini anaweza kuvuna fungu kubwa la fedha kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi. Inasemekana jeuri ya Tshishimbi kuwadengulia Yanga imetokana na taarifa za kutakiwa na Watani wao wa Jadi, Simba ambao inatajwa kuwa wako tayari kumpa kiasi cha fedha ambacho anakihitaji ili awatumikie msimu ujao. Ni nadra sana kwa mchezaji anayechezea Simba au Yanga kujitokeza hadharani na kusema kuwa mkataba wake unaelekea ukingoni, hajasaini mkataba mpya na yuko tayari kujiunga na timu yoyote itakayompa maslahi mazuri lakini Tshishimbi alifanya hivyo tena kwa zaidi ya vyombo vitatu tofauti vya habari.

Huwa ni vigumu kwa mchezaji wa timu mojawapo kati ya hizo mbili kutamba hadharani kuwa anapenda na angejisikia faraja kucheza pamoja na mchezaji/wachezaji wa upande wa pili wa watani hao wa jadi lakini Tshishimbi bila woga amezungumza hilo pasipo hofu yoyote.

Kujiamini huku kwa Tshishimbi nje ya Uwanja ni matokeo ya kile ambacho amekuwa akikifanya uwanjani. Anafahamu fika kuwa Wanayanga wataishia kunung’unikia katika nyoyo zao lakini hawatothubutu kutaka aachwe au asipewe nafasi kikosini. Ametengeneza pengo kubwa la ubora baina yake na viungo wengine ndani ya Yanga hivyo anafahamu fika mabosi wa timu hiyo watapambana kusaka fedha za kumpa ili asaini mkataba mpya lakini pia wataishia kusonya pindi atakapozungumza mambo ambayo hawayafurahishi.

Lakini kama wangekuwa wanajiamini na wana viwango bora na kuishi maisha ya weledi, ingekuwa rahisi kwao kufanya haya ya Tshishimbi.

Klabu zetu zimekuwa hazina ujanja na zina utumwa kwa wachezaji wanaofanya vizuri ndani ya uwanja na kuwa vipenzi vya mashabiki lakini usitegemee kuona zikifanya hivyo kwa wale ambao viwango vyao ni vya kawaida.

Laiti Tshishimbi angekuwa anasotea benchi na kiwango chake ni cha kusuasua, ni Yanga ndio wangekuwa na jeuri mbele yake lakini kinyume chake yeye ndio anawaendesha. Kuna funzo hapo.

Advertisement