Watu kibao wajitokeza tamasha Sauti za Busara

Saturday February 15 2020

Watu kibao wajitokeza tamasha Sauti za Busara,tamasha la  Sauti za Busara 2020 ,

 

By Rhobi Chacha,Zanzibar

IKIWA leo ni siku ya pili tangu kuanza kwa tamasha la  Sauti za Busara 2020 visiwani hapa watu wengi hujitokeza kuangalia burudani kutoka nchi mbalimbali za Bara la Afrika.
Idadi  inaonekana  kubwa kutokana na wageni hao kuujaza uwanja wa Mji Mongwe tofauti na siku ya ufunguzi wa tamasha hili,  kwa wastani wa wageni  hadi sasa wanakadariwa kufika 9000.

Leo kuna uwezekano  mkubwa  idadi ya wageni kuongezeka zaidi  kutokana na wanamuziki  wa Tanzania The Mafiki na Wakazi  kutumbuiza kwani mara nyingi tamasha hili ikiwa siku ya wanamuziki Watanzania kupanda jukwaani huwa idadi ya wageni inaongezeka hasa kutoka Tanzania.

Kuna faida nyingi zinazopatikana kutokana na uwepo wa tamasha hili. Utalii wa makumbusho mbalimbali visiwani Unguja huingiza pato kubwa sanjari na wakazi wa Mji Mkongwe wa Zanzibar kunufaika na ujio wa wageni.

Burudani zinazotolewa na wanamuziki zinaonyesha kuwafurahisha watu waliohudhuria tamasha hilo  kwani kila apandapo msanii  jukwaani , watu hulipuka na  shangwe za kelele wengine kupiga miruzi huku wengine kufuatilia nyimbo zinazoimbwa na wanamuziki hao.

Wasanii waliopanda leo jukwaani ni Apio Moro wa Uganda, Blinky Bill wa Kenya , Pigment, Swahili Encounters Zanzibar /Various

Pia wasanii waliotumbuiza siku ya ufunguzi wa tamasha hilo ni FRA kutoka Ghana, Lulu Abdalla wa Kenya, Siti and The Band kutoka Zanzibar, TaraJazz wa Zanzibar na Thais Diarra wa Senegal.

Tamasha la Sauti za Busara ikiwa na kauli mbiu ya Paza Sauti, pinga unyanyasaji wa kijinsia limeanza  Zanzibar  Mji Mkongwe, Ngome Kongwe Februari 13 na litamalizika Februari 16 mwaka huu.

Advertisement