Wasanii wenye alama zinazojirudia videoni

Sunday August 9 2020

 

By KELVIN KAGAMBO

JAMBO ambalo unaweza kuwa na uhakika nalo kwa asilimia 90 kabla ya mechi ya Barcelona kuanza ni kumuona Lionel Messi akiingia uwanjani akiwa amevaa jezi namba 10 mgongoni. Hiyo ni sawa na ambavyo baadhi ya wasanii wakitangaza wanataka kuachia video ya wimbo, unaweza kuwa na uhakika kwa asilimia kubwa kuona jambo fulani ambalo alilifanya kwenye video zilizopita pia, amelifanya na humo pia.

Jambo hilo linaweza kuwa uvaaji fulani wa nguo au kutumia waigizaji fulani kwenye video, lakini mwisho wa siku matarajio yote haya yanatengenezwa na msanii mwenyewe kwa kurudiarudia kufanya jambo kiasi kwamba sasa linakuwa ni kama alama yake.

Kuna alama nyingi walizozitengeneza wasanii hawa, lakini chache kubwa ni:

HARMONIZE KUKAA TUMBO WAZI

Ni tabia aliyoianzisha tangu akiwa WCB. Hata hivyo hakuwa akiifanya kwenye nyimbo zote. Lakini tangu alipochomoka na kwenda kuanzisha Konde Gang, Mmakonde huyu amekuwa na kawaida ya kuimba akiwa tumbo wazi kwenye kila video ya wimbo wake alioutoa.

Tazama wimbo wake wa mwisho kuachia unaoitwa Mpaka Kesho, kisha tazama wimbo wake wa kwanza kuutoa akiwa nje ya lebo ya Wasafi unaoitwa Uno, halafu tazama nyimbo zote za katikati ya hizo utaona hili tunalolizungumza hapa. Tembo mwenyewe anadai anafanya hivyo sio kwa sababu anataka kuonesha ‘six pack’ zake, hapana, bali ni kwa ajili ya kujitengenezea alama fulani ya kisanii.

Advertisement

MPOTO KUTEMBEA PEKU

Katika moja ya intavyuu zake hivi karibuni, Mjomba Mrisho Mpoto alidai kuwa sasa ameanza kuvaa viatu kwa sababu anaona licha ya kupekua kwa muda mrefu, lakini bado kuna watu wameshindwa kumzoea na wanaamini anafanya hivyo kwa sababu za kishirikina - eti labda nd’o alivyotumwa na mganga wake.

Tangu anaachia video ya wimbo wake wa kwanza, Mpoto alionekana akitembea bila viatu. Mashabiki wakadhani ni swaga tu za wimbo huo, lakini matokeo yake kila video ya wimbo alioutoa kutokea pale uliendeleza utamaduni wake huo na sasa imekuwa mazowea.

Isitoshe, kutembea peku kwa Mpoto sio jambo analolifanya kwenye video za nyimbo tu, hapana, bali hata katika maisha halisi - mshairi huyu hana kawaida ya kuvaa viatu.

Akihojiwa na BBC Swahili takriban miaka minne iliyopita, alisema anafanya hivyo kwa sababu anaamini ndivyo asili inavyotaka kila binadamu awe.

“Nadhani nature inataka tutembee peku ili kutengeneza connection kati ya mwili wa binadamu na dunia (ardhi).” alieleza.

DIAMOND NA NDUGU ZAKE

Kwenye video ya wimbo wake wa kwanza kabisa wa Kamwambie Bibi yake na Diamond aliigiza kama ndugu wa mwanamke anayeutesa moyo wa Diamond. Kisha kwenye wimbo wake wa pili wa Mbagala akamtumia kaka yake anayeitwa Rommy Jones kucheza kama mwanaume tajiri aliyevunja penzi la Diamond na mpenzi wake kwa kumuona mwanamke wa Diamond. Kwa kipindi kile baadhi ya watu walidhani labda kwa sababu ni msanii mchanga kwa hiyo hakuwa na uwezo wa kulipa watu waigize kwenye video zake, lakini haikuwa hivyo, kwani mpaka sasa anaendeleza tabia hiyo.

Mwaka 2013 akiwa kwenye penzi la Wema Sepetu alimtumia mrembo kwenye video ya wimbo wa Moyo wangu, na pia amewahi kumtumia mama wa watoto wake, Zari The Boss Lady kwenye video zaidi ya moja, bila kusahau amewahi kumtumia mama yake kama moja ya waigizaji kwenye video, amewatumia mameneja wake mpaka mashemeji zake — kwahiyo kutumia ndugu kwenye nyimbo zake ni kitu ambacho unaweza kuwa na uhakika kwa hata asilimia 70 kuwa Diamond atakifanya kwenye video ya wimbo wake ujao.

MHE. TEMBA NA KIJITI MDOMONI

Unawajua watu ambao kila unapowaona utawakuta na toothpick mdomoni? Mh Temba ni mmoja wao, na video za nyimbo zake zinathibitisha hili.

Mwanzo, wakati anaanza muziki wake hakuwa na hii tabia, lakini ilianza kujitokeza taratibu na mpaka baadaye ikawa ni moja ya alama zake kiasi kwamba karibu kila video ya wimbo ambao jamaa yupo ndani lazima kuwe na ‘scene’ ambayo ataonekana na kijiti mdomoni.

Kwenye moja ya intavyuu alipoulizwa kuhusu tabia hii alidai ni kitu ambacho amekuwa akikifanya sio kwa sababu ya video tu, bali ni moja ya tabia zake hata katika maisha halisi.

“Niko hivyo, mara nyingi na kijiti mdomoni. Sijaanza kufanya kwenye video, ila sasa watu wanaonifahamu wakasema unajua hii ya kijiti inaweza kuwa staili yako mpaka kwenye video, nikaona kwanini isiwe hivyo.” alitolea ufafanuzi.

Advertisement